23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

OMOG AKINGIWA KIFUA SIMBA

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

BAADA ya mashabiki wa Simba kupaza sauti zao wakitaka mabadiliko katika benchi lao la ufundi, uongozi wa Wekundu hao umemkingia kifua kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog, baada ya kusema unaendelea kumpa muda ukiamini atawapa mafanikio.

Simba juzi ilichomoza na ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya Yanga katika pambano la Ngao ya Jamii lililopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, kabla ya kufikia hatua ya kupigiana penalti, timu hizo zilimaliza dakika tisini kwa suluhu.

Katika mchezo huo, baadhi ya mashabiki wa Simba wakati wa mapumziko walionekana wakiwa vikundi vikundi  wakijadili kiwango cha timu yao ambapo walimtupia lawama kocha wao, Joseph Omog, wakidai alishindwa kuwaunganisha wachezaji wake, hivyo kusababisha ikose makali ya kutosha.

Mashabiki hao wanaamini kikosi cha timu hiyo kina wachezaji wenye ubora wa hali ya juu baada ya uongozi wao kufanya usajili wenye thamani ya Sh bilioni 1.8, hivyo kitendo ya kushindwa kuifunga Yanga ndani ya dakika 90 ni fedheha kwao.

Walienda mbali kwa kuutaka uongozi wa klabu yao kumfungashia virago kocha huyo na kusaka mwingine ambaye atakifanya kikosi chao kicheze soka linaloendana na thamani ya wachezaji  kilichonao.

Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Simba, Mohamed Hussein ‘Muddy Kigoma’, alisema uongozi wa klabu hiyo hauna mpango wa kuachana na Omog kwa sasa badala yake unaendelea kumpa muda zaidi kwa kuwa unaamini atawafanyia makubwa.

“Tumwache kocha afanye kazi yake, hizi tabia za kumwingilia tuachane nazo, kama uongozi tunaamini ni kocha mzuri,” alisema Muddy Kigoma.

Katika dirisha la usajili wa msimu ujao, Simba ilifanikiwa kuwasajili nyota kadhaa waliopata kuwika katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Miongoni mwao ni kiungo wa zamani wa Yanga, Mnyarwanda Haruna Niyonzima ambaye usajili wake kwenda Msimbazi ulikuwa mjadala mkuu wakati huo.

Katika kuonyesha kwamba hawakuridhishwa na kitendo cha kiungo huyo kutimkia Simba, baadhi ya wanachama wa Yanga walifikia uamuzi wa kuchoma jezi namba nane  iliyokuwa ikivaliwa na mchezaji huyo.

Simba pia ilifanikiwa kuwasajili mshambuliaji wao wa zamani, Emmanuel Okwi kutoka SC Villa ya Uganda, aliyekuwa kipa wa kutumainiwa wa Azam FC, Aishi Manula na mshambuliaji wa timu hiyo, John Bocco.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles