29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Spika Ndugai akata mzizi wa fitina

job ndugaiAkerwa Bunge kugawanyika vipande, kutoa msimamo leo

Na Mwandishi Wetu

-DODOMA

SPIKA wa Bunge,  amekata mzizi wa fitina huku akikemea tabia ya baadhi ya wabunge kuwatukuza baadhi watu wengine na wao kuonekana si lolote mbele ya jamii.

Kutokana na hali hiyo, amesema anahitaji kujenga Bunge moja ambalo lilionekana kumekuwa vipande viwili, hasa baada ya wabunge wa Kambi ya Upinzani kususia vikao vyote vilivyokuwa vinaendeshwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Nduguai alitoa kauli hiyo mjini hapa jana, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge, ambapo si jambo la busara kwa wabunge kutukuza watu wengine huku wengine wakififishwa.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Kamati ya Uongozi, kiliambia MTANZANIA kuwa kutokana na hali hiyo, Spika Ndugai alionekana kuwa mkali kwa lengo la kutaka suluhu kwa pande zote za wabunge hasa wale wa CCM na  wale wa upinzani.

Alisema hakubaliani na biashara ya kumtukuza mtu mmoja jambo ambalo alilipinga wazi mbele ya wajumbe hao.

“Kwanza nawapongeza wenyeviti wa kamati kwa kazi nzuri na wote mmewajibika vizuri. Lakini sio kumtukuza mtu mmoja tu. Hili la kumtukuza mtu mmoja na kuwadharau wengine mimi sikubaliani nalo.

“Nilikuwapo kwa siku 35 sote tulifanya kazi nzuri nawapongeza wote. Kuna kauli ya Trump (Donald mgombea urais wa Chama Republican) kwamba ‘I alone Can do’ na  Obama (Barack Rais wa Marekani)  anasema ‘Yes we can’ mimi nachagua hii ya Obama nataka Bunge moja,” alisema Spika Ndugai.

Pamoja na hali hiyo, alisema leo atazungumza na Taifa kuhusu mwelekeo wa Bunge na kutoa msimamo wake hasa kutokana na mazingira ya kikao cha Bunge la bajeti lilivyomalizika.

Licha ya hali hiyo, alisema katika siku 70 za Bunge la Bajeti yeye na Naibu Spika pamoja na wenyeviti wote wa Bunge waliendesha Bunge vizuri.

Akizungumzia ofisi ya wabunge, Spika Ndugai alisema suala la ofisi za wabunge kwa sasa lipo kwenye mazungumzo kati ya Bunge na Serikali, ingawa kwa mwaka huu haziwezi kujengwa kutokana na kutotengewa fedha za bajeti.

Akizungumzia kuhusu kuhamia Dodoma, alisema si jambo la ghafla kama alivyokuwa akisema Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msingwa (Chadema), bali ni sera ya CCM kwa kuwa wamechelewa kwa zaidi ya miaka 40 kutekeleza suala hilo.

Hata hivyo, aliiagiza Serikali kuhakikisha inatoa ratiba inayoeleza ni mawaziri gani wanahamia kwa kipindi hiki ili Bunge liweze kusimamia kidete kuhakikisha wanahamia.

“Waziri Mkuu inabidi atoe ratiba kabisa ili tusimamie mpaka wahamie maana isije ikawa siku chache mnaondoka,” alisema Ndugai

Katika mkutano wa Bunge la bajeti mwaka huu, Kambi yaUpinzani Bungeni ilitangaza kwa wabunge wa kambi hiyo kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge katika vikao vyote vitakavyokuwa vikiongozwa na Dk. Tulia.

Maazimio hayo yalikuja baada ya kuibuka mzozo mwingine katika kikao cha jana jioni kuhusu mjadala wa kutaka sakata la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambapo wabunge walitaka lijadiliwe, lakini Dk. Tulia alipinga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles