Aveline Kitomary -Mwanza
MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kanda ya ziwa, imechunguza sampuli 210 katika kubaini uchafuzi wa mazingira kwenye migodi midogo na mikubwa.
Akizungumza wakati wa kampeni za Tumeboresha Sekta ya Afya inayoendeshwa na maofisa habari wa taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Afya, Meneja wa GCLA Kanda ya Ziwa, Boniventure Masambu, alisema matokeo ya sampuli hizo yatatumika na Serikali kuchukua hatua za kisheria.
“Kabla ya mwaka 2015 maabara hii ilikuwa inapeleka sampuli za mazingira maabara ya Dar es salaam kwa uchunguzi, baada ya kuimarisha vifaa uchunguzi wa sampuli zote unafanyikia hapa.
“Itakumbukwa kuwa kulikuwa na mgogoro mkubwa wa uchafuzi wa mazingira wa kampuni ya Acacia North Mara, maabara hii ilihusika katika hatua zote za uchunguzi,”alisema Masambu.
Alisema kutokana na mitambo walaiyo nayo, uchunguzi wa sampuli umeongezeka kutoka 1,085 mwaka 2015 hadi sampuli 7,193 mwaka 2019.
“Uchunguzi wa aina zote za dawa za kulevya unafanyika hapa, pia hii imesaidia kuharakisha kesi za aina hizo katika mahakama hivyo mashauri ya dawa za kulevya yanachukua muda mfupi kwa kuwa taarifa za uchunguzi hutolewa baada ya muda mfupi,”alibainisha.
Masambu alisema ukaguzi wa maeneo yenye kemikali umeongezeka kutoka 151 mwaka 2015 hadi 213 mwaka 2019.
“Kutokana na kuongezeka kwa rasilimali watu tunawakaguzi katika mipaka ya Sirari, Kabanga, Rusumo, Kigoma na Matukula bandari ya Mwanza inakaguliwa na Ofisi ya Mwanza na Makao Makuu ya kanda, Kiwanja cha ndege cha Mwanza na mpaka wa manyovu bado wakaguzi wake ni maafisa Afya wa Wizara,”alifafanua.
Mafanikio mengine yaliyopatikana ni ongezeko la vibali vya kuingiza na kutoa kemikali nchini kupitia mipaka ya kanda ya ziwa ambapo vimeongezeka kutoka 1350 mwaka 2015 hadi 2246 mwaka 2019.