29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yapania kuvunja rekodi

 WINFRIDA MTOI – DAR ES SALAAM 

SIMBA imejipanga kusomba kila kitu msimu huu bila kuipa nafasi timu nyingine, baada ya uongozi wa klabu hiyo kuweka bayana kuwa unataka makombe yote yatue Msimbazi. 

Mabingwa hao mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watarajia kushuka dimbani kesho, kusaka taji la michuano ya Kombe la Shirikisho maarufu Kombe la Azam(ASFC) dhidi ya Namungo, katika mchezo wa fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga. 

Endapo Simba itaibuka bingwa wa mchuano hiyo, itakuwa imeweka rekodi ya kuchukua mataji matatu tofauti msimu huu, ikizipoteza Yanga na Azam zilizoshindwa kutamba msimu huu. 

Wekundu wa Msimbazi hao walianza msimu kwa kutwaa taji la Ngao ya Jamii kwa kuifunga Azam mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam, kabla ya kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara. 

Kuelekea mechi ya Kombe la Shirikisho, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck alitamba kuwa, lazima waweke rekodi ya tofauti msimu huu kwani ana imani kubwa na ubora wa nyota wake. 

Sven alisema pamoja na hali ya hewa ya Sumbawanga kuwa ya baridi kali, lakini wachezaji wote wapo vizuri kimwili na kiakili, huku akiwasisitiza kuvaa nguo nzito. 

Aliongeza kuwa, katika kuhakikisha malengo yao yanatimia, waliweka jijini Mbeya kujiandaa na mchezo, wakijua hali ya hewa inafanana na ya Sumbawanga. 

“Tunataka kuweka rekodi ya kuchukua mataji muhimu ndani ya msimu mmoja, tayari tumechukua ubingwa wa ligi, bado FA ambao tunacheza siku ya Jumapili (kesho). 

“Maandalizi yanaendelea vizuri, wachezaji wote wapo kwenye hali nzuri, ingawa hali ya hewa ya hapoa ni baridi lakini si tatizo, tutafanya vizuri, nafahamu Namungo ni timu bora yenye wachezaji wa viwango vya juu,” alisema Sven. 

Naye Mejeja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, amewataka mashabiki wa timu hiyo kwenda uwanjani wakiwa kifua mbele kuwasapoti wachezaji wao, kwa sababu wamejipanga kuondoka na kombe hilo. 

“Kama tulivyosema tunataka kuweka rekodi, tumemaanisha na hatutanii msimu huu ni wetu, kila shabiki aliyopo Sumbawanga na maeneo mengine asogee karibu Jumapili tuna jambo letu pale Uwanja wa Mandela,” alisema Rweyemamu. 

Wekundu hao wa Msimbazi , juzi walipata mapokezi makubwa kutoka kwa mashabiki wa klabu hiyo wa mjini Simbawanga, ambao walifurika barabarani kuwalaki. 

Taarifa kutoka mjini humo zinadai kuwa miongoni mwa mashabiki waliojitokeza kuipokea timu hiyo, wapo waliosafiri kutoka nchi jirani ya Zambia, lengo likiwa kumuona mchezaji kiungo Clatous Chama. 

Chama ambaye ni raia wa Zambia, amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Simba. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles