Mnada wa nyumba za Lugumi umehamia katika nyumba ya Upanga baada ya mnada wa kwanza katika nyumba iliyopo Mbweni, kuahirishwa kutokana na kushindwa kununuliwa baada ya wateja waliojitokeza kushindwa kufika bei elekezi.
Wateja watatu waliojitokeza walitaka kununua nyumba hiyo kwa Sh milioni 510 lakini Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Yono, Scholastika Kevela  ambayo imepewa dhamana ya kusimamia uuzwaji wa nyumba hizo alikataa kwa madai kuwa hawajafikia bei elekezi iliyowekwa na serikali.
Katika mnada wa awali uliofanyika Oktoba, mnada huo uliharibiwa na Dk. Louis Shika aliyedai anataka kunua nyumba hiyo lakini alishindwa kutokana na kutotimiza masharti ya mnada yaliyomtaka kulipia asilimia 25 kama malipo ya awali. Dk. Shika alidai fedha zake ziko nchini Urusi.
Hata hivyo, safari hii Dk. Shika hakuwapo katika mnada huo ambapo jana Mkurugenzi wa Yono alimuonya kuvuruga mnada huo lakini alimruhusu kwenda endapo anaamini mabilioni yake kutoka Urusi yameingia.