Na BENJAMIN MASESE -MWANZA
KITUO cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Wanyama Kanda ya Ziwa( ZVIC) kimewataka Watanzania kuondokana na tabia na mazoea ya kula nyama ambayo haijathibitishwa na daktari wa mifugo.
Kaimu Afisa Mfawidhi wa kituo hicho, Subira Samweli,alisema yamekuwapo mazoea ya watanzania ya kula nyama ambayo haijapitia katika machinjio yanayotambulika.
Alisema kitendo ambacho kinawafanya kula kitoweo ambacho hakijathibitishwa na daktari wa mifugo.
“Watu ambao wapo katika hatari ya kupata maradhi ni wale ambao mara nyingi wanapenda kula kwenye baa, migahawa, harusi, gengeni na sehemu nyingine ambazo mara nyingi hazizingatii usalama na afya kwa walaji.
“Tabia hii imejengeka kwa jamii yetu na wala hata hawahoji kama nyama wanayokula imekaguliwa.
“Leo hii baa nyingi zinajinchijia mbuzi katika maeneo yao, hivyo hivyo kwenye harusi, migahawa na magenge, wanyama hao wana magonjwa mbalimbali hivyo ni vema watu wakaepuka kula nyama ambayo hajapitia kwa mtalaamu,” alisema.
Aliwataka maofisa mifugo wa mikoa, wilaya, tarafa, kata , vijiji na mitaa kuwa na utaratibu wa kufanya operesheni katika maeneo yao kukomesha vitendo vya watu kuchinja ovyo katika maeneo ya biashara zao bila kuthibitishwa na mtaalamu wa mifugo.
Akizungumzia takwimu za ng’ombe waliofikishwa katika mnada wa Nyamatala na kuuzwa kwa ajili ya kitoweo kati ya Novemba 2016 hadi sasa ni Juni 2017, alisema mwitikio wa wafanyabiashara umepungua.
“Ukiangalia mnada ulipoanza Novemba 2016, ng’ombe waliofikishwa sokoni ni 6,556 na waliouzwa na kupata vibali kwenda kuchinjwa ni 4698, lakini kwa kipindi cha Juni mwaka huu ng’ombe waliofikishwa ni 11,139, cha kusikitishwa waliouzwa ni 3,716 pekee.
“Hapo utaona jinsi gani kuna idadi kubwa ya mifugo iliyopelekwa lakini iliyouzwa ni kidogo. Pale Nyamatala bado miundombinu ya mbuzi na kondoo inatenegenzwa ili nao wapelekwe na si kuuzwa tena Igoma,”alisema.
Samweli alishangazwa na kitendo cha halmashauri za mikoa hiyo kutokuwa na utaratibu wa kutuma takwimu za mifugo ikizingatiwa kwa kipindi cha Julai ni halmashauri 11 pekee zilizotuma ripoti zao.
Alizitaja halmashauri hizo kuwa ni Serengeti, Msalala, Bukoba, Ushetu, Musoma , Shinyanga mjini na Vijini, Misenyi, Rorya, Bunda Mjini na Vijiji.