27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NMB yaongeza faraja kwa wajawazito Kishapu

Mwandishi Wetu, Kishapu

Benki ya NMB kupitia tawi lake la Kishapu imetoa msaada wa vitanda saba vikiwemo vitatu vya kujifungulia na mashuka 25 kwa hospitali ya Jakaya Kikwete ya halmashauri hiyo.

Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 5 unaotarajiwa kuoboresha huduma kwa wajawazito wilayani humo ulikabidhiwa na Meneja wa NMB Kanda ya Magharibi, Sospeter Magesse.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba(aliyevaa kitenge)akipokea moja ya vitanda kutoka kwa Meneja wa kanda ya Magharibi wa NMB, Sospeter Magesse, ambapo benki hiyo ilikabidhi pia mitanda vitatu vya kujifungulia na vinne vya kawaida na magodoro yake, pamoja na mashuka 25 kwa ajili ya hospitali ya Jakaya Kikwete.

Akikabidhi msaada huo ambao ni muendelezo wa misaada inayotolewa na benki hiyo kuboresha sekta ya afya na elimu sehemu mbalimbali nchini, Magesse alisema huo ni utekelezaji wa sera ya benki ya kurejesha sehemu ya faida kwa jamii.

Alisema benki hiyo imetenga bajeti ya Sh1 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na misaada wakati wa majanga ya asili.

“Pamoja na sekta ya elimu na afya, NMB pia hushirikiana na Serikali na wadau wengine kusaidia jamii wakati wa majanga ya asili. Haya ni maeneo matatu tunayoyapa kipaumbele katika miradi yetu ya kusaidia jamii,” alisema Magesse

Akifafanua kwanini NMB imejikita katika miradi ya afya na elimu, meneja huyo ni kwa sababu sekta hizo ni maeneo muhimu kwa maendeleo na ujenzi wa Taifa.

“Ili kuendelea na kufanikiwa kiuchumi, Taifa linahitaji watu wenye afya njema na elimu bora; hii ndiyo maana NMB inasaidia maendeleo katika sekta za elimu na afya,” alisema Magesse

Mganga mkuu wa Halmashauri ya Kishapu, Dk Shani Mudamu alisema kupatikana kwa vitanda vitatu vya kujifungulia kutaiwezesha hospitali hiyo kuwahudumia wajawazito sita kwa wakati mmoja.

“Awali tulikuwa na uwezo wa kuwahudumia wajawazito wanne pekee kwa wakati mmoja. Sasa tutaweza kuhudumia sita huku kitanda kimoja kikiwekwa akiba kwa ajili ya dharura,” alisema Dk Mudamu

Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba aliushurku uongozi wa NMB kwa kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo wilayani humo.

“Mwanzoni tulipokea Sh5 milioni kusaidia kupaua vyumba vya madarasa na majengo ya zahanati; tukapokea Sh5 milioni nyingine ilichochea wazo la ujenzi kujenga shule ya sekondari ya wasichana Kishapu; na leo tumepokea vitanda na mashuka vyenye thamani ya Sh5 milioni. Tunaomba ushirikiano huu uendelee,” alisema Taraba

Kuhusu huduma za kibenki, Taraba aliwataka wakazi wa wilaya ya Kishapu kuchangamkia mikopo ya kuendeleza sekta sekta ya kilimo inayotolewa na benki hiyo kuongeza tija katika shughuli zao.

“Wafugaji wakope kunenepesha yao. Wakulima wakope trekta; tutumie benki hii kuongeza tija katika sekta ya kilimo na mifugo ambayo ndiyo njia kuu ya kiuchumi kwa Kishapu,” alishauri mkuu huyo wa wilaya

Mmoja wa wajawazito waliokuwa wakisubiri huduma hospitalini hapo, Mariam Masanja aliishukuru Serikali na wadau wa maendeleo ikiwemo benki ya NMB kwa kuboresha huduma hospitalini hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles