25.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 13, 2024

Contact us: [email protected]

Ni vigumu kutenganisha kodi na Maendeleo- DC Mbarali

Na Veronica Kazimoto- Mbarali

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Reuben Mfune amewaambia wafanyabiashara wa wilayani hapa kuwa, ni vigumu kutengenisha kodi na maendeleo kwani maendeleo ya nchi yoyote ile duniani hutegemea kodi.

Ameyasema hayo wakati wa semina ya wafanyabiashara hao kufuatia kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo imelenga kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi, kusikiliza changamoto zao za kikodi na kupokea maoni kwa ajili ya kuboresha huduma za TRA.

“Kodi huiwezesha Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini. Kwa mfano ujenzi wa barabara za lami, ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa zahanati na ununuzi wa dawa na mengine mengi, yote haya yanatekelezwa kwa kutumia kodi zinazolipwa na ninyi wananchi, alisema Mfune.

Mfune aliwasisitiza wafanyabiashara hao kujenga tabia ya kulipa kodi kwa hiari na kutumia vizuri mashine za kielektroniki za kutolea risiti kwa kutoa risiti kila wanapouza bidhaa na huduma mbalimbali.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wilayani hapo Michael Mwaiteleke alisema kuwa, kampeni hiyo licha ya kutoa elimu ya kodi lakini pia inajenga urafiki kati ya wafanyabiashara na TRA na hivyo kuongeza uhiari wa ulipaji kodi nchini.

“Tunaipongeza TRA kwa kuona umuhimu wa kututembelea kwenye maduka yetu na kutuita kwa ajili ya kutuelimisha masuala ya kodi. Hali hii inajenga urafiki kati yetu sisi na TRA na inatupa hamasa ya kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati”, alisema Mwaiteleke.

Naye Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wilayani hapa Elly Jogofu aliwaambia wafanyabiashara hao kuwa, wawe huru wakati wowote kumuona ofisini kwake au kumpigia simu kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili hasa zinazohusiana na kodi.

“Ofisi yangu iko wazi na namba yangu ya simu mnayo, hivyo naomba mkikutana na changamoto yoyote ya kikodi, msisite kuja kuniona ofisini au kunipigia simu,” aliongeza Jogofu.

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani Mbeya imemalizika na kwamba maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wanaofanya kampeni hiyo wanaelekea mkoani Njombe kwaajili ya kwenda kutoa elimu hiyo kodi katika mkoa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles