25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Nyalandu asalimu amri kwa Msigwa

Lazaro Nyalandu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu

Na Grace Shitundu

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ameifutia vibali vya umiliki wa vitalu vya uwindaji Kampuni ya Green Miles Safaris (Ltd).

Kampuni hiyo inadaiwa kukiuka sheria namba 5 ya mwaka 2009 ya uhifadhi wanyamapori.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Nyalandu alisema hatua ya kufuta vibali kwa kampuni hiyo imetokana na uchunguzi uliofanywa na kubaini ukweli wa tuhuma zilizotolewa bungeni na Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa, wakati wa kujadili bajeti ya wizara hiyo Mei, 14 mwaka huu.

“Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa kampuni hii imevunja sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 sambamba na kanuni za uwindaji hivyo nimeifutia vibali na ni marufuku kwa mtu, kikundi cha watu, wenyeji au wageni kuhujumu uchumi wa nchi na kuharibu urithi wa rasilimali tulizonazo,” alisema Nyalandu.

Alisema timu ya wataalamu wa Idara ya Wanyamapori imepitia video iliyoonyesha vitendo vilivyofanywa na wageni wa kampuni hiyo iliyokuwa ikimiliki vitalu vya Lake Natron GC East, Gonabis/Kidunda-WMA na MKI- Selous.

Nyalandu aliyataja makosa waliyoyafanya wageni wa kampuni hiyo kuwa ni pamoja na kuwawinda wanyama ambao hawakuruhusiwa kwenye leseni ya uwindaji wakiwamo nyani na ndege na kwenda kinyume na kifungu cha 19(1)(2) cha sheria ya wanyamapori.

“Wageni hao pia walichezea watoto wa pundamilia na ngiri kinyume na kifungu 19(1), waliwafukuza wanyama kwa magari na kuwapiga risasi wakiwa ndani ya magari kinyume na kifungu 65(1)(a)1.

“Makosa mengine ni kuwinda wanyama walio chini ya umri, kinyume na kifungu cha 56(1), kuruhusu mtoto chini ya umri wa miaka 16 kuwinda kinyume na kifungu cha 43(2)(a) pamoja na kuwinda huku wakipiga kelele jambo ambalo ni kero kwa wanyama na kinyume na kifungu cha 19(1) na (2),” alisema Nyalandu.

Kwa mujibu wa Nyalandu pamoja na kuifutia kampuni hiyo vibali pia ameivunja Idara ya Wanyamapori na badala yake wataanzisha Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania.

“Hali iliyoonekana katika video hii imeonyesha kuna udhaifu katika Idara ya Wanyamapori, hivyo tumeamua kuivunja idara hiyo na tutaanzisha mamlaka itakayosimamia mambo yote ya utoaji wa vibali vya uwindaji.

“Na kuanzia sasa Idara ya wanyamapori haitahusika na utoaji wa vibali na kazi yao kubwa itakuwa ni kuangalia na kusimamia sera ya wanyamapori,” alisema.

Hatua ya Waziri Nyalandu kuifutia vibali Kampuni ya Green Miles Safaris (Ltd), inafuatia video iliyoonyeshwa na Mchungaji Msigwa kwa waandishi wa habari inayoonyesha jinsi wanyamapori walivyouawa kinyama.

Video hiyo ya zaidi ya dakika 30 iliyorekodiwa na Kampuni ya Green Mile Safaris (Ltd), inaonyesha wawindaji hao wanaodaiwa ni kutoka familia ya Mfalme wa Abudhabi wakiwaua wanyama kwa kuwapiga risasi baada ya kuwafukuza kwa kutumia magari huku wakishangilia pindi walipowaua na kupongezana kwa lugha ya Kiarabu.

Wanyama walioonekana wakiuawa ni pamoja na nyumbu, nyati, tandawala weupe na weusi, ndege mbalimbali wakiwamo kanga huku wakionekana kuwakamata wanyama wengine wadogo wadogo ambao haijulikana waliwapeleka wapi.

Miongoni mwa wanyama wadogo waliokamatwa ni pamoja na mtoto wa ngiri na pundamilia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles