BADI MCHOMOLO
KWENYE uwanja wa Wembley leo hii kwa mara ya kwanza fainali itakuwa inapigwa bila ya mashabiki huku Arsenal ya kocha Mikel Arteta ikipambana na Chelsea ya Frank Lampard kwenye Kombe la FA.
Kwa mara ya kwanza makocha hao walianza kazi Ligi Kuu England mwaka mmoja 2019, huku Lampard akiwa mmoja kati ya makocha ambao hawakupewa nafasi kubwa ya kufika hapo alipo bila ya kufukuzwa kazi sambamba na Arteta kutokana na presha ya timu hizo, lakini wote wamefanikiwa kufika fainali.
Huu utakuwa mchezo wenye mbinu nyingi hasa kwenye sehemu ya safu ya kiungo kutokana na historia ya makocha hao kucheza nafasi ya viungo wakati wapo wachezaji.
Arteta alipita katika klabu mbalimbali, lakini sehemu ambazo alicheza sana ni Everton akicheza jumla ya michezo 162 ya Ligi Kuu England kuanzia mwaka 2005 hadi 2011 na baadae kujiunga na Arsenal kuanzia 2011 hadi 2016 alipotangaza kustaafu soka huku akiwa amecheza jumla ya michezo 110.
Lampard yeye alicheza sana katika klabu ya West Ham kuanzia mwaka 1995 hadi 2001 kwa jumla ya michezo 148, wakati huo 2001 hadi 2014 akicheza Chelsea kwa jumla michezo 429 ya Ligi Kuu.
Lampard mwenye miaka 42, ameanza vizuri msimu huu, amemaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi, hivyo atashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.Â
Arteta mwenye miaka 38, ambaye aliichukua Arsena katikati hajafanya vizuri na hajafanya vibaya japokuwa timu imemaliza nafasi ya nane, lakini akifanikiwa kutwaa taji hilo itakuwa heshima kubwa kwake.
Historia
Lampard mbali na kuwa ni msimu wake wa kwanza, lakini alifanya vizuri akiwa na klabu ya Ligi Daraja la Kwanza Derby County hadi play-off. Hapo ndipo safari yake ya kupewa jukumu la kuifundisha klabu yake pendwa Chelsea.
Huku Chelsea ikiwa imefungiwa kusajili kwa misimu miwili, Lampard alionesha ubora wa hali ya juu kwa kuwatumia wachezaji wengi vijana kama vile Mason Mount, Tammy Abraham na Reece James na kumpa matokeo mazuri.
Kama Lampard ataweza kutwaa taji hilo la FA na vile alivyomaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ni heshima kubwa sana kwake na utakuwa mwanzo mzuri wa maisha yake ya ukocha.Â
Arteta yeye alijiunga na Arsenal akitokea kuwa kocha msaidizi wa Pep Guardiola ndani ya klabu ya Manchester City na kuja kuchukua nafasi ya Unai Emery.
Matokeo yake yameanza kuonekana kiasi fulani ambapo Arsenal bado wanaamini kuna kitu kutoka kwake hapo baadae. Mchezo wa leo atahakikisha anashinda ili kuwafanya baadhi ya wachezaji wake waweze kuongeza mikataba mipya kama vile Pierre-Emerick Aubameyang.
Uzoefu
Kila mchezaji anajua umuhimu wa mchezo huu wa leo. Kocha wa Chelsea, Lampard amefanikiwa kuchukua taji hilo mara nne akiwa mchezaji wa Chelsea.
Wakati huo Arteta amefanikiwa kutwaa Kombe hilo mara mbili akiwa mchezaji wa Arsenal mwaka 2014 na 2015, kama atafanikiwa kuchukua leo, imani ya mashabiki na viongozi itazidi kuwa kubwa.
Msimu huu wawili hao wamefanikiwa kukutana mara mbili, mara ya kwanza ArsenalÂ
walikubali kichapo cha mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Emirates, Desemba 29, kabla ya kukutana tena kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, Januari 21 ambapo mchezo huo ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2, huku Arsenal wakiwa 10 uwanjani baada ya David Luiz kuoneshwa kadi n y e k u n d u dakika ya 26.
Mbinu
Lampard amekuwa akitumia mifumo mbalimbali kutokana na aina ya timu ambayo anakwenda kukutana naye, hasa mfumo anaoupenda ni 4-2-3-1, pale anapokutana na timu ngumu.
Lakini kuna wakati amekua akitumia 4-3-3 na mfumu huu aliwahi kuutumia kwenye mchezo dhidi ya Liverpool na Manchester City, hapo akiamini kazi kubwa itakuwa inafanywa na Christian Pulisic na Willian kwa kutokea pembeni. Inasemekana kuwa, mifumo hiyo miwili imekuwa ikiwafurahisha wachezaji wa Chelsea.
Arteta kwa upande wake anapenda kutumia 4-2-3-1, lakini kuna wakati anatumia 3-4-3 kama mchezaji wake Nicolas Pepe atakuwa sawa akishirikiana na Aubameyang, Alexandre Lacazette.
Mwonekano
Lampard ni mmoja kati ya makocha ambao wanaonekana kuwa na nidhamu ya hali ya juu, siku zote amekuwa muwazi wakati wa mahojiano na hata kama timu yake imefanya vibaya hashindwi kuwatupia lawama wachezaji wake.
Msimu huu alionekana mara moja akirushiana maneno na kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp wiki moja iliopita. Endapo Chelsea wataendelea kumuamini kocha huyo itakuwa na mabadiliko makubwa.
Kwa upande wa Arsenal, wengi walikuwa wanatarajia kuona mifumo ya Gaurdiola ikitumika kutokana na kufanya kazi na kocha huyo kwa mafanikio makubwa.Â
Msimu ujao unaweza kuwa na mafanikio makubwa kwa Arteta kama ataweza kuzitumia vizuri mbinu zake akichanganya na zile za Guardiola, ila lazima ajiweke sawa kwenye suala la usajili.
Arteta hana urafiki na wachezaji kama watashindwa kuonesha kile anachokitaka, amekuwa akimuacha benchi kiungo Mesut Ozil kutokana na kiwango chake pamoja na Matteo Guendouzi kwa siku za hivi karibuni.
Kila kocha kwenye mchezo huu wa leo anawaza mbali sana, hasa kutaka kuweka historia yake vizuri, huku kwa Arsenal wakiutaka ubingwa huo ili kumfanya Aubameyang kubaki kwenye klabu hiyo baada ya kugoma kuongeza mkataba mpya kutokana na timu kushindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini wakishinda kuna uwezekano mkubwa wa kubaki, lakini Lampard yeye anataka kuweka heshima yake.