22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

NIYONZIMA,TSHISHIMBI WALIVYOTEKA NGAO YA JAMII

BADI MCHOMOLO, DAR ES SALAAM

LICHA ya mashabiki wa klabu ya Simba kuibuka na furaha baada ya timu yao kuanza vizuri msimu huu kwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, dhidi ya Yanga SC, lakini kwa upande wa Yanga walikuwa wenye amani kutokana na kiwango cha maana kilichoonyeshwa na  kiungo wao mpya, Papy Tshishimbi.

Ilikuwa furaha kubwa kuanzia kwenye Uwanja wa Taifa hadi maeneo ya Msimbazi, Kariakoo yaliko makao makuu ya klabu hiyo, mashabiki wa Simba walikuwa na kiu ya taji kwa  miaka minne kutokana na klabu yao kushindwa kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Usajili walioufanya Simba msimu huu uliwashawishi mashabiki wengi kujitokeza kwa wingi  kwenye uwanja huo, huku wakiamini wana kila sababu ya kutwaa taji hilo dhidi ya watani wao wa jadi Yanga.

Dalili za Simba kujaza uwanja zilianza kuonekana Agosti 8, katika mchezo wao wa kutambulisha wachezaji (Simba Day), huku klabu hiyo ikifanikiwa kushinda bao 1-0 dhidi ya Rayon Sports FC ya Rwanda.

Hapo Simba walianza kuamini kuwa wana kikosi ambacho kina uwezo wa kufanya makubwa msimu huu, hasa kutokana na ujio wa mchezaji wao wa zamani, Emmanuel Okwi na usajili wa  Haruna Niyonzima, Aishi Manula, John Bocco na wakali wengine kadhaa.

Katika mchezo wa juzi, pia mashabiki wa Simba walijitokeza kwa wingi uwanjani hapo kuishuhudia timu yao ikicheza na Yanga.

Kwa upande wa Yanga, waliojitokeza ni wale wenye roho ngumu na wapenda soka, lakini walijikuta na furaha licha ya timu yao kupoteza mchezo huo kwa kuchapwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika bila ya kufungana.

Tangu kufanyika kwa mchezo huo hadi leo, mashabiki wa Yanga wanalizungumzia jina la Tshishimbi, huyu ni kiungo mpya aliyesajiliwa kipindi hiki cha usajili wa msimu ujao, ni kweli Yanga wana haki ya kumfurahia mchezaji huyo.

Kwa kipindi kirefu Yanga walikuwa wanakosa huduma ya kiungo mkabaji tangu kuondoka kwa Athumani Chuji, lakini sasa wanaamini mbadala wa Chuji ni Tshishimbi.

Hakuna ambaye alidhani kama jina la Tshishimbi lingeweza kutawala kwenye uwanja huo siku hiyo, lakini aliweza kuwashawishi mashabiki wa timu hiyo kusimama kwenye majukwaa yao na kuanza kuimba Tshishimbi, Tshishimbi, Tshishimbi.

Mchezaji huyo aliweza kuleta mawasiliano mazuri kati ya safu ya Ulinzi ya Yanga na sehemu yao ya ushambuliaji, alimfanya Kelvin Yondani na Andrew Vicent (Dante) wapate muda wa kupumzika.

Mipira mingi ya washambuliaji wa Simba ilikuwa inaishia kwa Tshishimbi, kwa kuwa viungo wa Wekundu hao walikuwa wanatumia muda mwingi kujaribu kupita katikati badala ya kuwatumia viungo wa pembeni.

Tshishimbi aliifanya safu ya ulinzi ya Yanga kuonekana kuwa bora, lakini washambuliaji wao walishindwa kupita kwenye ukuta wa Simba.

Mchezaji huyo ambaye alijiunga na Yanga wiki iliyopita, alicheza vizuri dakika zote 90, huku akifanikiwa kupiga jumla ya pasi 63, kati ya hizo 51 zikifika sehemu sahihi na 12 zilipotea.

Katika mchezo huo, pia mashabiki wengi wa Yanga waliingia uwanjani wakiwa na lengo la kumtazama mshambuliaji wao mpya, Ibrahim Ajib aliyejiunga nao akitokea Simba, lakini hakuweza kuwakosha vilivyo kama ilivyokuwa kwa  Tshishimbi.

Ajib katika mchezo huo aliweza kupiga jumla ya pasi zilizokamilika 10 katika dakika 45 za kipindi cha kwanza, huku akipoteza pasi nne, wakati  kipindi cha pili akipiga pasi saba zilizokamilika na akipoteza pasi nne, hivyo kufanya  dakika zote  90 kupiga  jumla ya pasi 25, nane kati ya hizo zikiharibika.

Kwa upande wa Simba, mbali ya ujio wa Okwi, lakini idadi kubwa ya mashabiki wa timu hiyo walikuwa wanataka kumuona Niyonzima aking’ara katika mchezo huo.

 

Kiungo huyo aliwapa furaha  mashabiki wa Simba kutokana na kile alichokifanya, aliweza kuufanya mpira vile anavyotaka na kufanya apigiwe  makofi ya pongezi.

Niyonzima alipiga pasi 34 zilizokamilika dakika 45 za kipindi cha kwanza, huku akipoteza pasi 2, hivyo aliweza kuzunguka sehemu kubwa ya uwanja kujaribu kuiunganisha timu sehemu ya mabeki na washambuliaji.

Katika dakika 45 za kipindi cha pili, Yanga walianza kwa kuutawala mchezo  kabla ya Simba kukaa sawa na kumfanya Niyonzima aendelee kupiga pasi za maana.

Niyonzima katika dakika 45 za kipindi cha pili alipiga jumla ya pasi 23 zilizokamilika na kupoteza pasi moja, hivyo kumfanya katika dakika zote 90 apige jumla ya pasi 57, huku pasi 54 zikifika sehemu sahihi.

Ni wazi kwamba mchezo huo ulikuwa wa Niyonzima na Tshishimbi, lakini Niyonzima alionesha kuwa ana uzoefu na soka la Tanzania na ndio maana aliweza kuzunguka sehemu kubwa ya uwanja na kukamilisha majukumu yake.

Kutokana na hali hiyo, Niyonzima aliweza kuisaidia timu yake kuongoza kwa idadi kubwa ya pasi, Simba ilipiga  jumla ya pasi 546, kati ya hizo 359 zilifika sehemu sahihi huku 187 zikipotea.

Yanga ilipiga jumla ya pasi 510, kati ya pasi hizo 425 zikifika sehemu zilizokusudiwa, wakati pasi 85 zikipotea.

Mpambano huo kwa ujumla ulikuwa na mvuto wa aina yake na ulitawaliwa na nidhamu ya hali ya juu kwa upande wa timu zote.

Tulishuhudia kadi nne za njano zikitoka kwenye mchezo huo, kila upande ukilambwa kadi mbili, hakukuwa na kadi nyekundu.

Walioonyeshwa kadi kwa upande wa Simba ni Method Mwanjale na  Niyonzima, wakati Juma Abdul na Kelvin Yondan wakilimwa kwa upande wa Yanga.

Mwamuzi wa mchezo huo, Elly Sassi, alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutafsiri sheria 17 za soka na hapakuwa na malalamiko makubwa kutoka kila upande na hili tunatarajia kuliona likiendelea hata katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles