JERUSALEM, Israel
MAMLAKA za dola nchini hapa zimesema zina ushahidi wa kutosha unaoonyesha Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu anahusika na vitendo vya rushwa na ufisadi ingawa yeye anakanusha akidai tuhuma hizo zinasambazwa na wapinzani wake wa siasa.
Polisi hao walisema jana kwamba uchunguzi wao unaonyesha Waziri Mkuu Netanyahu alipokea rushwa kuingilia kati katika moja ya kesi ambazo zilikuwa zikiikabili kampuni kubwa ya mawasiliano ya Bezeq.
Polisi walisema wana ushahidi huo ambao unaonyesha wazi Netanyahu na mkewe Sara, walipokea rushwa hiyo na kufuja fedha hizo kupindisha ukweli.
Katika madai hayo Netanyahu anashuhutumiwa kujichotea mamlioni ya dola katika kampuni hiyo ya Bezeq kuviziba mdomo vyombo vya habari vilivyokuwa vikiripoti kesi hiyo.
Washauri wake wawili waandamizi wamegeuka kuwa mashahidi na wanasema wamezipa mamlaka ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwapo vitendo hivyo.
Waandishi wa habari ambao hapo awali walifanya kazi katika tovuti ya Walla wamewahakikishia polisi kuwa walisumbuliwa na kulazimishwa kuandika habari nzuri tu zinazomuhusu Netanyahu.
Hata hivyo Netanyahu anakanusha taarifa hizo akisema zilianza kusambaa hata uchunguzi bado haujaanza kufanyika.
Kutokana na taarifa hiyo ya polisi kumeibuka wito wa kumtaka Netanyahu ajiuzulu.
“Waziri Mkuu hana tena sifa ya kuendelea kushikilia nafasi yake ni lazima ajiuzulu hata leo,” alisema Tamar Zandberg, ambaye anaongoza Chama chenye mlengo wa kushoto cha Meretz. “Israel ni lazima iingie katika uchaguzi,”aliongeza kiongozi huyo.
Hiyo ni mara ya tatu kwa polisi kutangaza mashitaka dhidi wa waziri mkuu huku mkewe akiwa ameshashitakiwa katika kesi tofauti zinazohusiana na matumizi mabaya ya fedha za serikali.