24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

UVAMIZI OFISI ZA WAKILI WA MANJI WAIBUA HOFU

Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM


UVAMIZI wa ofisi ya Wakili wa Yusufu Manji, Hudson Ndusyepo, umeibua hofu kubwa miongoni mwa baadhi ya mawakili ambao baadhi wamedai wako tayari kufanya kazi bila kuogopa ili kuinusuru taaluma ya sheria.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutotaja majina yao kwa ajili ya usalama walisema wamepokea taarifa hizo za uvamizi kwa masikitiko makubwa na wamepata hofu kwa kitendo cha uhalifu kuendelea kutokea katika ofisi za mawakili wakitolea mfano Kampuni ya Uwakili ya IMMA ilivyolipuliwa hivi karibuni.

“Tutapambana tu maana mwanasheria ukianza kuogopa kuvamiwa ni bora ukaacha kufanya kazi ya kuwakilisha wananchi mahakamani uende shamba ukalime.

“Ukishindwa kufanya kazi kwa kuogopa bora ukalime….afadhali tumeanza kufahamu mapema ili kila mmoja achague upande anaohitaji lakini hatutakiwi wote kuwa na mawazo yanayofanana ya hofu…lazima wengine tujitoe kufanya kazi bila kuogopa.

“Mwanasheria huwezi kukwepa chochote kwa sababu kila unayemwakilisha hasa katika kesi za jinai wapo watu nyuma wasiopenda uwakilishi wako,”alisema.

Wakili mwingine alipohojiwa ili kupata maoni yake alijibu kwa maneno machache kwa huzuni.

“Mmeamua kutuvamia…endeleeni kutuvamia,”alisema.

Akizungumzia uvamizi huo, Wakili Ndusyepo alisema ni kweli walivamiwa katika ofisi zao na wavamizi walichukua kabati la kuhifadhia nyaraka mbalimbali ikiwemo leseni ya ubia wa uwakili.

Inadaiwa watu wanane wanaodaiwa kuwa ni wahalifu walivamia Jengo la Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza  Upanga jijini Dar es Salaam na kufanya uharibifu wa mali mbalimbali za wapangaji.

Jengo hilo la Prime House lina ofisi na kampuni mbalimbali ikiwamo ofisi ya Wakili Ndusyepo , duka la dawa na sehemu ya kufanya mazoezi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni alithibitisha ni kweli tukio lilitokea kuanzia saa 8 hadi 9 usiku wa kuamkia jana.

 

Alisema hawezi kusema wahalifu walilenga ofisi gani maana zipo ofisi nyingi katika jengo hilo aliomba apewe nafasi ya uchunguzi kisha watatoa taarifa.

Manji anakabiliwa na kesi mbili tofauti za jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo moja wapo ni ya uhujumu uchumu.

Katika kesi ya uhujumu uchumi mbali na Manji, washtakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Deogratius Kisinda, Abdallah Sangey na Thobias Fwere.

Katika kesi hiyo, Manji na wenzake wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na Usalama wa Taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200 na mihuri.

Katika kesi ya pili Manji anashtakiwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya Heroine na kesi hiyo iko katika hatua ya utetezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles