Na Mwandishi Wetu
-Bujumbura
RAIS wa Burundi, Pierre Nkurunziza amesifu ubora wa bidhaa zinazotengenezwa nchini akisema kuwa sasa zitakuwa mkombozi kwa wananchi wa nchi hiyo.
Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki alipotembelea maonyesho ya kwanza ya biashara ya Tanzania yaliyofanyika nchini hapa.
Maonyesho hayo yanalenga kuangalia soko pana la bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali kutoka Tanzania.
Maonyesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Tempete vilivyopo jijini Bujumbura yalianza Septemba 28, na kuhitimishwa juzi.
Yaliandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa lengo la kuongeza fursa za biashara katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Hii ni ishara ya kukomaa kwa undugu kati ya Tanzania na Burundi, wananchi wa Burundi walikuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata bidhaa hadi Dar es Salaam, lakini sasa wameletewa mlangoni.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukifurahia bidhaa aina hii lakini bei zilikua kubwa kutokana na gharama za usafiri, kwa sasa mambo yamekua mazuri.
“Uhusiano wetu unazidi kuimarika, naamini ile dhana ya utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inatekelezwa kwa vitendo. Naahidi kuunga mkono juhudi zote za kuimarika katika uchumi kati ya nchi mbili hizi,” alisema Rais Nkurunziza
Katika maonyesho hayo, ubalozi wa Tanzania nchini Burundi, ukiongozwa na Balozi Rajabu Gamaha kwa kiasi kikubwa umeshiriki kufanikisha maonyesho hayo.
Gamaha ndiye aliwisihi maofisa wa TanTrade kuwa na maonyesho aina hiyo kutokana na maombi ya kupata bidhaa kutoka Tanzania kuwa mengi ofisini kwake.
Awali katika hotuba yake ya ufunguzi Septemba 27 mwaka huu, Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, Dk. Joseph Bitore alisema biashara ni kitu kinachounganisha mataifa mawili katika uchumi hivyo watatumia maonyesho hayo kujifunza lakini pia kutanua wigo wa uhusiano wa uchumi kati ya Tanzania na Burundi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TanTrade, Christopher Chiza alisema uamuzi wa kupeleka bidhaa Burundi ulipofika mezani kwake hakutaka kusita kwa sababu alijua hiyo ni njia pekee ya kufikisha mbali bidhaa za Tanzania.
“Tunapofanikiwa kufika Burundi maana yake tunalenga soko pana la ukanda huu, tunatarajia kufikia soko la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa sababu hata wao tumearifiwa kuwa wananunua bidhaa kutoka Burundi,” alisema.