25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Nyuma ya pazia JPM kumteua mwanajeshi kuongoza magereza

Grace Shitundu- Dar es Salaam

UTEUZI alioufanya Rais Dk. John Magufuli juzi usiku wa viongozi wa wizara, mahakama, mikoa na majeshi, umeonekana kugusa Jeshi la Magereza na Zimamoto kwa namna ya kipekee.

Katika uteuzi huo Rais Magufuli amemteua Brigedia Jenerali Suleiman Mungiya Mzee kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza.

Brigedia Jenerali Mzee anachukua nafasi ya Phaustine Kasike ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Dalili za Rais Magufuli kuwapelekea Magereza kiongozi kutoka Jeshi la Wananchi (JWTZ) zilianza kuonekana tangu Machi 16 mwaka jana alipofanya ziara ya kushtukiza na kukuta ujenzi wa nyumba za makazi ya askari wa Jeshi hilo Ukonga, uliokuwa ukifanywa na Wakala waMajengo (TBA)  ukisuasua.

Kutokana na hali hiyo  Rais Magufuli aliagiza mradi huo ukabidhiwe kwa JKT na kuwataka wataalamu wa TBA na askari Magereza kuondoka na kuwapisha JKT ambao walijenga Ukuta wa Mererani, nyumba 45 za serikali Dodoma.

Alipokuwa akikabidhi ujenzi huo kwa JKT Rais alinukuliwa akisema; “Siku tutawakabidhi Magereza nyumba zilizojengwa na jeshi, inawezekana siku moja wakaanza kujifunza kuona aibu, lakini siku moja wasije wakashangaa nikimteua mkuu wa magereza akawa mwanajeshi.

“Ni aibu kuleta jeshi jingine la wananchi kuja kuwajengea nyumba nyinyi, wakati nyumba mnaakaa nyinyi, mlitakiwa muwe mmeshapanga mkakati kwamba TBA wamesuasua, ngoja tufyatue matofali, tuanze kujenga”alinukuliwa Rais akisema katika ziara hiyo ya kushtukiza.

Januari 23 mwaka huu wakati akikabidhi nyumba hizo zilizokamilishwa baada ya miezi sita na JKT, Rais Magufuli aliwapongeza akirejea maneno yake yale yale.

“Mnafanya kazi nzuri mlijenga Mererani mkamaliza, ujenzi wa mji mpya wa Dodoma , ukuta wa Ikulu wamemaliza kila sehemu wanakopelekwa, kila mahali panaposhindikana wanapelekwa JKT.

“Najiuliza Magereza mmeshindwaje kujifunza huko, mkachukua hata maaskari magereza wakaenda kujifunza huko hata miezi sita, wakaujua uchawi wa JKT, mbona kozi ni zile zile, mbinu za medani ni zile zile” alinukuliwa Rais akisema.

Alisema alishawahi kuzungumza na Kamishna Jenerali wa magereza zaidi ya mara tatu lakini wanakwama katika miradi mbalimbali.

Kabla ya hapo Rais Magufuli aliwahi kushangazwa na hata kuhoji kitendo cha Magereza kukosa chakula ili hali wana wafungwa wengi wanaoweza kulima vizuri.

Kutokana na hayo na uteuzi huo mpya wa mwanajeshi ndani ya magereza, baadhi ya wachambuzi wanaona kuna kila dalili za mwenendo wa jeshi hilo kiutendaji kubadilika na kuanza kujitegemea.

Watu wanaomfahamu Brigedia Jenerali Mzee ambaye alikuwa akiongoza chuo cha ugavi Morogoro wanasema ni mtu ambaye amekuwa mfano kujitegemea hasa kwenye kilimo.

Wanasema anasifika kwa kufanya kilimo cha mfano na hata alipokabidhiwa chuo hicho baada ya muda mfupi kilianza kujitegemea hasa kwenye upande wa chakula.

MABADILIKO MAPYA

Katika mabadiliko hayo mapya mbali na kumteua mwanajeshi huyo Magereza, Rais alimteua Naibu Kamishna wa Magereza (DCP) John Masunga kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuchukua nafasi ya Thobias Andengenye ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Katika uteuzi huo ambao Rais Magufuli ameonekana kuwapandisha watumishi wa umma na si kuwachukua nje ya mfumo huo, pia amemteua Dk. Hassan Abbas aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo amepanda na kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Dk. Abbas ambaye alikuwa pia ni alikuwa ni Msemaji wa Serikali amechukua nafasi ya Suzan Mlawi ambaye amestaafu.

Wengine walioteuliwa na Rais ni pamoja na Mary Makondo ambaye amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akimrithi Doroth Mwanyika ambaye amestaafu.

Kabla ya uteuzi huo Makondo alikuwa ni Kamishna wa Ardhi katika wizara hiyo.

Pia amemteua Profesa Riziki Shemdoe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara akichukua nafasi ya  Profesa Joseph Buchweishaija ambaye amestaafu.

Awali Profesa Shemdoe alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma.

Wengine walioteuliwa ni Zena Said, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati akichukua nafasi ya Dk. Hamis Mwinyimvua ambaye amestaafu.

Kabla ya uteuzi huo Zena alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Tanga.

Amemteua Christopher Kadio  aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza kuwa  Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akichukua nafasi ya Meja Jenerali Jacob Kingu ambaye ameteuliwa kuwa Balozi baada ya kuomba kujiuzulu.

Rais Magufuli pia alifanya uteuzi wa Leonard Masanja kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ambaye awali alikuwa ni Kamishna wa Umeme na Nishati Mbadala.

Katika uteuzi huo pia Rais ameteua makatibu tawala wa mikoa mitatu ya Tanga, Mwanza na Ruvuma.

Walioteuliwa ni pamoja na Judica Haikase Omari (Tanga), Stephen Mashauri (Ruvuma) na Emmanuel (Mwanza).

Kwa upande wa Ardhi, Nathaniel Nhonge ambaye awali alikuwa Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya Dar es Salaam na Pwani ameteuliwa kuwa Kamishna wa Ardhi katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

MAHAKAMA

Aidha Rais Magufuli ameigusa mahakama kwa kumteua Wilbert Chuma kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama, Kelvin Mhina kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani na   Shamira Sarwat kuwa Msajili wa Mahakama Kuu.

Pia amewateua Jaji Dk. Gerald Ndika, Wakili Julius Bundala na Wakili Genoveva Kato kuwa Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles