24.7 C
Dar es Salaam
Saturday, April 13, 2024

Contact us: [email protected]

‘NILIMWOKOA EBOUE SAA NANE USIKU’

NA SOSTHENES NYONI-MTANZANIA


MTANZANIA, Yasmin Razak, ameeleza namna alivyokutana na nyota wa zamani wa Arsenal na timu ya Taifa ya Ivory Coast, Emmanuel Eboue, kabla ya kumpa hifadhi nyumbani kwake.

Eboue alikutana na majanga hayo baada ya mahakama moja nchini Uingereza kutoa uamuzi wa kuvunja ndoa yake na aliyekuwa mkewe.

Mbali ya kuvunja ndoa hiyo, mahakama  hiyo ilimtaka mchezaji huyo kuondoka katika jumba alilokuwa akiishi na familia yake pamoja na kunyang’anywa mali zake nyingine ili zikabidhiwe kwa mtalaka wake.

Akifafanua kwa kina sakata hilo jijini Dar es Salaam ambako yupo kwa shughuli binafsi, Yasmin, alisema kitendo kilichomtokea mchezaji huyo kinapaswa kuwa darasa kwa wanasoka wengine wa Afrika.

“Kimsingi mimi nafahamiana na wachezaji wengi nyota kule Uingereza hasa wa Afrika si Eboue tu, mimi ni kama dada yao na nimekuwa nikiwasaidia kwa mambo mengi ukiwemo ushauri.

“Kimsingi nilimhifadhi Eboue kwangu baada ya kutimuliwa katika nyumba yake kwa amri ya polisi, nakumbuka ilikuwa Januari mwaka jana aliponipigia simu saa nane usiku,” alisema Yasmin.

“Aliniambia sina pa kwenda, niliwasha gari nikamfuata, nikamchukua nikamleta nyumbani kwangu nikaishi naye kwa miezi mitatu, baada ya hapo alikuwa anaondoka na kurudi, wakati huo alikuwa anaenda kwa marafiki zake Waafrika wengine wanaoishi miji mingine.”

Yasmin anasema baada ya sakata hilo, alimtafutia mwanasheria ambaye alimsaidia kurudishiwa mojawapo ya nyumba zake na wakati huo walikata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama kumpora mali.

“Ukiangalia matatizo yote haya yametokana na ukosefu wa elimu, kwani wakati mahakama inaendesha kesi, hakuweka mwanasheria, pia alikuwa haudhurii, hii ilikuwa fursa tosha ya mkewe kuidanganya mahakama,” alisema Yasmin.

Aliwataka wachezaji wa Afrika hasa wanaocheza soka barani Ulaya  kuhakikisha wanakuwa na wanasheria watakaowasimamia mambo yao ikiwemo mikataba ili kuepukana na kilichomkuta Eboue.

“Kuna mengi yapo nyuma ya wachezaji  wa Afrika, wengi hawajasoma kutokana na kutoka familia za kimasikini, wakipewa pauni 50,000 kwa wiki wanachanganyikiwa, wanapaswa wawe na wanasheria.

“Binafsi huwa nawasiliana sana na Mbwana Samatta, huwa namwelekeza mambo mengi,” alisema Yasmin ambaye ameweka makazi jijini London.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles