24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Nkurunziza aahirisha uchaguzi wa wabunge

Rais PierreBujumbura, BURUNDI
RAIS wa Burundi, Pierre Nkurunziza ameahirisha uchaguzi wa wabunge uliokuwa ufanyike Jumanne wiki ijayo kwa siku 10, bila kugusia ule wa urais.
Amri hiyo imetolewa huku makabiliano kati ya polisi na waandamanaji yakiibuka na kutishia umwagikaji wa damu katika taifa hilo.
Msemaji wa Rais, Willy Nyamitwe aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kuwa kutokana na jaribio la mapinduzi la wiki iliyopita na vurugu zilizofuatia, ni vema kusogeza mbele kidogo uchaguzi huo.
”Uchaguzi wa ubunge ulikuwa umepangwa kufanyika Mei 26 mwaka huu lakini sasa inatubidi kuuahirisha ili kuwasikiliza washirika wetu wa kimataifa na Tume ya Uchaguzi ambayo pia inatumia muda huo kutatua maswali yaliyowasilishwa na vyama vya upinzani,” alisema Nyamitwe.
Hadi kufikia sasa tarehe rasmi ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanywa Juni 26 haijabadilika.
“Kuhusu uchaguzi wa urais hilo halijaamulia, bado. Wacha tuone,” Nyamitwe aliwaambia waandishi wa habari alipojibu swali kuhusu uchaguzi huo.
Kuchelewesha uchaguzi huo hakutarajii kuwatuliza waandamanaji ambao wanasema mpango wa Nkurunziza wa kugombea urais kwa muhula wa tatu unakiuka katiba na makubaliano ya amani yaliyomaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2005.
Katika kile kinachoonekana kama sehemu ya maisha ya kila siku, umati ulikusanyika muda mfupi baada ya mapambazuko ukiimba nyimbo na kukabiliana na polisi na wanajeshi wakitaka mhadhiri huyo wa zamani wa michezo mwenye umri wa miaka 51 asigombee tena urais.
Mabomu ya machozi na risasi zilisikika katika kitongoji cha Musaga. Muda mfupi baadaye waandamanaji walionekana wakimbeba mtu aliyekuwa akivuja damu kwa wingi mguuni, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (Reuters).
Inasemekana mtu huyo alipigwa risasi na polisi.
Wanajeshi waaminifu kwa Nkurunziza walizima jaribio la mapinduzi Jumatano iliyopita.
Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) aliyeko hapa, Ruth Nesoba, amesema tayari Rais Nkurunziza ametia saini amri hiyo ya kuahirishwa uchaguzi wa wabunge.
Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU), wametoa wito kwa uchaguzi huo uliokumbwa na utata mkubwa uahirishwe kutoa fursa kwa mazungumzo ya upatanishi kuendelea.
Juzi, Rais wa Afrika Kusini naye alijitokeza kutaka kuahirishwa kwa uchaguzi huo kwa vile mazingira ya sasa hayaruhusu uchaguzi kufanyika kwa ufanisi.
Takriban watu 20 wameuawa kufuatia makabiliano baina ya polisi na waandamanaji mjini Bujumbura.
Maandamano hayo yalifikia kilele chake wakati makamanda waasi walipoendesha jaribio lililoshindwa.
Nkurunziza alikuwa Dar es Salaam kuhudhuria mkutano wa viongozi wa kanda uliolenga kutatua mzozo wa siasa nchini mwake.
Baada ya Nkurunzinza kufanikiwa kurudi nyumbani, maandamano yameibuka upya yakiendelea na msimamo ule ule kupinga Nkurunziza kuwania muhula wa tatu
Nkurunziza amekuwa akisisitiza haki ya kuwania muhula mwingine kwa madai kwamba ule wa kwanza hakuchaguliwa na wananchi bali wabunge.
Takriban watu 300,000 wamekimbilia mataifa jirani wakihofia kuibuka upya kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles