24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

NDUGAI: NIMEPOKEA BARUA YA KUJIUZULU WAITARA

 

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam


SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema amepokea barua ya kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, aliyejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ndugai alisema hayo jana Ikulu Dar es Salaam, wakati wa hafla ya Rais Dk. John Magufuli kutoa hati za viwanja vilivyopo Dodoma kwa mabalozi 62 wa nchi mbalimbali na mashirika matano ya kimataifa kujenga ofisi na makazi.
“Kwa kuwa nimeambiwa ninaonekana nchi nzima, napenda nitangaze kuwa leo asubuhi nimepokea barua kutoka kwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, kuwa amejivua uanachama wa chama chake na kujiuzulu ubunge,” alisema Ndugai.

Alisema baada ya kupokea barua hiyo, hatua inayofuata ni kuiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili nyingine ziweze kufuata.

“Kilichobakia ni kuiandikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa rasmi Jimbo la Ukonga liko wazi,” alisema Ndugai.
Waitara alitangaza kujivua uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM Jumamosi iliyopita na kwa sasa yuko katika kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma kumnadi mgombea ubunge wa chama hicho tawala, Christopher Chiza.

Katika kampeni hizo, ataungana na wabunge wa chama hicho wanaomnadi mgombea huyo wakiwamo Hussein Bashe wa Nzega Mjini na Nape Nnauye wa Mtama.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wakati akitangaza kujiuzulu, Waitara alisema sababu zilizomfanya kuchukua hatua hiyo ni kutofautiana na viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema baada ya kuhoji kuhusu matumizi ya ruzuku na demokrasia ndani ya chama.

Alisema kuwa alihoji matumizi ya Sh milioni 237 za ruzuku kila mwezi kwani hadi sasa chama hicho hakina ofisi ya makao makuu, kanda wala mkoa.

Pia alisema alitofautiana na viongozi wenzake baada ya Mwenge wa Uhuru kwenda kuzindua miradi ya maendeleo ambayo aliipigania.

“Naambiwa usiende pale (uzinduzi wa mradi) na mimi shida yangu haikuwa CCM, ilikuwa ni miradi niliopigania… Leo nimejiondoa rasmi Chadema, kwahiyo mimi si Mbunge tena, nimetupa jongoo na mti wake.
“Mimi nataka niende mahali ambako kuna kazi za kufanya,” alisema Waitara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles