21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

DC aonya wanufaika TASAF wanaotumia fedha vibaya

Na Allan Vicent, Igunga

Wakazi wa kata ya Ibologero wilayani Igunga mkoani Tabora wanaonufaika na mpango wa serikali wa kunusuru kaya masikini (TASAF III) wametakiwa kuacha kutumia vibaya fedha wanazopewa ili waweze kujikwamua kimaisha.

Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa wilaya hiyo, John Mwaipopo, alipokuwa akizungumza na wanufaika wa mpango huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa ofisi ya serikali ya kijiji cha Iborogelo katani hapo.

Alisema kumekuwa na malalamiko kuwa baadhi ya wanufaika hususani wanaume hutumia fedha wanazopata kuolea wanawake na wengine kunywea pombe jambo ambalo ni kinyume kabisa na malengo ya kuanzishwa kwa mfuko huo.

Alibainisha lengo la serikali kuanzisha mpango huo kuwa ni kuwezesha kaya zisizo na uwezo kuondokana na umasikini hivyo kila mnufaika anapaswa kuzitumia vizuri kwa ajili ya chakula, kupeleka watoto shule, kliniki ikiwemo kuanzisha  miradi midogo ya kiuchumi mfano ufugaji kuku, mbuzi au kilimo.

“Nawapongeza wale wote walioingizwa katika mpango huo na kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kununulia watoto wao nguo za shule na kupeleka kliniki watoto wachanga, endeleeni kufanya hivyo,” alisema.

Awali akitoa taarifa ya kijiji, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho Juma Mayunga alisema kuwa jumla ya kaya 125 zinanufaika na mpango huo katika kijiji hicho chenye wakazi 4,000 kati yao wanawake ni 2,300 na wanaume 1,700.

 Alisema walengwa wameendelea kupewa mafunzo ya namna ya kuanzisha rasilimali zalishi ili pindi mpango huo utakapoisha waweze kujisimamia wenyewe kiuchumi na kuwa na maisha yaliyo bora zaidi.

 Diwani wa kata ya Iborogelo, Emmanuel Busongo (CCM), aliwataka wanufaika wa mpango huo kutumia fedha wanazopewa kujiongezea kipatao, aliahidi kufuatilia kwa karibu zaidi maisha ya kila mlengwa na matumizi ya fedha wanazopata.

Baadhi ya walengwa kutoka kijiji cha Iborogelo, Amina Maganga na Johari Makala walisema kuwa fedha za TASAF zimewasaidia kuanzisha miradi ya ufugaji kuku na mbuzi ikiwemo kukodi mashamba ya kulima na kukiri kuwa hali zao zimebadilika sana sio kama walivyokuwa huko nyuma.

Mratibu Msaidizi wa TASAF wilayani humo, Richard Mtamani, alisema kuwa jumla ya Sh milioni 274 zimetolewa na serikali ili kuhawilisha maisha ya kaya maskini 4,766 zilizopo katika vijiji 57 wilayani humo kati ya Novemba na Desemba 2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles