24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

NYUMA YA PAZIA KOFFI OLOMIDE, URAIS AFRIKA


NA MARKUS MPANGALA

KOFFI Olomide raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ni miongoni mwa watu maarufu duniani kutokana na shughuli zake za muziki. Taswira ya mwanamuziki huyo imejengwa katika burudani, maisha ya kijamii pamoja na kujihusisha na masuala ya kisiasa.

Mara kadhaa, Koffi, amekuwa akionekana kama mwanamuziki mwenye taswira tata kutokana na kufukuzwa baadhi ya nchi ikiwemo Kenya. Mwanamuziki huyo ametajwa pia kwenye tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia.

Jambo jingine kubwa ni pale alipotajwa kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi na mke wa zamani wa Rais mpya wa Liberia, George Weah, ikidhaniwa kuwa ungezuka mgogoro baina ya magwiji hawa wawili katika michezo.

Hata hivyo, kuna taswira nyingine ambayo Koffi ameijenga katika anga za kisiasa barani Afrika. Sifa kubwa ya mwanamuziki huyo ni kuwa rafiki wa viongozi mbalimbali hususani wanasiasa katika nchi za Afrika akipewa heshima kutumbuiza na mengineyo.

Ukianzia ukanda wa nchi za Kusini mwa Afrika, ukigeukia Magharibi mwa Afrika, Mashariki mwa Afrika, kote huko utakutana na alama ya Koffi Olomide, kushiriki kampeni za urais.

Makala haya yanachambua maeneo yote ambayo Koffi Olomide, ameshiriki kufanya kampeni za wagombea urais na kuwapa ushindi wote alioshirikiana nao.

LIBERIA

Wananchi wa Liberia walipiga kura kwa mara ya kwanza Oktoba 10, mwaka jana kuchagua Rais wa nchi yao kati ya mgombea wa Muungano wa Upinzani, George Weah, dhidi ya makamu wa Rais, Joseph Boakai.

Weah, aliyewahi kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika kushinda tuzo ya mchezaji bora duniani, aliongoza katika duru la kwanza la uchaguzi huo kwa kupata asilimia 39 wakati mpinzani wake Boakai, akimfuata kwa asilimia 29.

Katiba ya Liberia inatamka kuwa mgombea lazima afikishe asilimia 51 ili kutangazwa mshindi, kutokana na Weah kushindwa kutimiza matakwa ya kikatiba ilibidi Tume ya Uchaguzi nchini humo itangaze Novemba 7, mwaka jana kama siku ya marudio ya uchaguzi.

Siku chache baadaye mahakama ilisimamisha uchaguzi huo hadi ilipotangazwa kufanyika tena Desemba 26, mwaka jana. Katika uchaguzi huo wa marudio, George Weah, alitangazwa kuwa Rais wa Liberia na Tume ya uchaguzi nchini humo.

Siri ya ushindi wa George Weah, haiwezi kumweka kando mwanamuziki Koffi Olomide ambaye aliwasili nchini Liberia zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Koffi Olomide aliungana na mwigizaji Van Vicker pamoja na maelfu ya wananchi waliokuwa wakimuunga mkono Weah. Katika kampeni za uchaguzi huo, Koffi Olomide, alizunguka mitaani huku na huko kumwombea kura Weah. Baadaye aliungana na wafuasi wa Weah takribani 150,000 kutoka chama cha CDC walizunguka mitaa mbalimbali na kulakiwa na maelfu ya watu.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa kimataifa wanakiri kuwa Weah alicheza vema karata zake kwani iliongeza hamasa kwa wananchi pamoja na kuwavutia baadhi ya watu waliokuwa hawajaamua kupiga kura.

Kama inavyofahamika kuwa wanamuziki wamekuwa kivutio na ushawishi mkubwa katika jamii hivyo kwenye medani ya kisiasa ilimpa ushindi Weah. Wanasema hata Hilary Clinton ambaye aliungwa mkono na magwiji wa muziki, Jay Z na mkewe Beyonce Knowles, walikuwa chachu ya kampeni za chama cha Democratic nchini Marekani.

CONGO-BRAZZAVILLE

Jina la Kofi Olomide liliibuka tena kwenye kampeni za urais nchi jirani na kwao yaani Congo-Brazzaville. Ni mwaka 2016 ambapo Olimide alishiriki kampeni za mgombea wa urais, Dennis Sassou Nguesso, ambaye alikuwa akiwania katika kipindi cha tatu. Nguesso alipata nafasi ya kuwania muhula wa tatu baada ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2015 yaliyoondoa ukomo wa urais kumpa nafasi ya kugombea tena. Uchaguzi wa Congo-Brazzaville ulifanyika Machi mwaka 2016. Licha ya kulaumiwa na wapinzani wa Rais Guesso kwa kumsapoti kiongozi huyo aliyeamua kubadili katiba ili kumwezesha kugombea tena, lakini ukaribu wao umedumu hadi sasa.

RWANDA

Mwaka 2017 Taifa la Rwanda lilifanya Uchaguzi Mkuu Agosti 4, Rais Paul Kagame, alikuwa akigombea muhula wa tatu. Marekebisho ya Katiba ya mwaka 2015 yalimwezesha Rais Kagame kugombea tena nafasi hiyo ambayo atadumu nayo hadi mwaka 2024.

Kama ilivyoada jina la Koffi Olomide, likajitokeza tena kwenye kampeni za urais wa Rwanda baada ya kushirikiana bega kwa bega na chama tawala cha Rwandese Patriotic Front (RPF).

Uzinduzi wa kampeni za chama cha RPF ulifanyika ndani ya Uwanja wa Amahoro jijini Kigali nchini Rwanda. Koffi Olomide, alikuwa miongoni mwa wanamuziki waliotumbuiza katika uzinduzi huo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Burudani ya RPF, Jean Pierre Karabaranga, aliviambia vyombo vya habari kuwa walimchukua Koffi Olomide, kutokana na umahiri wake pamoja na kushiriki kwake kwenye kampeni za wagombea urais katika nchi mbalimbali barani Afrika.

“Sijatunga wimbo maalumu wa kampeni lakini muziki wangu una ujumbe mzito. Namheshimu sana Paul Kagame. Ninamkubali pia,” alisema Olomide aliwapowasili uwanja wa ndege nchini Rwanda, mwaka jana kwenye uzinduzi huo.

Sifa nyingine iliyotajwa ni kuwa Olomide amekuwa akifanya kampeni kwa wagombea ambao hushinda uchaguzi hali ambayo inawapa hamasa wanasiasa wengine wakiwemo Kagame kumwalika mwanamuziki huyo.

JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO  

Mwaka 2012 nchini kwake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Koffi Olomide, aliungana na wanamuziki wengine maarufu kama Papa Wemba na Werasson kumpigia kampeni Rais Joseph Kabila.

Katika kampeni hizo, Joseph Kabila, alishinda kiti cha urais akiwa na alama za mwanamuziki Olomide ambaye hajawahi kuona wagombea anaowasapoti na kuwafanyia kampeni wakishindwa kinyang’anyiro.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles