27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WATOTO WALIOKUWA WAMETEKWA WASIMULIA

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

WATOTO wawili waliokuwa wametekwa na watu wasiojulikana mkoani Arusha, Ayub Fredy na Bakari Suleiman, wamewaeleza wazazi wao  kwamba walikuwa wakila wali na maji tangu Agosti 21 walipotekwa.

Hayo yalielezwa jana na wazazi wa watoto hao wenye umri wa miaka mitatu walipozungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti.

Mama mzazi wa Ayub aliyejitambulisha kwa jina la Agness

Hussein,  alisema pamoja na mtoto kupatikana  bado anaonekana kuwa na hofu kutokana na mazingira aliyokuwa akiishi tangu Agosti 21 mwaka huu.

“Sisi ambao watoto wetu walikuwa wametekwa ni majirani na siku ya tukio watoto wetu walikuwa wakicheza nje ya nyumba yetu ambako ndiko walikochukuliwa na mwendesha pikipiki mmoja.

“Wakati wanawachukua  waliacha ujumbe uliokuwa na namba za simu wakitutaka wazazi tuwasiliane nao bila kulijulisha Jeshi la Polisi.

“Lakini  kwa sasa tumshukuru Mungu, watoto wetu wamepatikana ila bado wana hofu na wanaogopa hata kutembea wenyewe,” alisema mzazi huyo.

Naye mama wa mtoto Bakari aitwaye Asha Shaban, alisema watekaji hao waliwataka watoe Sh milioni tano  ili wawarudishie  watoto wao.

“Walitaka tuwape Sh milioni tano ili watupatie watoto wetu. Wakati wa mawasiliano na hao watu, balozi wetu aitwaye Tarimo, ndiye aliyekuwa akiwasiliana nao na kuwaambia hatuna fedha hiyo.

“Kwa hiyo, walichokifanya waliendelea kushusha mpaka kufikia Sh milioni mbili kisha wakasema tuwatumie Sh 500,000 na baadaye

wakaomba tuwapatie Sh 100,000.

“Walipokuwa wakiwasiliana, Tarimo aliwaomba wawalete watoto hao kwanza au wamtume mtu atakayewaleta watoto hao kisha wapewe fedha hizo.

“Kwa hiyo, watekaji hao walimtuma dereva wa pikipiki aliyewapeleka watoto katika baa ya Balozi iliyopo Kwamorombo. Alipofika hapo, alianza kuulizia wazazi wa watoto hao ili wampe fedha hizo.

“Kwa vile polisi walikuwa eneo hilo, waliweza  kumkamata mwendesha pikipiki huyo ingawa alisema hajui chochote juu ya watoto hao,” alisema mzazi huyo.

Watoto hao wawili na wenzao wawili, walitekwa kwa nyakati tofauti hivi karibuni kabla ya watekaji kuanza kuwaomba wazazi fedha ili wawarudishie watoto hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles