Na MWANDISHI WETU,
MATUMIZI ya tumbaku yamethibitika kisayansi kudhuru karibu viungo vyote vya mwili na kusababisha magonjwa kama vile saratani na kifo. Mbali ya kuwa ina madhara kiafya, tumbaku inasababisha uharibifu wa mazingira, hekta takribani 1200 za misitu zinamalizwa kila mwaka kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni za kukaushia tumbaku.
Mataifa mengi yamefanya jitihada nyingi ili kupambana na janga hili la kiafya, mazingira na uchumi. Kufikia Agosti, 2012 nchi 175 zilikubaliana kuchukua hatua kukomesha matumizi ya tumbaku. Hata hivyo, kuna mambo yanayoendeleza mazoea hayo. Kila mwaka, kampuni za kutengeneza tumbaku hutumia fedha nyingi katika matangazo ya kibiashara ili kuvutia wateja wapya, hasa wanawake na vijana katika nchi zinazoendelea.
KWANINI NI VIGUMU KUACHA KUVUTA TUMBAKU?
Vitu vinavyotengenezwa kutokana na tumbaku vinaweza kumfanya mtu awe mraibu (Addicted) kama ilivyo katika kutumia dawa za kulevya.
Pia mtu anapovuta nikotini, inaingia ndani ya ubongo baada ya sekunde saba tu. Nikotini ina asili ya sumu isiyoachika ndani yake.
Mara nyingi kuvuta tumbaku huwa ni sehemu muhimu ya maisha ya mtu kwa kuwa anaivuta anapokula, anapokunywa, anapozungumza, anapotaka kuondoa mfadhaiko na kadhalika.
Vile vile wavutaji hawajajikubali kwamba sigara ni haramu na si nzuri kiujumla.
Ili uweze kuacha kuvuta sigara kwa urahisi zaidi kuna mambo kadhaa ambayo unapaswa kuyafuata.
Andika sababu zinazokufanya uache
Maandishi hayo unapaswa kuwa nayo karibu ili iwe rahisi kwako kuangalia pale unaposhawishika kuvuta.
 Panga tarehe mahususi ya kuacha kuvuta
Baadhi ya wataalamu hushauri kuacha taratibu ingawa utafiti unaonyesha kwamba endapo mvutaji atavuta sigara chache tofauti na mwanzo basi kuna uwezekano wa kuvuta mpaka mwisho kila moja ya sigara hizo, hali hii huchangia kiwango cha nikotini kuwa juu karibu na ilivyokuwa mwanzo. Hivyo, ni bora zaidi kuacha mara moja ikifika tarehe iliyopangwa.
 Imarisha azimio lako
Ukitaka kuacha kuvuta sigara unapaswa kuazimia kabisa kuacha. Fikiria jinsi utakavyo faidika pindi utakapoacha kuvuta sigara ikiwa ni pamoja na kuokoa fedha, afya yako inaweza kuwa nzuri zaidi, pia utampendeza Muumba wako
Tafuta msaada
Watafute wale ambao wamefaulu kuacha mazoea hayo kwa kuwa huenda zaidi ya kuelewa hisia zako, wanaweza kukusaidia. Marafiki na washiriki wa familia mara nyingi hutoa ushirikiano kwako ili uweze kutimiza azma yako.
Kama kuna wenzako unaoishi nao wanavuta tumbaku washawishi waache pamoja nawe kwa kuwa nguvu za pamoja ni tofauti na nguvu ya mmoja kupambana na tatizo hili. Usipowashawishi kuacha wanaweza kukushawishi kurudia tabia yako ya uvutaji tumbaku hata kama uliazimia kuacha.
 Teketeza vitu vyote vinavyokufanya uvute
Ni muhimu kutekeza vitu ambavyo vinakushawishi kuvuta sigara kama vile kiberiti cha kuwashia tumbaku na vinginevyo.
Jiandae kukabiliana na madhara
Uchunguzi unaonyesha kwamba karibu asilimia 90 ya wale wanaojikwaa hurudia kuvuta. Unapoacha kuvuta unaweza kupatwa na dalili za ajabu mfano hamu ya kutumia nikotini, kichefuchefu, kujisikia mgonjwa, kichwa kuuma, kushuka moyo, kutokuwa na subra na kujisikia vibaya tu.
Dalili hizi hutokea kutokana na mwili kukosa nikotini iliyokuwa ya kawaida mwilini. Dalili hizi hupamba moto saa 12 hadi 24 baada ya kuacha kuvuta tumbaku na taratibu huacha kati ya wiki ya mbili hadi sita.
Mambo yanayoweza kukusaidia ni pamoja na kulala kwa muda mrefu zaidi, kunywa maji mengi au maji ya matunda, kula chakula chenye lishe, kufanya mazoezi ya kadiri na kuvuta pumzi kabisa na uwazie hewa safi ikijaa ndani ya mapafu yako.
Tegemea kupata kikohozi
Ni kawaida kupatwa na kikohozi pale unapoacha kuvuta tumbaku kwa sababu njia za hewa zinaanza kurudi katika uhai wake. Watu wengi hudai kikohozi hufanya hali kuwa mbaya na kuwashawishi kurudia kuvuta tumbaku. Jitahidi kujizuia kwa kuwa kikohozi hiki hupotea chenyewe kadri muda unavyopita.
Zitambue hali zote zinazokufanya uvute
Mara nyingi unywaji wa pombe huzuia jitihada za kuacha kuvuta tumbaku. Unapaswa kupunguza kiwango cha pombe utakachokunywa pale utakapoacha kuvuta sigara endapo utashindwa kuacha kabisa. Pia unashauriwa kunywa maji mengi na maji ya matunda.
 Zikumbuke siku zote unazofanikiwa kutovuta
Weka alama kwenye kalenda kwa siku zote unazofanikiwa kuacha kuvuta na ziangalie pale unaposhawishika kuvuta, huku ukijiambia sipaswi kuanza tena upya.
Kuwa mwenye mawazo chanya
Unaweza kuwaambia wengine huvuti, utakuwa na harufu nzuri. Baada ya wiki chache utajisikia vizuri zaidi, utapata ladha nzuri ya vyakula na hutokohoa. Pia utakuwa na fedha zaidi kwa kuwa hukutumia kununua tumbaku.
Vyakula vinavyotakiwa kwa wanaojaribu kuacha
Watu wengine huwa na hofu ya kunenepa wakiacha kuvuta sigara kwa kuwa hamu na ladha ya vyakula huwa bora zaidi pindi wanapoacha kuvuta tumbaku. Yapaswa utegemee kuongezeka kwa ladha na hamu ya vyakula ila jitahidi kutokula vyakula vya wanga na mafuta kwa wingi badala yake ule vyakula vingine na matunda.
 Usikate tama pale unaposhindwa
Chunguza ni kwanini ulishindwa wakati uliopita na jirekebishe. Kwa wastani watu waliofanikiwa kuacha kuvuta wamewahi kujaribu kuacha mara tatu hadi nne wakati uliopita.
Tembelea kliniki za kuzuia uvutaji
Madaktari wanaweza kukupa msaada unaouhitaji endapo unafikiri ni vigumu kuacha kuvuta tumbaku.
 Dawa mbalimbali zinaweza kukusaidia
Utafiti mmoja ulibaini kuwa asilimia 88 ya watu waliofaulu kuacha kuvuta sigara wanasema walifanya hivyo bila kutumia dawa zozote. Dawa hizo huhusisha dawa mbadala ya nikotini na huwa katika mifumo tofauti kama vidonge au bazoka. Pia kuna sigara za kieletroniki (e-cigarette) ambazo zimetengenezwa na hukufanya ujisikie kama unavuta sigara ya kawaida.
 Chagua marafiki
Epuka kuwa na watu wanaovuta tumbaku wanaoweza kukupa sigara. Pia waepuke watu wanaojaribu kuvuruga jitihada zako za kuacha kuvuta tumbaku, labda kwa kukudhihaki.
Dhibiti hisia zako
Katika uchunguzi mmoja karibu asilimia 66 ya wale walio anza tena kuvuta sigara walifanya hivyo baada tu ya kufadhaika au kupandwa na hasira. Ukipatwa na hisia fulani inayokuchochea kuvuta sigara, jikengeushe fikra labda kwa kunywa maji, kutafuna bazoka au kutembea. Jaribu kufikiria mambo yanayofaa.
 Epuka kusema ninavuta mara moja tu
Ukweli ni kwamba kuvuta mara moja tu kunaweza kutosheleza takribani asilimia 50 ya vipokezi vya nikotini kwenye ubongo kwa saa tatu. Matokeo yatakuwa kwamba utaanza tena kuvuta sigara.
Ukweli kuhusu kuvuta sigara husaidia kutuliza mfadhaiko
Uchunguzi unaonyesha kwamba nikotini huongeza kiwango cha homoni zinazomfanya mtu afadhaike. Hisia zozote zinazokudanganya kuwa mfadhaiko wako hupungua unapovuta sigara zinaweza kuwa zinasababishwa tu na athari za kuacha kuvuta sigara.
Ni kweli kwamba athari za kuacha kuvuta sigara zina nguvu, lakini zitapungua baada ya majuma machache tu.
Ikiwa unatibiwa tatizo lako la akili, kama vile mshuko wa moyo au schizophrenia, mwombe daktari akusaidie uache kuvuta sigara. Bila shaka atajitahidi kukusaidia labda hata atabadili matibabu yako ili yasiongeze ugonjwa wako au kuathiri dawa unazotumia.
FAIDA
Utafurahia maisha zaidi.
Watu wanapoacha kuvuta tumbaku, uwezo wao wa kunusa na kuonja unaboreka na kwa kawaida wana kuwa na nguvu zaidi na sura yao inapendeza zaidi.
Utaokoa fedha, afya yako inaweza kuwa nzuri zaidi, utajiamini zaidi.
Familia yako na marafiki watafaidika. Utampendeza muumba wako.