33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Nimeridhishwa ujenzi wa kivuko Mafia – Majaliwa

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameridhishwa na ujenzi wa kivuko cha Mafia ambacho kitatoa huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Nyamisati na Mafia.

Ujenzi wa kivuko hicho chenye urefu wa mita 36 na upana mita 12, umefikia asilimia 95 na kina uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 100. Ujenzi huo umegharimu kiasi cha Sh bilioni 5.3.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya kivuko hicho jana, katika karakana ya Kampuni ya Songoro Marine iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam, Majaliwa alisema ujenzi wake ni mkakati wa Serikali wa kuendelea kujenga vivuko vinavyokwenda kwenye visiwa vilivyopo nchini.

“Ujumbe kwa wana-Mafia ni kwamba meli hii tunatarajia ianze kuingizwa kwenye maji kuanzia mwezi ujao, baada ya kila kazi kukamilika na Tasac kuja kujiridhisha kwamba ubora wa chombo hiki umekamilika, tunaamini wana-Mafia sasa kero yao itakuwa imeisha,” alisema Majaliwa.

Alisema wananchi wa Mafia wanasubiri kwa hamu kuona kivuko hicho kikianza safari zake kurahisisha huduma za usafiri ikiwamo biashara. 

Majaliwa alitoa wito kwa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) kuisaidia Kampuni ya Songoro Marine kuhakikisha mzigo wa vifaa vya ukamilishaji wa kivuko hicho unapofika bandarini unatoka haraka ili Marine wakamilishe taratibu zao.

Alisema ujenzi wa vivuko unawapa uhakika Watanzania wa kuunganishwa na maeneo yote nchini ili kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi, kurahisisha mawasiliano na kurahisisha gharama za usafiri.

Aliipongeza Kampuni ya Songoro Marine kwa ujenzi wa vivuko vyenye ubora wa hali ya juu.

“Sasa Serikali ina uhakika na kampuni ya utengenezaji wa vivuko nchini kwa sababu ya uwezo wake wa kukamilisha kazi kwa wakati na ubora,” alisema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles