24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

UHAMIAJI WAMUHOJI MDOGO WAKE ASKOFU NIWEMUGIZI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


SAKATA la uraia wa Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki la Rulenge Wilaya ya Ngara mkoani Kagera limechukua sura mpya baada ya Idara ya Uhamiaji kumuhoji mdogo wake.

Taarifa zinaeleza kuwa Lucius Zagaraza Mathayo (57), ambaye ni mdogo wa askofu huyo, alihojiwa wiki iliyopita.

Akizungumza na MTANZANIA mwishoni mwa wiki, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, hakukubali wala kukataa badala yake alitaka waachwe waendelee na uchunguzi.

“Jambo la uchunguzi halifai kuliongelea kabla halijafikia mwisho wa matokeo. Tunaomba mtupe nafasi watu wafanye kazi,” alisema Dk. Makakala.

Naye Askofu Niwemugizi alisema uchunguzi kuhusiana na uraia wake unaendelea lakini yeye alishatoa taarifa muhimu zilizohitajika.

“Mimi nilijaza taarifa zangu, za baba na za mama walizaliwa wapi, sasa ikabidi kujua babu na bibi walizaliwa wapi lakini nilitafuta na kukamilisha.

“Naona sasa wanatumia njia zao nyingine kuendelea na uchunguzi,” alisema Askofu Niwemugizi.

Kuhusu suala la mdogo wake kuhojiwa alisema; “Mdogo wangu alinipigia akasema na yeye ameitwa kuhojiwa lakini sikuwa ‘interested’ kujua walimuhoji uraia wake au wa kwangu.

“Tulizaliwa wanne kwa baba na mama, wawili waliaga dunia hivyo tumebaki wawili (akimaanisha yeye na mdogo wake Lucius),” alisema.

Suala la uraia wa Askofu Niwemugizi liliibuka mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuitwa na kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji Ngara.

Katika mahojiano maalumu na MTANZANIA yaliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana, Askofu Niwemugizi alisema alihojiwa Novemba 28 na Desemba 4 mwaka jana.

Alisema alitakiwa kupeleka nyaraka muhimu kama hati ya kusafiria, kitambulisho cha kupigia kura na cheti cha kuzaliwa na kutakiwa kujaza fomu maalumu.

Alisema alizaliwa Juni 3 mwaka 1956, katika Kitongoji cha Kayanza, Kijiji cha Kabukome, Kata ya Nyarubungo Wilaya ya Biharamulo.

Alisema pia alibatizwa katika Parokia ya Katoke, Biharamulo.

Kuhusu elimu alisema alisoma katika Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo na Shule ya Sekondari Nyakato Bukoba (O-level).

“Baada ya kumaliza ‘O-level’ niliingia Seminari Kuu ya Ntungamo Bukoba halafu nikatoka hapo nikaenda Kipalapala Tabora,” alisema.

 Askofu huyo alisema mama yake alizaliwa Lusahunga wakati baba yake alizaliwa katika Tarafa ya Nyarubungo, Kijiji cha Kabukome Kitongoji cha Kayanza.

“Wote wameaga dunia kwa nyakati mbalimbali, kaburi la baba lilishapotea kwa sababu alizikwa Nyamilembe kabla hapajawa na idadi kubwa ya watu karibu na ziwa.

“Baadaye watu wameongezeka pale na eneo alipozikwa pamejengwa nyumba,” alisema.

Alisema katika maisha yake yote hakuwahi kuhisiwa kuhusu uraia wake na mara zote amekuwa akitumia hati ya kusafiria na hakuna aliyemuuliza uraia wake.

“Baada ya kutoa ushauri kwamba ni vizuri mchakato wa katiba ukarejewa watu wali – react na naweza kupata picha sasa nini kimesababisha nianze kuhisiwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles