NA ESTHER MNYIKA,DAR ES SALAAM
TANZANIA imeigomea Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu ndoa ya jinsia moja, katika mapendekezo ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binadamu.
Kaimu Mkurugenzi wa Katiba na Sheria na Haki za Binadamu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Alecia Mbuya amesema hiyo ni kutokana na mfumo wa nchi wa sheria sera, imani za dini, utamaduni, mila na desturi za nchi.
Akizungumza Dar es Salaam jana alisema mapendekezo 227 yaliyotolewa na nchi wanachama wa UN ili Tanzania iyatekeleze.
Mbuya alisema mapendekezo hayo yamejikita katika majukumu ya kimataifa kwenye mikataba mbalimbali ambayo Tanzania imeridhia.
Baadhi ya mikataba hiyo ni masuala ya katiba na sheria, haki za binadamu na masuala ya watu wenye ulemavu, alisema .
“Baada ya kupitia mapendekezo hayo Tanzania ilikubali kutekeleza mapendekezo 130 ambayo tuliyaona hayakinzani na katiba, sheria na sera zetu za nchi au yanahusu masuala ambayo tayari yapo kwenye hatua za utekelezaji,”alisema Mbuya.
Alisema Tanzania ilikataa kutekeleza mapendekezo 72 ambayo hayaendani na mfumo wa nchi wa sheria ,sera, imani za dini ,utamaduni, mila na desturi.
Baadhi ya mapendekezo ambayo Tanzaninia ilikataa kutekeleza ni kufutwa adhabu ya kifo, ndoa ya jinsia moja, masuala ya ubakaji ndani ya ndoa, na kuridhia mikataba ambayo haiendani na sheria za nchi, alisema.
Alisema mapendekezo 25 hayakutolewa uamuzi na yaliahirishwa kwa kuwa yanahitaji kupata mwongozo kutoka kwenye vyombo vya uamuzi wa sera au yanahitaji fedha kutumika na mapenekezo mengine ambayo yapo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
“Kwa muktadha huo, serikali itajitaidi kuyatekeleza mapendekezo ambayo imeyakubali kwa kushirikiana na wadau wote nchini.
“Tanzania inatakiwa kuwasilisha majibu ya mapendekezo yaliyoahairishwa kabla ya kikao cha 33 cha Baraza la Haki za Binadanu kilichopangwa kufanyika Septemba mwaka huu,”alisema.
Alisema ofisi ya AG inakabiliwa na changamoto nbalimbali ikiwamo kushindwa kutekeleza majukumu muhimu ya ushirikiano wa kanda na kimataifa kutokana na uwezo mdogo wa fedha unaosababisha ushiriki mdogo wa shughuli hizo.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ofisi haijaiwakilisha serikali kwenye majukwaa ya kanda na kimataifa tangu mwaka 2014 na kuchelewesha kuwasilisha taarifa za nchi za haki za binadamu kutokana na ufinyu usiokidhi mahitaji ya ongezeko la majukumu.