Na WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, anatarajia kutumia mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga , kufuatilia viwango vya wachezaji ambao amekuwa akiwajumuisha katika kikosi chake.
Ndayiragije atakiongoza kikosi cha Taifa Stars kitakachoshiriki fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan), ambazo zinatarajia kutimua vumbi kuanzia Aprili 4 hadi 25 nchini Cameroon.
Akizingumza na MTANZANIA, Ndayiragije, alisema atakuwepo kwenye dimba la Taifa, kufuatilia mchezo huo kama alivyofanya katika mechi nyingine.
Alisema anajua ana kazi ngumu ya kutengeneza kikosi imara, licha ya kwamba maandalizi yameanza muda mrefu baada ya kufuzu michuano hiyo.
“Hakuna mechi nakosa kuingalia kwa sababu ni jukumu langu kama kocha wa timu ya Taifa, wachezaji wangu wapo katika timu zote Tanzania, ni lazima nifuatilie maendeleo yao,” alisema Ndayiragije.
Stars imepandwa Kundi D katika michuano hiyo na itazindua kampeni zake Aprili 7 kwa kuumana na Zambia.
Nchi nyingine zinazounda kundi hilo ni Namibia na Guinea.