MSANII wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Ney wa Mitego’, amesema yupo tayari kumtolea dhamana mpenzi wake wa zamani, Siwema ambaye amehukumiwa kwenda jela miaka miwili kwa kosa la kumtukana shabiki kwenye mtandao wa kijamii.
Ney na Siwema walifanikiwa kukaa kwenye uhusiano kwa kipindi kirefu na kufanikiwa kupata mtoto ambaye walimpa jina la Curtis kabla hawajatengana.
Akizungumza na MTANZANIA, Ney wa Mitego alisema: “Mimi na Siwema kwa sasa si wapenzi kila mtu na maisha yake lakini ni mama wa mtoto wangu, niliposikia kuwa amehukumiwa jela miaka miwili sikuwa sawa kabisa kwa sasa napambana kile nitakachoweza kuangalia kama kuna uwezekano wa kumpa msaada.
“Kuna vitu nafikiria kuvifanya ili kujaribu kumsaidia, yeye ni mzazi mwenzangu na tulikaa muda mrefu kwa sasa si mpenzi wangu lakini nawaza kumsaidia kumtolea dhamana,” alisema Ney wa Mitego.