25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Tiketi bandia zaitia hasara MSC

meli mwanza
meli mwanza

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

KAMPUNI ya Huduma za Meli (MSC) inapata hasara kutokana na kuwapo tiketi bandia zinazoingizwa kwenye mauzo na fedha hizo kuishia mifukoni mwa wajanja.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA Jumamosi umebaini kuwa katika safari moja ya MV. Victoria zinakuwapo tiketi bandia 100 na hivyo kusababisha kupotea zaidi ya Sh milioni 1.6 kila meli hiyo inapofanya safari.

Tayari watumishi watatu wa kampuni hiyo wamesimamishwa kazi akiwamo Karani Daraja la II (Traffic Clerk II), Fasso Obondi, wakituhumiwa kuhusika na usafirishaji watu bila ya tiketi pamoja na kuwapo tiketi feki.

Meneja Mkuu wa MSC, Pojest Kaija, alithibitisha kusimamishwa kazi baadhi ya watumishi hao, hata hivyo hakutaka kufafanua zaidi ya kusema masuala hayo ni ya nidhamu ya kawaida kwa watumishi.

“Hili ni suala ambalo tunalichunguza, linahitaji muda kuchunguzwa, hivyo nakuomba usitoe katika vyombo vya habari kwa vile linaweza kuharibu ufuatiliaji ninaoufanya, kuna watu nimewasimamisha juzi kwa kuhusika na makosa kama hayo,” alisema Kaija.

Uchunguzi wa MTANZANIA Jumamosi umebaini kuwa wizi unaofanyika katika tiketi hufanywa kwa ustadi mkubwa na kuhusisha makarani wa mauzo ya tiketi, wakaguzi ndani ya meli pamoja na ofisi ya Meneja Mkuu ambayo kazi ya kwanza ni kukusanya tiketi zilizotumika, kuziba matundu yanayotobolewa wakati wa ukaguzi na kuzirejesha kwa ajili ya kuuzwa upya.

Uchunguzi ulibaini kuwa tiketi zilizotumika zimepigwa muhuri wa tarehe mara mbili na namba zake za usajili zimekuwa za chini tofauti na namba za usajili za tiketi halali ambazo huingizwa katika hesabu ya kampuni.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi mmoja wa makarani wa MSC alisema: “Kwa kawaida tiketi hutolewa na kampuni na kuuzwa zikiwa na namba maalumu, kama ni A basi namba zake zinakuwa na digiti tano zikianzia na 0 hadi kufikia 10,000, hivyo hivyo na b, c, d, hivyo wakati wa kuanza kuuzwa zikifunguliwa tiketi za namba C basi hutolewa 10,000 na kuandikishwa namba ya kwanza na ile ya mwisho kuuzwa.”

Uchunguzi umebaini kuwa tiketi za Februari huuzwa Julai, ambapo katika kipindi cha Julai tiketi zilizotumika zilikuwa ni C 08000 hadi C 08300 ambazo ziliuzwa na kuingizwa katika hesabu ya kampuni.

Uchunguzi huo umebaini kuwa tiketi bandia zilizoingizwa sokoni zilikuwa ni C 04700 hadi C 07500.

Imebainika kuwa tiketi bandia nyingi zinazouzwa ni zile za daraja la tatu kwa Sh 16,000 na huingizwa katika daraja hilo tiketi 100 hadi 200 ikitegemea na wingi wa abiria wanaosafiri. Tiketi 100 ni sawa na Sh milioni 1.6.

“Utaratibu wa MSC ulivyo, anayekata tiketi dirishani haruhusiwi kusimamia ukaguzi wa tiketi wakati abiria wakiingia, lakini kutokana na kuwapo mpango maalumu karani wa ndani ya meli amekuwa akisimamia abiria kuingia kwa lengo la kupitisha tiketi zao na kisha kuhusika na ukaguzi wa ndani ya meli,” alisema mmoja wa makarani.

Taarifa za kuwapo kwa wizi huo zimekuja ikiwa ni siku chache baada ya gazeti hili kufichua ajira za wafanyakazi watatu walioajiriwa upya baada ya kufukuzwa kwa makosa ya wizi.

Wafanyakazi hao waliajiriwa upya kuanzia Julai 17, 2012 na Machi 7, 2013 kwa madai kuwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali licha ya kwamba walihusika na upotevu wa mamilioni ya fedha za kampuni hiyo ya meli.

Wafanyakazi hao ni Fasso Obondi, Karani Daraja la II (Traffic Clerk II), Magayane Walu akiwa ni Karani daraja la III na Jacob Kimwaga aliyekuwa Karani Utumishi (Personal Clerk).

Walitimuliwa kazi kwa vipindi tofauti kwa makosa ya wizi wa fedha za kampuni Tawi la Kigoma chini ya Meneja Biashara, Projest Kaija ambaye sasa ni Meneja Mkuu wa kampuni hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles