23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MBINU ZA UPORAJI ARDHI, MAJINA YANAVYOBADILIKA


Na Marcelina Kibena, Morogoro 

TUNAPOZUNGUMZIA demokrasia mbadala kitu cha msingi ni kuzingatia ujenzi wa mfumo unaowapatia nguvu ya wazalishaji wadogo katika kumiliki na kudhibiti rasilimali za nchi yao. Rasilimali kuu ni ardhi, ambayo kimsingi ndiyo maisha na uhai wa wazalishaji wadogo.

Hii ni kwa sababu wazalishaji wadogo wanatumia ardhi kujipatia mahitaji yao ya kila siku. Pia, taratibu zao za maisha zinategemea ardhi na hizo ndizo zinawafanya waishi vizuri kwa kuzingatia mazingira yaliyopo.

Inapaswa kuangalia sera au sheria zilizopo kwa sasa, hasa sheria ya ardhi ya vijiji na. 5 ya 1999, ambayo inawapa mamlaka wazalishaji wa vijijini kutumia mkutano mkuu wa kijiji kusimamia ardhi yao, pamoja na kupanga jinsi ya kuitumia na kujiwekea uamuzi kwa kutumia sheria ndogo ndogo. Kwa hiyo mkutano mkuu wa kijiji ni chombo cha kidemokrasia ambacho wanakijiji wote walio watu wazima ni wajumbe.

Halmashauri ya kijiji ambayo huchaguliwa na mkutano mkuu ina jukumu tu la kusimamia ardhi lakini iko chini ya mkutano mkuu, na uamuzi wowote inaoutoa kuhusu ardhi lazima upitishwe na mkutano mkuu wa kijiji.

Kwa hiyo, sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999 pamoja na mapungufu yake mengi, imetoa nafasi kwa wazalishaji wadogo wenyewe kusimamia na kuidhibiti ardhi yao ya kijiji. Na hapa ndipo tunapotakiwa kupatazama kwa umakini kwa sababu viongozi wa vijiji wanaporubuniwa kutokana na nafasi waliyo nayo ili kutumia vibaya nafasi zao kuwezesha kuondoa udhibiti wa rasilimali ardhi kutoka kwenye mkutano mkuu wa kijiji.

Viongozi wasio waadilifu kutoka halmashauri za wilaya pamoja na wizara wamekuwa wakiwarubudi viongozi wa vijiji kwa vitu vidogo vidogo kama hongo ya fedha, vinywaji au hata kujengewa vibanda ambavyo havikidhi mahitaji ili kurahisisha uporaji wa ardhi ya kijiji.

Ardhi ya kijiji inagawiwa kwa mwekezaji, mkutano mkuu wa kijiji unaporwa nguvu ya kusimamia ardhi hiyo kwa sababu umiliki wake unahama toka kundi la ardhi ya kijiji chini ya Sheria na. 5 ya 1999 kwenda ardhi ya jumla chini ya sheria na 4 ya 1999. Ardhi ya vijiji husimamiwa na mkutano mkuu lakini ikishaingizwa katika ardhi ya jumla, usimamizi huo huhamia kwa kamishna wa ardhi.

Huo ni uporaji wa aina mbili: kwanza, wanakijiji wanaporwa ardhi yao wanayoitumia kwa uzalishaji. Ardhi hiyo inatoka katika umiliki wa wengi ambao ni wazalishaji wadogo wadogo kuwekwa katika umiliki wa wachache, ambao ni mabepari wakubwa. Pili, wanakijiji wanaporwa mamlaka yao ya kusimamia na kudhibiti rasilimali ardhi, ambayo yanatolewa kutoka kwenye chombo cha kidemokrasia na yanapelekwa kwenye ofisi ya mtawala (wa kirasimu).

Kwa kuwa hivi sasa tuko kwenye utandawazi na sera za uwekezaji, msukumo wa kupora ardhi ya kijiji umeongezeka zaidi, na hapa tunaona kwamba kuna mwanya mkubwa zaidi wa kuhamisha ardhi ya kijiji kwenda kwenye ardhi ya jumla kwa ajili ya uwekezaji. Ndio maana tunashuhudia mipango mbalimbali ya serikali ikiwekwa ili kurahisisha na kubadilisha matumizi ya ardhi.

Mfano wa mipango hiyo ni ule mkakati maarufu kwa Kilimo Kwanza. Mkakati huo una nguzo 10, lakini mimi nitajadili nguzo mbili. Nguzo namba 5 iko wazi kabisa; inazungumzia jinsi gani sera ya ardhi inapaswa kubadilishwa kwa ajili ya kurahisisha ardhi ya kijiji kuporwa na kuwekwa mikononi mwa wawekezaji wakubwa, na taasisi zilizopewa mamlaka ya kusimamia hilo ni Wizara ya Ardhi na TAMISEMI.

Hivi sasa utekelezaji wa nguzo hiyo umeanza na tayari kuna rasimu ya sera mpya ya ardhi ya mwaka 2016. Ukiisoma rasimu hiyo mabadiliko inayotaka kuyaleta:

(a) ardhi iwe bidhaa kama bidhaa nyingine zinazoweza kuuzwa kibiashara na kutumiwa kama dhamana katika mabenki. Kipengele hiki pia kinaonyesha kwamba karatasi zina uzito zaidi kuliko mtu ambaye amezaliwa na kuendeshea maisha yake katika ardhi hiyo. Kwa hiyo, mtu ambaye hana karatasi anaonekana kuwa hana ardhi. Kwa hiyo, tulitegemea kuwa serikali yetu, kama inataka kujenga sera nzuri, basi ingejaribu kufuta mifumo hiyo ya kikoloni badala ya kuiendeleza.

(b) Wawekezaji kutoka nje wanaweza wakapewa umiliki kamili kama wapewavyo Watanzania, tena milki ya miaka 99 kwa ajili ya kujenga nyumba za kuuza.

(c) Inazungumzia kuanzisha benki ya ardhi kwa ajili ya shughuli za uwekezaji na kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa wawekezaji wakubwa. Kwa hiyo, umiliki utakuwa wa wazi; na ardhi itahama kutoka kutoka mikononi mwa wazalishaji wadogo, na itahamia kwa mabepari wakubwa, na haitarudi kwa wazalishaji wadogo.

(d) Inampatia Kamishna wa ardhi mamlaka ya kusimamia ardhi ya kijiji. Kabla ya hapo, kamishna alikuwa ni mshauri tu kwa wanakijiji, lakini hivi sasa anapora mamlaka ya mkutano mkuu wa kijiji na kujipatia yeye mwenyewe.

(e) Inaendeleza mamlaka ya kikoloni aliyokuwa nayo malkia juu ya ardhi yetu. Japokuwa ardhi inasemekana kuwa ni ya umma, lakini ipo chini ya mikono ya rais. Na rais anaweza kuamua chochote, ikiwemo kufuta kijiji na kuhamisha ardhi ya kijiji kwenda ardhi ya jumla. Huyo mtu amepewa mamlaka makubwa sana, na sera hii imeyadumisha mamlaka hayo.

Sera hii mpya inakwenda kinyume kabisa na kauli ambayo Mwalimu Nyerere aliitoa mwaka 1958 akituonya juu ya kuuza ardhi ya wanyonge:

Nanukuu kauli ya Nyerere;“Katika nchi kama yetu, ambayo Waafrika ni masikini na wageni ni matajiri, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mwafrika akiruhusiwa kuiuza ardhi, katika miaka themanini au mia ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri wageni, na wenyeji watakuwa watwana. Lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la watanganyika matajiri wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache, kutakuwa na kundi dogo la waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana.”

Viongozi wetu wamepuuza onyo hilo la mwasisi wa taifa letu. Je, ni kwa sababu amefariki ndio maana viongozi wetu wanajidai kusahau nasaha zake, au ndio kusema kwamba zimepitwa na wakati?

Kutokana na kupuuza onyo la Mwalimu Nyerere, viongozi wanatekeleza sera za kiporaji za ardhi; ndio maana tunashuhudia kuongezeka kwa migogoro ya ardhi iliyopo kati ya wakulima na wafugaji au wawekezaji na wakulima wadogo inayotokana na suala zima la ardhi kubwa kuwa mikononi mwa waporaji wachache, ambao kwa jina zuri tunawaita wawekezaji. Lakini ni walewale mabepari, mabeberu, makabaila, ila tu tumewabadilishia majina ili kuficha uporaji wao.

Walio wengi wanabaki kugombania kipande kidogo cha ardhi, ambacho pia kipo hatarini kuporwa. Hii inatuonyesha wazi kwamba tuliowakabidhi mamlaka hawana uadilifu, uaminifu na ile imani ya ndani kwamba Tanzania ni ya watu wote, hasa wanyonge na wazalishaji wadogo, ambao nao wanahitaji kuishi kwa amani na utulivu.

Tumeshuhudia wazi panapotokea migogoro ya ardhi baadhi ya viongozi huigeuza kuwa miradi kwa sababu wafugaji wenye mifugo mingi hutumika kama chanzo cha fedha cha kuwashibisha viongozi. Kwa hiyo, viongozi hao huendelea kuchochea migogoro hiyo iendelee ili wao wafaidike lakini pia kusiwe na umoja miongoni mwa wazalishaji wa msingi.

Kwa hiyo kitu kinachoonekana ni kwamba mwisho wa siku hii migogoro ya wakulima na wafugaji ndio inayozungumziwa, wakati chanzo halisi, ambacho ni uwekezaji mkubwa wa kiporaji, hakionekani kama ni tatizo.

Huko Kilwa yupo mwekezaji aliyechukua hekta 34,000 kwa ajili ya kilimo cha mibono. Huyo ni mwekezaji mkubwa katika wilaya ya Kilwa lakini amewekeza nini? Amechukua ardhi, amefyeka miti akaiuza, ameharibu vyanzo vya maji. Shamba bado ni lake japo liko wazi, na labda ameshachukua mkopo kwa kutumia hati ya ardhi aliyopewa. Wengine hukodisha mashamba hayo kwa wanavijiji walioporwa ardhi.

Hapo mwanzo nimezungumzia nguzo namba 5 ya Kilimo Kwanza ambayo inachochea uporaji wa ardhi. Sasa naomba nizungumzie nguzo na 7 ya Kilimo Kwanza ambayo inahusu suala la pembejeo – mbegu, mbolea, madawa, nakadhalika.

Ili hayo makampuni makubwa ya nje yaweze kufanya biashara yameamua kuja kwenye soko la Afrika. Hivi sasa makampuni hayo yanasisitiza matumizi ya mbegu ya zilizobadilishwa vinasaba. Kwa kweli, si mbegu salama. Zina madhara ya kiafya na ndio maana hata haziruhusiwi katika nchi kadhaa za Ulaya, yanakotokea makampuni hayo. Mimi naamini zimeletwa Afrika ili kuua nguvu kazi, na waweze kutupora ardhi yetu.

Zaidi ya hapo, GMOs zinatugeza kuwa watumwa wa mbegu. Mbegu zenyewe za GMOs haziwezi kuhifadhiwa msimu hadi mwingine. Kama huna fedha maana yake huwezi kuendeleza kilimo. Afrika inazidi kutekwa na hizo fikra za kipuuzi, kwamba Waafrika hawawezi kutegemea chakula chao mpaka wategemee makampuni ya kibeberu.

Kwa hiyo kikubwa ni kwamba tunaendelea kufuata mifumo ya kikoloni inayowanyang’anya wanyonge wa vijijini rasilimali zao na mamlaka yao. Hatutaki kuivunja mifumo hii. Lakini wanyonge ni lazima waungane kuivunja mifumo hii na kujenga mifumo ya kijamaa, ili watu wagawane rasilimali kutokana na mahitaji ya msingi ya kila mtu na sio ulafi wa kujilimbikizia mali wa watu wachache.

Nguvu ya muungano tunaiona kwa mabepari ambao wameungana kwa ajili ya kututawala na kutunyonya. Lakini wazalishaji wadogo hawana sauti ya pamoja. Watu wa Kilosa mkoani Morogoro wanaporwa ardhi, sisi wengine hatusikii. Tunaona ni tatizo lao.

Watu wa shamba la Kidago katika kijiji cha Lukonde wananyanyaswa na kufungwa lakini sauti zao hatuzisikii. Tunaona ni tatizo lao wenyewe. Pia, tumegawanywa kwenye nchi. hatuzungumzi kama wanyonge wa Afrika.

Kumbuka wakoloni walitugawanya katika nchi ili watutawale na wapore rasilimali zetu kiurahisi. Lakini tukiunganisha nguvu na kupambana kama wavujajasho wa Afrika, hata mabepari wenyewe watatuogopa. Wakienda kupora ardhi Kilosa, wajue sisi wote tutaungana kupambana nao. Basi watatuogopa, wakijua kabisa kuwa wakimpora mmoja wetu ni sawa na kutupora sisi sote na Afrika nzima tutaungana kupambana nao. Hivyo ni lazima tuachane na haya masuala ya nchi, tupambane kama wanyonge wa Afrika nzima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles