28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Vifo majeruhi ajali lori la mafuta vyazidi kuongezeka

Aveline Kitomary -Dar es salaam

IDADI ya majeruhi wa ajali ya lori la mafuta iliyotokea mkoani Morogoro waliofariki dunia, imefikia 95.

Wakati idadi ikiongezeka, majeruhi Rusuje Mollel (38), ambaye alikuwa akipatiwa matibabu hospitali ya mkoa huo, jana amehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Mollel, anakuwa majeruhi wa 47 waliopokewa hospitalini hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema majeruhi waliobaki ni 20 na wote wamelazwa chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

Aligaesha alisema majeruhia Rajab Ally (32), alifariki dunia usiku wa kuamkia jana na kufanya idadi ya majeruhi waliofariki wakipatiwa matibabu hospitalini hapo kufikia 27.

“Jana mchana tulimpokea majeruhi mmoja ambaye alikuwa akipatiwa matibabu Morogoro, baada ya kuzidiwa ameletwa Muhimbili ili apate matibabu zaidi.

“Lakini usiku wa kuamkia leo (jana), majeruhi mmoja amefariki dunia na kufanya idadi yao kufikia 27 waliofariki dunia, wamebaki 20 na wote wako ICU,” alisema.

WATU WAZIDI KUTOA DAMU

Aligaesha alisema kuanzia Agosti 11, hadi jana, wamefanikiwa kupata chupa 700 za damu ambazo zimetokana na juhudi za watu na makundi mbalimbali waliojitokeza kutoa msaada.

“Mwitikio wa watu kujitokeza kuchangia damu ni mkubwa na tangu Agosti 11, mwaka huu, mpaka sasa tumepata uniti 700, natoa wito kwa makundi, taasisi na watu binafsi waendelee kuchangia damu kwani inatumika hata kwa wagonjwa wengine,” alieleza  Aligaesha.

Jana, zaidi ya watu 50 kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (Chawamata), walitoa damu kwa matumizi ya majeruhi hao.

Akizungumza wakati wa uchangiaji damu, Katibu Mkuu wa Chawamata, Greysona Michael, alisema wao kama madereva wameamua kutoa damu kutokana na kuguswa na tukio lililotokea, hivyo wameamua kuwasaidia majeruhi hao.

“Tumekuja na wanachama wetu zaidi ya 50 kuchangia damu kwa majeruhi wa ajali, suala hili limetugusa sisi kama madereva. Aliyepata ajali ni mwanachama wetu, tunafanya mpango wa kumsaidia,” alisema Michael.

Alisema wanaendelea kupitisha michango katika chama chao ili kuweza kutoa misaada mingine ya vifaa vitakavyoweza kuwasaidia majeruhi hao.

“Hatutaishia tu kutoa damu, wiki ijayo tuna mpango wa kuwasilisha  msaada wa vifaa kwa majeruhi hawa ili kuwatia moyo na kuwafariji. Tunajiona kama sehemu muhimu kwa msaada kwao,” alisema Michael.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles