26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugai ataka wahitimu kutojihusisha na siasa

Koku David -Dar es salaam

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amewataka wahitimu Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kutojihusisha na mambo ya kuandamana yanayoweza kuvuruga amani,badala yake wanatakiwa kujikita  kujiajiri ili kutimiza ndoto zao katika maisha.

Hayo aliyazungumza mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa mahafali ya 46 ya chuo hicho, Dar es Salaam ambapo aliwataka vijana kufikiria kujiajiri baada ya kuhitimu na sio kufikiria ajira au kuingia barabarani kuandamana.

Alisema  vijana ambao ni wasomi wanatakiwa baada ya kuhitimu kwenda kuwa wasomi bora kwa kujikita kujiajiri na kuweza kutoa ajira kwa wengine.

“Hivi sasa vijana wengi waliomaliza darasa la saba ndiyo matajiri wanaotoa ajira kwa wasomi hivyo ifike wakati wasomi nanyi mbadirike kwa kujikita kwenye kujiajiri ili muweze kuwa wasomi bora na wawekezaji wakubwa.

“Msije mkakubali kwenda barabarani kuandamana,i mtakutana na wanaume huko wawavunje miguu bure, mnatakiwa kujikita katika kufikiria kujiajiri kwa kufanya uwekezaji katika masuala mbalimbali ya kilimo, utalii, ufugaji na uvuvi,” alisema Ndugai.

Alisema lazima iwepo tofauti kati ya mtu aliyehitimu elimu ya msingi na chuo kikuu, kwa kuwa wabunifu na kutumia fursa zilizopo kwenye utalii, ufugaji, kilimo, na uvuvi  ili kuondoa dhana iliyopo miongoni mwa jamii kwamba uwekezaji katika ngazi ya juu, si kitu. Aliongeza kuwa vijana ambao wamesoma kwa mkopo wa serikali wanatakiwa kuurejesha ili kuwezesha vijana wengine kuweza kupata mkopo na hatimae kuliwezesha taifa kuwa na wasomi wengi.

Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Thadeus Satta alisema  katika mahafali hayo, kampasi ya Dar es Salaam, wahitimu 3,962 walitunukiwa vyeti na tangu kuanzishwa kwa chuo hicho kimekuwa na mafanikio makubwa katika udahili wa wanafunzi.

Alisema chuo  kilianzishwa mwaka 1972 kilianza kikiwa na wanafunzi 72, hadi sasa kutokana na ongezeko lililopo chuo kimefikia idadi ya wanafunzi waliokwishakuhitimu kuwa ni 12,565 na kozi zimefikia 34 kutoka kozi mbili wakati kikianza.

“Pamoja na mafanikio,zipo changamoto mbalimbali ikiwamo idadi ndogo ya wakufunzi mwalimu mmoja ufundisha wanafunzi 50,o tunaiomba Serikali kutupa kibali cha kutoa ajira kwa wakufunzi ili kupunguza changamoto hiyo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles