25.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

TETEKUWANGA: UGONJWA UNAOWATESA ZAIDI WATOTO

tete

Na HERIETH  FAUSTINE,

TETEKUWANGA ni ugonjwa wa kuambukiza ambao husababishwa na virusi vinavyojulikana kwa jina la kitaalamu Varicella Zoster Virus.

Maambukizi ya tetekuwanga huonekana zaidi kwa watoto wadogo ingawa hata watu wazima pia hupata ugonjwa huu.

Tetekuwanga hupatikana duniani kote, hasa katika nchi zenye majira ya baridi. Utafiti umebaini kuwa maambukizi ya ugonjwa huu hupatikana zaidi kipindi cha majira ya baridi na masika.
Kirusi kinachosababisha ugonjwa huu husababisha uvimbe ulio sawa na vipele, mwasho, uchovu na joto katika mwili wa mwanadamu.

Pindi mtu anapoambukizwa ugonjwa huu, huanza kutokwa vipele vilivyoambatana na mwasho sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo usoni.

Ugonjwa huu huwakumba zaidi watu walio na umri chini ya miaka 15 pamoja na watoto walio na umri wa miaka minne hadi sita.

Watoto wengi hupata maambukizi ya tete kuwanga kabla ya kufikia umri wa kubalehe, ingawa asilimia 10 ya vijana nao wanakuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi hayo.
Katika nchi za kitropiki, maambukizi ya tete kuwanga huonekana kwa watu wakubwa na huwa ni hatari mno.
Inakadiriwa kuwa tete kuwanga huambukiza kwa kiwango cha asilimia 90.

 Maambukizi ya tetekuwanga

Tetekuwanga huambukizwa kupitia njia ya hewa au endapo mtu atagusana mwili na mgonjwa na kupata majimaji yanayotoka kwenye vipele vya mgonjwa basi ni lazima ataugua.

Mtu yeyote yule anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kutoka kwa mgonjwa wa tetekuwanga kwa njia ya kushikana, kucheka, kupiga chafya na kukohoa.
Hii inatokana na kusambazwa kwa virusi ya Varicella zoster kwa njia ya hewa pindi mgonjwa anapocheka, kupiga chafya au anapokohoa.

Dalili

Viashiria vya awali vya tetekuwanga ni pamoja na kichefuchefu, kukosa hamu ya kula, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli na kuumwa tumbo.

Viashiria hivi baadae hufuatiwa na hatua ya mgonjwa kutoka vipele, uchovu na homa ambayo si kali, hatua hii ndio huonyesha kuwapo kwa ugonjwa wa tetekuwanga.
Vipele hivi mwanzo huonekana kama alama nyekundu ndogo kwenye uso, kichwa, tumbo, kifua, sehemu za juu za kwenye mikono na miguu ambapo baada ya saa 10-12 alama zile nyekundu hugeuka kuwa uvimbe ambao baadaye hujaa maji na kupasuka.
Baadae vipele vipya huanza kuchipuka kwa makundi, kwenye sehemu za siri za mwanamke, kope na mdomoni, kisha hupasuka na kuwa vidonda vidogo vidogo.
Vipele hivyo pia vinaweza kutokea kwenye viganja vya mkono, nyayo na hata kwenye pua, midomo, masikio pamoja na njia ya haja kubwa.

Hatua hii ya kutokea vipele huanza kuonekana kuanzia siku ya 10-21 baada ya mtu kupata maambukizi ya tete kuwanga na huambatana na kuwashwa mwili.

Vipele venye majimaji (blisters) hutokea siku ya 4-7 baada ya kutoka vipele kuanza na hupotea kuanzia siku ya tano na kuendelea.

Mtu ambaye ana maambukizi ya tete kuwanga huweza kuambukiza watu wengine siku moja au mbili kabla ya kuanza kutoka vipele na kuendelea kuwa na uwezo wa kuambukiza wengine kwa siku nne – tano baada ya vipele kutokea.

Ugonjwa huu ni nadra kuwa na madhara makubwa ingawa madhara huweza kuonekana kwa wagonjwa walio na upungufu wa kinga mwilini, wenye kuugua magonjwa sugu au wajawazito ambao hawakupata chanjo ya ugonjwa huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles