27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ni Dk. Shein Z’bar, mabalozi waonya

Ali-Mohamed-SheinNa Mwandishi Wetu, Zanzibar

MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, amemtangaza mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein, kuwa mshindi wa urais kwa kupata kura  299,982  sawa na asilimia 91.4.

Dk. Shein amefuatiwa na mgombea  wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed ambaye amepata kura 9,734 sawa na asilimia 3.0, huku mgombea aliyetangaza kujitoa katika kinyang’anyiro hicho kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, akipata kura 6,076 sawa na asilimia 1.9.

Wagombea wengine na idadi ya kura zao kwenye mabano ni, Khamis Idd Lila wa Chama cha ACT-Wazalendo (1,225), Juma Ali Khatib wa ADA-TADEA (1,562), Said Soud Said wa AFP (1,303), Ali Khatib Ali wa CCK (1,980) na Tabu Mussa Juma wa Demokrasia Makini (210).

Wengine ni Abdallah Kombo Khamis wa DP (512), Kassim Bakari Aly wa Jahazi Asilia (1,470), Seif Ali Idd wa NRA (266), Issa Mohamed Zonga wa SAU (2,018)  na Hafidh Hassan Suleiman wa TLP   kura 1,496.

Jecha alisema   kura halali zilizopigwa ni 328, 327,wakati  zilizoharibika ni 13,538.

Alisema idadi ya wapiga kura wote walioandikishwa ni 503,580.

Kutangazwa  kwa matokeo hayo kumeibua mjadala  ikizingatiwa  CCM ilipata ushindi wa historia tangu ulipoingia mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.

Matokeo hayo yanaakisi tofauti kubwa kati ya matokeo ya mwaka huu na yale ya mwaka 2010 ambako mahasimu wakuu wa  siasa visiwani humo kati ya Dk. Shein na Maalim Seif, walipishana kwa tofauti ya asilimia moja.

Matokeo ya mwaka  2010

Akitangaza matokeo hayo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Khatib Mwinyichande, alisema Dk. Shein alipata kura 179,809 sawa na asilimia 50.1.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Maalim Seif, ambaye amegombea urais kwa mara ya nne, alipata kura 176,338 ambazo ni sawa na asilimia 49.1 ya kura zote 358,815.

Alisema  vyama vilivyosimamisha wagombea urais katika uchaguzi huo, ni   AFP, CCM, CUF, Jahazi Asilia, NCCR-Mageuzi, NRA na Tadea.

“Matokeo yanaonyesha mgombea wa NRA amepata kura 480 (asilimia 0.1), wa CCM kura 179,809 (asilimia 50.1), wa CUF kura 176,338 (asilimia 49.1), Jahazi Asilia kura 803 ( asilimia 0.2), NCCR kura 363 (asilimia 0.1), NRA kura 525 sawa (0.1) na Tadea kura 497 sawa na asilimia 0.1,” alisema Mwinyichande.

Wakati wa kutangaza matokeo hayo aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif alikuwapo   na akakubali kwenda mbele kutoa hotuba ya kukubali matokeo.

“Kwa mara ya kwanza uchaguzi umefanyika kwa amani, bila ya vitisho. Kampeni ziliendeshwa kwa uungwana na kwa ustaarabu,” alisema Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa waziri kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Alisema uamuzi huo umeweka historia mpya ya Serikali ya Umoja wa Taifa na kwamba Wazanzibari wamempa Dk. Shein jukumu la kuongoza kwa mara ya kwanza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Katika hotuba hiyo, Maalim Seif  alitoa tahadhari kwa Dk. Shein na CCM kwa kutaja mambo makuu matatu muhimu.

“Kwanza ni shukrani kwa Tume ya Uchaguzi kwa kuendesha uchaguzi ambao ulikuwa na afadhali kulinganisha na uchaguzi mwingine.

“Lakini kuna dosari ambazo ni lazima zirekebishwe. Mwenye matatizo si wewe mkurugenzi… ni baadhi ya maofisa wako.

“Jambo la pili ni kwamba Dk. Shein ni rais mteule. Ametangazwa tu kuwa mshindi, lakini hakuna mshindi. Washindi ni Wazanzibari wote na Shein ni mteule tu,” alisema.

Maalim alionya katika suala lake la tatu kuwa baada ya matokeo hayo kusiwepo na siasa za kubezana.

“Siasa za kubezana zitachafua hali ya hewa kabisa,” alionya Maalim Seif akimtaka Dk. Shein afikishe ujumbe huo kwa viongozi wenzake wa CCM na wanachama wao.

Kwa upande wake, Dk. Shein  alimshukuru Maalim Seif kwa hotuba yake  aliyoielezea kuwa ilijaa busara na hekima na kuahidi kutekeleza yote ambayo kiongozi huyo wa CUF aliyazungumzia.

“Nafahamu fika kuwa kazi hii ni nzito… Mungu anisaidie, anipe hekima na busara niifanye kwa uadilifu,” alisema Dk. Shein.

Baada ya matokeo ya mwaka 2010, Rais Dk. Ali Mohamed Shein, aliunda Serikali ya Umoja wa Taifa kwa kushirikiana na chama kikuu cha upinzani visiwani humo cha  CUF.

Hiyo ni baada ya pande hizo mbili kufikia maridhiano ambayo yalilifanya Baraza la Wawakilishi kuridhia kupitisha sheria inayoruhusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mwafaka huo ulifikiwa baada ya viongozi wakuu wa vyama viwili, Rais Amani Abeid Karume kukutana kwa faragha Ikulu na  Maalim Seif Novemba 4, 2009.

Matokeo Oktoba 26, 2015

Aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif alizungumza na waandishi wa habari na kutangaza matokeo ya kura ya urais visiwani humo.

Alisema baada ya chama chake kukusanya fomu zote za matokeo kutoka vituoni, yeye alipata kura nyingi.

“Baada ya kukusanya matokeo yote, nimepata kura 200,007 dhidi ya kura 178,363 za mgombea wa CCM anayetetea nafasi yake, Dk. Ali Mohammed Shein,” alisema.

Maalim Seif aliitaka ZEC kutangaza matokeo halisi kama yalivyo kwenye fomu zinazotoka vituoni.

Katiba

MAJIBU; Ibara ya 39 ya Katiba ya Zanzibar inasema

  1. (1). Kutakuwa na Makamu wawili wa Rais ambao watajulikana kama Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais.

(2) Ndani ya siku saba, baada ya kushika madaraka, Rais atateua Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais

(3) Makamo wa Kwanza wa Rais atatakiwa awe na sifa za kumwezesha kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa Rais

Isipokuwa kwamba:-

(i) Iwapo chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa Rais kimepata chini ya asilimia 10  ya kura zote za uchaguzi wa Rais, au

(ii) Endapo Rais atakuwa hana mpinzani,

basi nafasi ya Makamo wa Kwanza wa Rais itapewa chama chochote cha upinzani kilichotokea cha pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.

4) Makamu wa kwanza wa Rais hatakuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi

(6) Makamu wa Pili wa Rais, atateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka chama anachotoka Rais.

Pamoja na hali hiyo, hakuna chama kilichofikisha asilimia 10 ya kura za urais, hivyo kutokana na matakwa hayo ya katiba suala la kuwapo  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ni kitendawili kikubwa kwani hakuna chama cha upinzani kilichopata wajumbe wa Baraza la Wawakilishi zaidi ya CCM.

Dk. Shein anena
Baada ya kutangazwa mshindi, Dk. Shein alivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusema vimefanya kazi kubwa kwa kuituliza nchi na kusisitiza hana mjadala na mtu atakayejaribu kuvuruga amani ya Zanzibar.
wapo watu waliojaribu kufanya vituko katika mitandao ya kijamii na mitaani, lakini anamshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kufanikisha kazi ya kulinda amani ya Zanzibar.
“Dk. Magufuli amefanya kazi kwa vitendo, ameonyesha msimamo wake kwa vitendo juu ya kauli yake ya kuulinda Muungano.

“Zanzibar ni nchi ya amani inajiuza, watalii wanakuja kwa sababu ya amani, inahitaji maendeleo,” alisema Dk. Shein.

 

Tamko la mabalozi

 

Nao mabalozi na wawakilishi wa nchi za Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya (EU), Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Uswisi,  Uingereza na Marekani,  jana wametoa tamko kuhusu uchaguzi huo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana, ilisema nchi hizo zimesema zimesikitishwa na uamuzi wa ZEC kuendesha uchaguzi wa marudio.

“Tumesikitishwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wa kuendesha marudio ya uchaguzi uliofanyika Oktoba  25, 2015 bila kuwapo makubaliano ya pamoja baina ya pande kinzani na ufumbuzi wa mgogoro wa  siasa visiwani humo uliotokana na majadilino baina ya pande husika.

“Ili uwe wa kuaminika na kukubalika, lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa dhati matakwa ya watu.

“Tunarejea wito wetu kwa Serikali ya Tanzania kuonyesha na kuchukua uongozi katika suala la Zanzibar, lazima ufumbuzi wa mgogoro huu upatikane kupitia mazungumzo ya pande husika kwa lengo la kudumisha amani na umoja katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa mara nyingine tunawapongeza wananchi wa Zanzibar kwa utulivu na ustahimilivu waliouonyesha katika kipindi chote cha mchakato huu na kuvitaka vyama vyote na wafuasi wao kuanzisha tena mchakato wa maridhiano ya  Taifa ili kupata ufumbuzi jumuishi, endelevu na wa amani,” ilisema taarifa hiyo.

 

 AWADH

Akizungumzia ushindi wa Dk. Shein, mwanasheria maarufu visiwani hapa, Awadh Ali Said, alisema matokeo hayo yameirudisha nyuma Zanzibar na kuipeleka katika mpasuko.

Alisema hivi  sasa jamii imegawanyika  katika siasa, ingawa zilifanyika juhudi kubwa za kuondoa mpasuko huo na ndiyo maana Katiba ya mwaka 1984 ikabadilishwa na kuondoa  hali aliyeshinda achukue kila kitu.

“Ndiyo tukaweka Serikali ya Umoja wa Kitaifa, demokrasia imejeruhiwa, si rahisi tena wananchi wakaiamini,” alisema Awadh.

Alimtaka Dk. Shein kujiuliza iwapo anakaa madarakani kwa uhalali wa wananchi na kuuungwa mkono kwa sababu anaamini kwa hali ilivyo itakuwa vigumu Zanzibar kupata maendeleo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles