24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

BENKI 5 KUFUNGWA

 


BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imezifutia leseni benki tano kwa kushindwa kutekeleza mpango mkakati wa kuongeza kiwango cha mtaji kinachotakiwa cha Sh bilioni mbili kila moja.

Benki hizo ni Covenant Bank for Women Ltd, Efatha Bank Ltd, Kagera Farmers Cooperative Bank, Njombe Community Bank na Meru Community Bank ambazo amana zake inafikia Sh bilioni 67.8 sawa na asilimia 0.38 za amana zote zilizopo kwenye sekta ya fedha.

Aidha, benki za Kilimanjaro Cooperatives, Tanzania Women’s Bank (benki ya wanawake) na Tandahimba Community Bank zimepewa muda wa miezi sita kuanzia Januari hadi Juni 30 mwaka huu kuhakikisha zinaongeza mtaji wake vinginevyo nazo zitafungwa na kuwekwa chini ya ufilisi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Gavana anayemaliza muda wake, Profesa Benno Ndulu alisema benki hizo zimeshindwa kukidhi matakwa ya sheria ya kufikisha mtaji wa Sh bilioni mbili kwa kipindi cha miaka mitano.

Alisema benki hizo zilishindwa kuandaa na kuwasilisha  mpango mkakati unaokubalika wa kuongeza mtaji, huku akiwataka wale wanaotoa huduma kwenye benki hizo watafute njia mbadala kwa sababu haziwezi kufanya kazi tena.

“Kutokana na kutotimiza matakwa ya sheria ya kuwa na mtaji kamili na wa kutosha, Benki Kuu imeamua kusitisha shughuli zake zote na kufuta leseni za biashara ya kibenki  na kuziweka chini ya ufilisi kuanzia Januari 4, 2018,” alisema Profesa Ndulu.

Gavana huyo anayemaliza muda wake alisema  benki hizo tano zilizofutwa zitakuwa chini ya Bodi ya Bima ya Amana.

“Benki Kuu imeiteua Bodi ya Bima ya Amana kuwa mfilisi wa benki tano hizo kuanzia leo (jana) kwa ajili ya ufilisi wa mali na kulipa amana za wateja, wadeni na wanahisa wa benki hizo,” alifafanua.

Aidha Profesa Ndulu aliendelea kufafanua kuwa kabla ya hatua hiyo, benki hizo zilipewa muda wa miaka mitano tangu mwaka 2012 ambapo Benki Kuu iliongeza kiwango cha chini cha mtaji wa benki za wananchi (community banks) kuwa Sh bilioni 2 kutoka Sh milioni 250.

Hata hivyo wateja wote wa benki zilizofungwa  watalipwa fedha  zao na Bodi ya Bima ya Amana, ambapo kwa  wale wenye fedha chini ya Sh milioni 1.5 watalipwa fedha zote lakini wale wenye fedha nyingi kwa mfano Sh milion 10 au 300 nao watalipwa Sh milioni 1.5 ambacho ni kiwango cha mwisho,” alisema Profesa Ndulu.

Alisema Benki hizo zilipewa muda wa miaka mitano ili kuongeza mtaji kufikia kiwango kipya ambao uliisha Juni 30, waka jana na ukaongezwa kwa miezi sita iliyoishia Desemba 31, 2017.

“Jumla ya benki nane hazikuweza kuongeza mtaji kufikia kiwango kamili kilichohitajika. Benki tano kati ya hizo zilishindwa kuandaa na kuwasilisha Benki Kuu mpango mkakati unaokubalika wa kuongeza mtaji na kuzifanya endelevu,” alisema Profesa Ndulu.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mabenki wa BoT, Kened Nyoni alishindwa kutoa idadi ya wateja wa benki hizo zilizofutwa, licha ya Profesa Ndulu kumtaka afanye hivyo kwa waandishi wa habari.

Hatima ya benki tatu

Aidha Profesa Ndulu alieleza kuwa benki za Kilimanjaro Cooperatives, Tanzania Women’s Bank na Tandahimba Community Bank ambazo kiwango cha mtaji hakikidhi, zimewasilisha benki kuu mpango mkakati unaokubalika wa kuongeza mtaji na kuzifanya ziwe endelevu.

Hatima ya wateja wa benki zilizo chini ya ufilisi

Kwa mujibu wa Benki Kuu, Bodi ya Bima ya Amana (DIB) inasimamia benki yoyote iliyofilisika na kuchukua dhamana ya kulipa fidia ya bima wateja wenye amana (depositors) wanaodai benki pamoja na wanahisa.

Alisema Bodi ya Bima ya Amana inawalipa wenye amana wote kwa kiasi cha ukomo wa Sh milioni 1.5 ambapo wenye amana hupewa kipaumbele, na fedha zikibaki wanaoidai benki hulipwa na wanahisa wanakuwa wa mwisho kulipwa kama fedha zimebaki.

“Naamini zaidi ya asilimia 90 ya wenye amana kwenye benki hizi watalipwa fedha yao kikamilifu kwa sababu wengi wao ni wateja wadogo wadogo,” alisema.

Pia alielezea kuwa baada ya wenye amana kulipwa na fedha zimebaki wanayoidai benki watalipwa na zikibaki tena wanahisa ndio wanalipwa wakiwa wa mwisho.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana, Richard Malisa, alifafanua kuwa sheria inataka wafanye haraka iwezekanavyo na wanajipanga kuanza kazi ya kufuatilia benki zilizo chini ya ufilisi.

“Kwa mujibu wa sheria ya kimataifa, huchukua siku saba kuanza kulipa wenye amana lakini kutoka na mfumo wetu wa ndani mwezi moja tutakuwa tumekamilisha na kutoa taarifa,” alisema Malisa.

Bodi ya Bima na Amana itakuwa na jukumu la kukusanya madeni ambayo benki zilizofilisiwa zinadai na kumiliki kila mali za benki na kufanya taaratibu zote za ulipaji wa wateja wake.

Athari kwenye sekta ya fedha.

Profesa Ndulu alifafanua kuwa kufungwa kwa benki hizo tano hakuwezi kuathiri sekta ya fedha nchini kwa kuwa hizo ni benki ndogondogo.

“Hizi benki nyingi ni ndogo haziwezi kuleta mtikisiko kwenye sekta ya fedha kwa sababu shughuli zake ni ndogo zikifananishwa na sekta ilivyo kwa ujumla wake,” alisema.

Katika mkutano huo gavana huyo aliwataka wale wanaotoa huduma kwenye benki hizo watafute njia mbadala kwa sababu haziwezi kufanya kazi tena.

Matatizo ya benki ndogondogo

Alifafanua kuwa  mtikisiko mkubwa unaozikumba benki ndogo ni kutokana na wigo wa biashara zao.

“Mara nyingi uwigo  wa biashara yao ni mdogo na hawajawahi kufikia wakaanza kupata faida, kitu kinachokua ni mtaji, ukubwa bodi, na gharama zingine za uendeshaji ambazo kwa kawaida zinahitaji kuhimili ukiwa na biashara iliyokubwa zaidi,”…….

Kwa habari zaidi, jipatie nakala yako ya MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles