32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

OLE SOSOPI: BAVICHA HII TOFAUTI NA YA KATAMBI, HECHE

Mwenyekiti wa Baraza lam Vijana Chadema (BAVICHA), PAtrick Ole Sosopi, akizungumza katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari wa gazeti hili (MTANZANIA), Dar es Salaam hivi karibuni.

Na EVANS MAGEGE

PATRICK Ole Sosopi ni mmoja kati ya vijana wanaotumikia vema gurudumu la siasa za upinzani nchini.

Ole Sosopi ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha). Amepata kuwa makamu mwenyekiti wa baraza hilo ngazi ya taifa kwa takribani miaka mitatu.

Nafasi ya uenyekiti aliipata baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa baraza hilo, Patrobas Katambi, kujivua uanachama wa Chadema na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Novemba mwaka jana.

Gazeti hili limefanya mahojiano maalumu na mwanasiasa huyo na kuzungumzia masuala mbalimbali ya kisiasa, elimu na kijamii.

Pia ameelezea mtazamo wake juu ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo –Chadema, waliokihama chama hicho na jinsi Bavicha ilivyoipokea kauli ya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, aliyoitoa hivi karibuni ya kupongeza utendaji kazi wa Rais John Magufuli.

Endelea kufuatilia mazungumzo hayo…

MTANZANIA Jumapili: Ulikuwa  makamu mwenyekiti na sasa umechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bavicvha, vijana wa Chadema pamoja na wafuasi wa chama hicho wategemee nini kutoka kwako?

Ole Sosopi: Nimepata dhamana ya kuwa mwenyekiti na kabla ya hapo nilikuwa makamu mwenyekiti wa BAVICHA, nilichaguliwa Septemba 14, 2014.

Mwenyekiti wangu kipindi hicho, Patrobas Katambi, tulifanya naye kazi vizuri. Kilichotokea Watanzania wanakifahamu. Desemba Mosi mwaka jana kwa mujibu wa katiba yetu, ulifanyika uchaguzi kuziba pengo la mwenyekiti (Katambi) ambaye aliondoka kwa maana ya kukihama chama.

Katika uchaguzi huo ndio nikapata hii dhamana kwa kuchaguliwa na wajumbe wa kamati tendaji ya halmashauri kuu ya taifa.

Katiba inaruhusu kuwa nafasi ya uenyekiti inapokuwa wazi mwaka mmoja kabla ya uchaguzi, mkutano mkuu utakaimisha kamati tendaji ya Bavicha kufanya uchaguzi wa kuziba pengo hilo kwa kupata mwenyekiti na si kaimu.

Bavicha niliyoitumikia kama makamu mwenyekiti, kikatiba nilikuwa nafanya kazi ya kutumwa na mwenyekiti.

Kwa hiyo mtu mwenye wajibu mkubwa aliyekuwa anapaswa kulitumikia baraza wakati wote ni mwenyekiti kwa mujibu wa Katiba ya baraza letu, kwamba mwenyekiti ndiye mwenye mamlaka yote, makamu mwenyekiti anafanya kazi pale mwenyekiti anapokuwa hayupo au kuagizwa na mwenyekiti.

Kwa sasa namshukuru Mungu kuwa nimepata fursa rasmi ya kuwa mwenyekiti wa baraza hili taifa. Kimantiki ninaona nina kazi kubwa mbele yangu nikiwa kama mwenyekiti nakwenda kuongoza Baraza la Vijana, nafikiri baraza hili ndilo Baraza la vijana wengi kuliko mabaraza yoyote ya vyama vya siasa nchini.

Chadema tuna mashabiki, wanachama na wapenzi wengi ambao ni vijana, kwa sababu zipo tafiti zinazoonyesha chama chetu kinaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na vijana kuliko taasisi nyingine za vyama vya siasa.

Kwa hiyo naona fahari kuwa nimepata dhamana ya kuongoza baraza kubwa na lenye vijana wengi, lakini pia naamini baraza letu linakwenda kufanya kazi kama baraza kivuli la kundi la vijana Tanzania.

Kwa sasa naiona Bavicha imara ambayo nategemea kuiongoza. Kazi ya kwanza kubwa ninayopaswa kuifanya ni kuhakikisha Chadema inarudi katika misingi yake mikuu ya kuwa ni chama cha kupigania haki, kutetea wanyonge na makundi mbalimbali.

Sina maana ya kwamba tulipata kuondoka katika misingi yetu, la hasha! bali mwenyekiti aliyekuwapo, alilifanya baraza kuzorota.

Ikumbukwe kwamba nilikuwa na uwezo wa kumshauri kama makamu wake, lakini ushauri kwa kiongozi wako wa juu haina maana kuwa umemlazimisha kwa mawazo yako, bali anaweza kukusikiliza au asikusikilize.

Kwa hiyo ninatambua kuwa nakwenda kuongoza, Baraza linategemea uhai wake kuifanya Chadema kusonga mbele.

Kazi kubwa ninayopaswa kuanza nayo ni kuwa na data za idadi ya vijana ndani ya Baraza nchi nzima. Kwa muktadha huo, nakwenda kufanya kanzidata za vijana nchi nzima, tayari nimekwishatoa maagizo hayo na kazi imeanza.

Pia, nategemea kuwa na makundi mbalimbali ya vijana walio na taaluma tofauti. Sitegemei kuwa na baraza la vijana ambalo litafanya siasa wakati wote, kwa sababu kuna wakati tutahitaji kusaidia jamii, kisheria na hata katika sekta ya afya.

Bila itikadi za vyama tutawasaidia watu wenye uhitaji wa sheria, iwe ni mahakamani au sehemu yoyote.

Tuna madaktari wengi wanaotaka kujitolea kwa jamii, mfano kuna watu hawana uwezo wa kwenda hospitali kutibiwa hata tu kupima mapigo ya moyo au macho, sisi Bavicha tunaweza kutoa taarifa kwa Serikali na vyombo husika waturuhusu kupitia madaktari wetu kuhudumia jamii walau kwa kutoa vipimo vya magonjwa mbalimbali bure.

Kwa hiyo zipo taaluma nyingi ndani ya Bavichs, tutatengeneza kanzidata ya wataalamu wa kila taaluma na ni lazima tufahamiane ili waweze kufikisha mchango wao katika jamii.

Ndani ya hii miezi sita ya kuandaa kanzidata ya idadi ya vijana nchini, nitafanya ziara nchi nzima kwa lengo la kukutana na vijana katika maeneo mbalimbali wanakofanyia shughuli zao.

Kwa mipango hii miwili, nakwenda kuiona Bavicha inarudi na kuwa imara tena.

MTANZANIA Jumapili: Unaipimaje Bavicha unayoiongoza na ile ya watangulizi wako, yaani Katambi na John Heche?

Ole Sosopi: Bavicha yangu nategemea itakuwa imara zaidi tofauti na ile ya Katambi, kwa sababu ya uimara wangu.

Nasema uimara wangu katika misimamo, uimara katika kulipigania baraza, kuwa kisemeo kwa vijana wote, ninataka kuwa sauti ya wasiokuwa na sauti, kujenga taasisi na baraza langu linahitaji kuwa shirikishi.

Najenga baraza ambalo si la mtu mmoja, bali shirikishi kwa viongozi wote ngazi ya taifa hadi mkoa.

Kwa watangulizi wangu nitaanza kwa kumzungumzia Katambi, yeye alikuwa imara, lakini tuangalie kilichomsukuma kukimbia chama na kujiita karai inahakikisha pia hakuwa imara.

Nasema hivyo kwa sababu wapambanaji huwa hawakimbii mapambano, kwa maana hiyo nafasi aliyokuwa nayo hakustahili kuwa nayo. Bavicha ya kwangu itafuta Bavicha ya Katambi iliyodumu kwa miaka mitatu.

Bavicha ya Heche sitaki kuifanananisha sana na Bavicha ya kwetu. Bavicha yangu katika hali ya kisiasa tuliyonayo tegemea utendaji kazi wake utaendana na hali ya kisiasa ilivyo katika nchi.

Bavicha yangu ukitaka kuifananisha na ya Heche itazame katika mtazamo wa kisiasa,  kwa maana ya kwamba wakati Heche alikuwa na uwezo wa kufanya mikutano ya kisiasa mahali popote ilimradi atimize takwa la kisheria kwa kutoa taarifa polisi tu, hapakuwa na kizuizi chochote kile,  leo mimi nikitaka kukutana na vijana, hata kama nina ujumbe mkubwa wenye nia na uhitaji wa watu ninaminywa.

Natambua ni sheria inayotutaka tufanye shughuli za kisiasa kwa mikutano, maandamano pale yanapotakiwa, kwa sababu inatambuliwa kikatiba, leo hii hakutakiwi kufanya kitu kama hicho.

Kwa hiyo ninachokiona, utendaji kazi wetu ni bora kuliko utendaji kazi wa mabaraza yaliyopita, kwa sababu tunafanya kazi katika wakati mgumu sana wa kisiasa, mfano tu nilipokuwa makamu mwenyekiti nilikamatwa zaidi ya mara saba kwa tuhuma za uchochezi.

Kumbuka mimi ndiye nilikuwa mtu wa kwanza kukamatwa kwa tuhuma za uchochezi, baada ya hapo Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu) akafuata kwa tuhuma hizo hizo.

Kwa hiyo sisi tupo kwenye wakati mgumu sana, kwa wakati huu kama tukiamua kubeba wajibu wetu wa kuikosoa serikali ujue hatuko salama, lakini hii haina maana tutaacha, hatutaacha na sitapata kuacha hata siku moja.

Bavicha ya Heche ilifanya kazi iliyotukuka, lakini kwa ukweli halisia, Heche alifanya kazi kama Heche, yaani alifanya kazi kama mwenyekiti. Tofauti yangu ni kwamba mbali ya kufanya kazi uangu ya uenyekiti, lakini lazima makamu wenyeviti wote wafahamike na nitawapa msingi wa kufanya hivyo.

Tunataka kufanya kazi kama taasisi, si kwa  mtu mmoja mmoja kwa sababu nikikamatwa leo, makamu wenyeviti wanahitaji kuwa imara kwa kutoa tamko kueleza, ninapokuwa sipo nataka makamu wenyeviti wanasimama na kuzungumza, leo hii nimekuwa mwenyekiti kwa sababu wakati nilipokuwa makamu mwenyekiti nilifanya kazi kwa ufanisi mkubwa, pale mwenyekiti aliposhindwa  mimi niliziba pengo.

MTANZANIA Jumapili: Kwanini Katambi alikihama Chadema?

Ole Sosopi: Katambi alikwishaeleza sababu za kuhama kwake. Binafsi natoa masikitiko yangu makubwa sana kwa Katambi.

Nitaeleza kwa kifupi, Katambi aliondoka na kwa bahati mbaya siku anaondoka nilikuwa nimealikwa na Mstahiki Meya wa Ubungo, Boniface Jackob, kufanya mkutano katika Kata ya Saranga.

Nilitoka Iringa na kumfahamisha Katambi kuwa nakwenda Dar es Salaam kufanya mkutano, nikaahidi kuonana naye, kwa bahati mbaya akaniambia yuko Karatu anafanya shughuli ya chama ya kutoa mafunzo kwa madiwani.

Akaniambia atanitafuta kwa sababu kuna mambo ya kifamilia yanamsumbua, nikamwambia anishirikishe japo kwa ufupi ili sisi kama baraza tuangalie namna ya kusaidia, akaniambia hapana.

Nilipofika Dar es Salaam nikaenda hotelini, asubuhi niliwasha televisheni kwa sababu kulikuwa na mkutano mkubwa wa CCM, nikashangaa kumwona Katambi kwenye mkutano ule wa CCM wakati nilijua yupo Karatu.

Nilishtuka sana, sikuamini kama ndio yeye, lakini baada ya hapo nilimtumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu nikimwambia kila la heri bosi, naye akanijibu Mungu anibariki sana na huo ulikuwa mwisho wa mawasiliano kati yangu naye.

Niliamini tu kwamba kwenye siasa hakuna rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu na sikuwahi kuwa na ugomvi naye kabisa.

MTANZANIA Jumapili: Hukuona dalili yoyote ya yeye kutaka kukihama chama?

Ole Sosopi: Sikuwahi kuona dalili yoyote na sikuwahi kufikiri kwa sababu kuna vitu vingi tulikuwa tunapanga na nilimshauri vitu vingi sana kama mwenyekiti wangu.

MTANZANIA Jumapili: Kumekuwapo na tuhuma mbalimbali zikitolewa kuwa baadhi ya wanaohama Chadema wanashawishiwa na CCM, unadhani Katambi alishawishiwa na nani katika upande huo?

Ole Sosopi: Hilo ni suala binafsi mno kwa sababu kuwa Chadema haina maana ya kwamba huwezi kuwa na marafiki CCM au chama kingine chochote cha siasa.

Na kama niliwahi kumwona na watu wa CCM lakini sikuiruhusu akili yangu kufikiri kwamba walikuwa na mkakati wa kumnunua, kumshawishi au kutengeneza mazingira ya yeye kuondoka ndani ya chama.

Namsikitikia kweli, yaani ameondoka kama mwenyekiti wa vijana wa chama kikuu cha upinzani bila ya kuwa na ushawishi wa kuondoka hata na wenyeviti japo wawili au watatu wa mikoa, hata basi angeondoka na viongozi wa Bavicha ngazi ya wilaya, kata hata wa tawi?

Ninachokiona ni kwamba, Katambi katusaidia sana kama baraza au ninaweza kusema huo ni mpango wa Mungu, yaani kwa kiongozi mkubwa kama yeye kaondoka bila kulitikisa baraza.

Tangu ameondoka taasisi imeendelea kuwa imara vilevile, inamaana uwepo wake kwenye taasisi ulikuwa ni wa mashaka, kwa maana ya uwezo wake wa kutenda kazi na ushawishi aliokuwa nao.

Nimepata kuona taasisi nyingi ambazo kiongozi akiondoka unatokea mtikisiko mkubwa na Chadema kama chama kikuu cha upinzani kilipofikia hapa leo ambapo kina wabunge 72, madiwani zaidi ya 1,000 na kinaongoza majiji manne kati ya matano, halafu kijana mwenye sura ya upinzani unayeongoza taasisi kubwa kama hii unaondoka na watu wasitambue kwamba kuna mtu ameondoka ni sawa na kusema bora angeenda kufanya kazi nyingine, hata ya kuchunga mbuzi kuliko kuendelea kwenye siasa.

Huwezi kuwa mwanasiasa usiyekuwa na ushawishi, yaani unaondoka kama umesafiri. Tuliona Lowassa (Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa) alipoamua kutoka CCM na kujiunga na Chadema, CCM ilitikisika kwa kiasi chake.

Nachosema ni kuwa, tunamshukuru Katambi na bora alivyoondoka, nahisi alichelewa kuondoka, alipaswa kuondoka mapema kwa sababu ndani ya kipindi hiki cha mwaka mmoja tutafanya vitu vingi na mambo makubwa.

MTANZANIA Jumapili: Mkoa wa Iringa, ambao wewe unatoka huko, unaripotiwa kuwa madiwani wengi wa Chadema wanakihama chama hicho na kujiunga CCM, tatizo ni nini hasa?

Ole Sosop: Nikizungumza kama kiongozi wa chama, yako mambo mengi sana yameendelea kutokea katika nchi hii kwa sasa. Si kwa Iringa tu, wanaohama kutoka ndani ya chama si Iringa peke yake, tumeona Arumeru, Arusha, Tarime, Kinondoni na Siha.

Nachokisema kwa Iringa wameondoka kwa sura ile ile ambayo wengine pia wameweza kuionyesha walipoondoka. Sababu zote za wanaoondoka zinafanana, kwa kusema wanahama kwa kumuunga mkono Rais. Ni aibu sana, kwa sababu CCM inafanya vizuri basi mtu anaamua kuacha Chadema na kwenda CCM. Unakuta anayefanya hivyo ni mbunge kabisa ambaye wananchi wanamwamini.

Unajua katika mtazamo wa Kiafrika na desturi zetu tunaamini kuwa mtu anapokuwa kiongozi hupimwa kuwa na heshima na busara ya hali ya juu sana, kuna watu wanaweza kuwa na matatizo yao wakaja kuomba msaada wa kuwashauri kutokana na kukuamini wakapokea ushauri kwa kutambua una busara  na umepanuka kimawazo, inapotokea watu wana mawazo mfu ya kusema wanamuunga mkono Rais kwa kuhama chama na cha ajabu kuliko yote, chama kile kile walichohamia wanateuliwa tena kugombea nafasi ileile .

Hii inatupa kutuaminisha kuwa hawa watu wananunuliwa na moja ya makubaliano yao wanapewa fedha na wanapewa uhakika wa kuaminishwa kwamba lazima warudi kugombea katika nafasi ile ile halafu wao watahakikisha wanashinda kwa gharama yoyote.

Tumetoa ushahidi Arumeru, tumewapelekea ushahidi Takukuru na wanasema hawawezi kuendelea na uchunguzi kwa sababu jambo hilo limekuwa la kisiasa. Sasa jiulize unawezaje kupuuza jambo muhimu na linatokea kwa wanasiasa kwa kusema jambo hilo ni la kisiasa?

Ni jambo la aibu mtu kusema anaunga mkono juhudi za Rais. Tujiulize kama mtazamo ni huo nafikiri Marekani pasingekuwapo na vyama vya siasa.

Nasema hivyo kwa sababu Marekani kuna maendeleo, maendeleo ya Marekani tunayoyazungumzia ni huduma bora za afya, miundombinu, umeme, elimu na zile huduma za kawaida kama ulinzi sasa, kama ingekuwa ni msingi wa kusapoti maendeleo anayoyafanya Rais, Marekani kusingekuwa na vyama vya siasa kwa sababu watu wote wangeungana na Rais Donald Trump.

Sasa sisi ukimzungumzia mtu anayehama kwa kuunga mkono maendeleo yanayoletwa na Rais, hana maji, barabara, umeme na unakuta mwingine hana hata kituo cha afya kwenye kata yake.

Kwa hiyo kinachofanyika Iringa na mahali pengine hakiwezi kuiua Chadema, kumnunua diwani au mbunge wa Chadema haimaanishi umenunua upinzani, bali umenunua mtu. Watu wanatakiwa kufahamu upinzani ni fikra na imani na watu wanatambua hilo kwamba kununua diwani au mbunge hakuwezi kuua upinzani.

ITAENDELEA WIKI IJAYO

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles