26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO, KUBENEA KUHOJIWA KAMATI YA MAADILI

Na MAREGESI PAUL-DODOMA


SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ameziagiza kamati mbili za Bunge, ziwahoji wabunge wawili wa upinzani, Saed Kubenea (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), baada ya kutuhumiwa kwamba wametoa kauli zisizofaa juu ya Bunge na Spika.

Akizungumza bungeni jana, Spika Ndugai aliiagiza Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, imhoji Kubenea ambaye ni Mbunge wa Ubungo, baada ya kukaririwa akiwa katika kanisa moja akizungumzia tukio la kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).

Pia, Spika aliiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, imhoji mbunge huyo kutokana na kauli yake aliyoisema kanisani humo kwamba Spika Ndugai ni mwongo kwa kuwa alitaja idadi chache ya risasi zilizotumika kumshambulia Lissu wiki iliyopita.

Kuhusu Zitto, Spika Ndugai aliiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, imhoji mbunge huyo baada ya kukaririwa katika mitandao ya kijamii, akilalamikia uamuzi wa Spika wa kutoruhusu taarifa za kamati za kuchunguza madini ya tanzanite na almasi, zijadiliwe bungeni.

“Kuna mjadala umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu juu ya ni chombo kipi kati ya Bunge, Serikali na Mahakama, kina nguvu kuliko chombo kingine.

“Kuna watu wanasema Bunge ndilo lenye nguvu kwa sababu ndilo linalotunga sheria, wengine wanasema Serikali ndiyo ina nguvu kwa sababu inatekeleza sheria zilizotungwa na Bunge na wanaosema mahakama ndiyo ina nguvu wanasema hivyo kwa sababu ndicho chombo kinachotafasiri sheria.

“Kwa hiyo, nawaomba wabunge tuwe makini tunapolizungumzia Bunge kwa sababu wakati mwingine tunamweka Spika katika ‘bad light’, jambo ambalo si jema kabisa.

“Pamoja na hayo, mbunge mwenzetu Kubenea amekuwa mara kadhaa akitoa kauli zinazolifedhehesha Bunge na kuna maneno ameyasema madhabahuni hivi karibuni kuhusu tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

“Katika maelezo yake, inaonekana mheshimiwa Kubenea analijua vizuri tukio hilo, hivyo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge imwite ili imhoji ili aweze kusaidia upatikanaji wa taarifa muhimu.

“Pia, mheshimiwa Kubenea amesema mimi nililidanganya Bunge kwa sababu nilitaja idadi ndogo ya risasi zilizotumika kumshambulia mheshimiwa Lissu wakati akijua mimi nilitoa taarifa ya Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Dodoma.

“Sasa basi, kwa kuwa amesema mimi nililidanganya Bunge, aitwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili aeleze nililidanganyaje Bunge.

“Naagiza popote alipo mheshimiwa Kubenea, ahojiwe na Kamati ya Adadi (Adadi Rajabu, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama) kesho na afike kwa utaratibu wowote ule,” alisema Spika Ndugai.

Akizungumzia suala la Zitto na kamati za kuchunguza biashara ya tanzanite na almasi, Spika alisema kauli za mbunge huyo ni za upotoshaji kwa kuwa kamati hizo ziliundwa na Spika na hivyo hakukuwa na haja ya kuziwasilisha bungeni kwa ajili ya mjadala.

“Zitto amezungumzia suala la taarifa za kamati kutowasilishwa bungeni wakati kamati hizo niliziunda mimi na si Bunge.

“Siku zote, kamati au tume huundwa kutokana na mapendekezo ya wabunge baada kuwa nimewahoji na nyie mkakubali.

“Inapotokea hivyo, taarifa itakayoandaliwa na kamati au tume husika, basi italetwa bungeni kwa ajili ya mjadala kwa sababu Bunge ndilo lililokubali kuundwa kwa kamati husika.

“Sasa, naomba niwaulize ni lini wabunge mliulizwa hapa juu ya kuundwa kwa kamati za tanzaniate na almasi mkakubali ziundwe?

“Ninavyojua mimi, ni mimi Spika ndiye niliyeona busara, nikaziunda mimi na nikasema zitakuwa kamati za ushauri kwa Serikali na nikasema watakapokuwa kazini, watafuata mambo haya na watakapokamilisha kazi zao, wataniletea ripoti zao.

“Kwa hiyo, huyu Zitto naye lazima ahojiwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa sababu ameonekana kunituhumu mimi wakati kamati hazikuundwa na Bunge,” alisema Spika Ndugai.

Pamoja na hayo, Spika alionekana kumshutumu Zitto kwa kutofika bungeni bila taarifa tangu Bunge lilipoanza Septemba 5, mwaka huu.

Baada ya uamuzi huo wa Spika Ndugai, Zitto aliandika katika akaunti yake ya Twitter  ambapo alisema kuwa anamuheshimu lakini kiongozi huyo amekuwa haoni heshima ya Bunge ikiporomoka.

“Anajua ninavyomheshimu (Ndugai). Kama imefikia haoni heshima ya Bunge inavyoporomoka namsikitikia. Nitakwenda Kamati ya Maadili amekuwa Spika wa kwanza katika historia ya nchi yetu kushuhudia mbunge anapigwa risasi mkutano wa Bunge ukiendelea,” alisema Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles