Na MWANDISHI WETU
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imetoa ripoti ya utafiti wa asali yenye chembechembe za kemikali ya nikotini iliyofanyiwa majaribio na kuonyesha kwamba haina madhara kwa binadamu.
Akizungumza jana, Meneja Mawasiliano wa TFS, Glory Mziray alisema wamekuwa wakikusanya sampuli kila baada ya miaka miwili kutoka kwa wafugaji nyuki na kuzipeleka kwenye maabara za kimataifa.
Alisema mara zote zimekutwa na ubora wa hali ya juu unaokidhi masoko ya taifa na mataifa.
Mziray alitaja utafiti uliofanyika mara mbili mwaka 2016 kuwa lengo lilikuwa ni kuainisha madhara ya ufugaji nyuki kwenye maeneo yanayolima tumbaku.
Aliyataja maeneo ambayo yaliyofanyiwa utafiti huo kuwa ni mikoa ya Tabora na Kigoma.
Mziray alisema utafiti huo ulionyesha kuwa kiwango cha nikotini kinachopatikana kwenye asali iliyochavushwa katika mikoa inayolima tumbaku ni sawa na nikotini inayopatikana kwenye asali ilivyochavushwa na mimea mingine.
Alisema watumiaji wa asali wamekuwa wakihukumu uwepo wa nikotini kwenye asali kwa kuangalia rangi,uchungu lakini asali ya Tanzania inatengenezwa kwa mchanganyiko wa maua ya mimea mbalimbali jambo ambalo linathibitishwa si nikotini peke yake ndiyo inasababisha uchungu bali mimea mingine kama vile muarobaini.
Mziray amewataka watumiaji wa asali kuendelea kuitumia kwa vile ni chakula cha asili kinachotengenezwa kwa mchanganyiko wa mimea mbalimbali.
Alisema asali ni mchanganyiko wa maji, sukari (fruktosi, glukosi, sakrosi) madini na vitamin ambayo inaleta afya kwenye mwili wa binadamu na si vinginevyo.