24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

KESSY ALINDA HESHIMA YANGA

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM


BAO la dakika 90 la beki Hassan  Kessy limeipa Yanga ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKU katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Amaan,Unguja.

Kwa ushindi huo,Yanga imefikisha pointi sita na kukamata nafasi ya pili katika kundi A baada ya kushuka dimbani mara mbili.

Singida United inakamata usukani katika kundi hilo ikiwa na pointi sita sawa na Yanga lakini ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Mlandege ipo kwenye nafasi ya tatu,ikiwa na pointi sita kama ilivyo kwa Yanga na Singida,lakini ikitupwa chini kutokana na wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.Hata hivyo Mlandege tayari imecheza michezo minne.

JKT wapo nafasi ya nne wakiwa na pointi nne sawa na Taifa Jang’ombe walioko nafasi  ya tano kutokana na tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa,wakati Zimamoto inakamata mkia ikiwa na pointi tatu.

 

Mchezo huo ulianza kwa kasi,ambapo dakika ya tisa mkwaju wa Chande Faki wa JKU ulipaa juu la lango la Yanga.

JKU iliendelea kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Yanga, huku ikimiliki sehemu kubwa ya mchezo huo na kuwafanya mabeki wa Yanga,Nadir Haroub ‘Canavaro’ na Kelvin Yondan kufanya kazi ya ziada kuzuia wavu wao usiguswe.

Dakika ya 12 Canavarro alionyeshwa kadi ya njano  baada ya kumfanyia madhambi,Nassor Bakar wa JKU.

Yanga ilizinduka dakika ya 15, ambapo mshambuliaji Matheo Antony akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga alipiga shuti lililopaa.

Dakika 34,Yanga ililifikia lango la JKU,lakini Juma Mahadhi alipiga kichwa kilichopaa.

JKU  ilirudi mchezoni  dakika ya 35, ambapo kiki kali ya   Faki ilitoka nje kidogo ya lango la Yanga.

Dakika ya 40 kiungo wa Yanga alimjaribu kipa wa JKU,lakini kiki yake ilipaa.

Dakika ya 41,Yanga ilifanya mabadiliko,alitoka Matheo na nafasi yake kuchukuliwa na Yohana Mkomola.

Mabadiliko yalionekana kukiongezea nguvu kikosi cha Yanga,ambapo dakika ya 44m, Mkomola nusura aiandikie timu yake bao la kuongoza lakini kiki yake ilitoka nje kidogo ya lango la JKU.

Dakika 45 zilimalizika kwa timu hizo kutoshana nguvu,kipindi cha pili Yanga ilifanya mabadiliko,  alitoka Canavarro na kuingia Raphael Daud,pia alitoka Mahadhi na nafasi yake kuchukuliwa na Said Mussa.

Mabadiliko hayo kwa kiasi fulani yaliongeza kasi ya mashambulizi ya Yanga kuelekea kwa wapinzani wao JKU.

Dakika 49 mpira wa kichwa wa  Raphael Daud akiunganisha faulo iliyochongwa na Haji Mwinyi uliokolewa na kipa wa JKU.

Dakika ya 54,JKU  ilifanya mabadiliko,alitoka Nassor Musa na kuingia Salum Mussa.

Mabadiliko hayo yalikuwa na tija kwa JKU kwani dakika ya 56 ilifanya shambulizi langoni mwa Yanga,lakini kiki ya  Faisal Salum ilitoka nje kidogo ya lango.

 

Yanga ilifanya  mabadiliko mengine dakika ya 58,  alitoka Emmanuel Martin na kuingia Ibrahim Ajib.

Ajib aliongeza nguvu kwa kiasi kikubwa katika kikosi cha vijana hao wa Jangwani.

Dakika ya 63,kiki ya Yohana Mkomola baada ya kupokea pasi ya Ajib iliishia mikononi mwa kipa wa JKU.

Faisal Salum nusura awaiue mashabiki wa JKU dakika ya 65,lakini shuti shuti kali lilitoka nje kidogo ya lango la Yanga.

Dakika 68 Saidi Mussa wa Yanga alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Faisal.

JKU  itajilaumu yenyewe kwa  kushindwa kutumia vema nafasi iliyopata dakika ya 75 baada ya kutokea piga ni kupige kwenye lango la Yanga,lakini kiki ya  Mayunga kukosa macho .

Yanga walifanya mabadiliko mengine dakika ya 76, ambapo alitoka Tshishimbi na nafasi yake kuchukuliwa na Geofrey Mwashiuya,wakati dakika ya 82,JKU ilifanya mabadiliko alitoka Mbaruk Faki na kuingia Salum Said.

 

Wakati mashabiki wakianza kuinua vitini wakijua pambano hilo ni sawa,Kessy aliwapa furaha mashabiki wa Yanga baada ya kupachika bao safi dakika ya 90.

Kessy alifunga bao hilo baada ya kupokea pande murua la kisigino la Pius Biswita,kabla ya kufunga bao hilo wawili hao waligongeana vema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles