Mwandishi Wetu- Mbeya
MSAJILI wa Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), Vickness Mayao, ameyaondoa mashirika zaidi ya 158 katika rejista ya mashirika yasiyo ya kiserikali.
Hayo yamesema jijini Mbeya na Mkurugenzi Msaidizi Uratibu wa NGOs kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Grace Mbwilo kwa niaba ya mkurugenzi na msajili wa NGOs.
Alisema Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Namba 24 ya mwaka 2002, kama ilivyofanyiwa mabadiliko na Sheria Namba 3 ya mwaka 2019, imefafanua bayana kuwa jukumu la kusajili mashirika yanayoendesha shughuli za kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, utawala bora, haki za kibinadamu na mazingira katika ngazi ya jamii kwa lengo la kutogawana faida na ambazo hazina mrengo wa kukuza biashara, zimeelekezwa kusajililiwa na Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs).
“Mashirika yaliyoondolewa kwenye daftari la msajili wa NGOs ni yale ambayo yalisajiliwa chini ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002 ambayo yanafanya kazi kwa lengo la kunufaisha wanachama wake, kugawana faida, yenye mlengo wa dini, yenye lengo la kukuza biashara na bodi za wadhamini,” alisema Grace.
Alisema hatua ya kuyaondoa mashirika haya kwenye daftari, imefikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Marekebisho Na. 3 ya mwaka 2019 iliyoanza kutekelezwa kuanzia Julai mosi, mwaka huu.
Grace alisema kwa kuzingatia ufafanuzi wa mipaka ya usajili ulioainishwa na Sheria Namba 3 ya Mwaka 2019, msajili wa NGOs, anayakumbusha mashirika yanayofanya shughuli kwa lengo la kugawana faida, yenye mrengo wa dini na ambayo yana malengo ya kukuza biashara, yatafutwa kwenye daftari la msajili, na baada ya kipindi cha miezi miwili kuanzia Julai mosi, mwaka huu, yatahamishiwa chini ya mamlaka nyingine za usajili kutokana na kukosa sifa.