Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Benki ya NMB imezindua kampeni inayojulikana kama ‘Bonge la Mpango’ ambayo itawawezesha wateja wake kushinda fedha taslimu, pikipiki ya miguu mitatu, gari aina ya Tata ‘Kilikuu’ pamoja na gari la kifahari aina ya Toyota Fortuner yenye thamani ya Sh milioni 169.
Akizungumza leo Februari 22, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, amesema kuwa hiyo ni moja ya njia ya kurudisha faida kwa wateja wao waaminifu wanaotunza fedha ndani ya benki hiyo huku ikikusudia kuhamasisha utamaduni wa kutunza fedha kwa matumizi ya baadaye.
“Katika kipindi chote cha kampeni wateja wetu wanaoweka akiba ya walau Sh 100,000 wataingia kwenye orodha ya wanaostahili zawadi zilizopo ambazo ni fedha taslimu Sh 500,000 kwa washindi 10 kikao wiki.
“…pikipiki ya kubebea mizigo aina ya Lifan, gari ya kubebea mizigo maarufu kama Kilikuu au Toyota Fortuner, kampeni hii itaendelea mpaka Mei mwaka huu.
“Tunatoa fursa kwa wateja wetu sambamba na kuwahamasisha kujenga utamaduni wabkujiwekea akiba hasa kipindi hiki ambacho kila mmoja anaugulia maumivu ya msimu wa Sikukuu za mwisho wa mwaka zinazomaliza Fedha,” amesema Mponzi.