24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

N’daw afunga usajili Simba

Guirane-N-Daw-Birmingham-City-1024_2700680MWALI IBRAHIM NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM

MSHAMBULIAJI raia wa Senegal, Pape N’daw, ameifungia usajili klabu ya Simba baada ya juzi kufuzu majaribio yake na kupewa mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia timu hiyo kwenye Ligi Kuu msimu huu unaotarajia kuanza Septemba 12.

Sambamba na mchezaji huyo pia Simba imempa mkataba wa miaka miwili Boniface Maganga kutoka kituo cha soka cha Marsh Athletes Academy kilichokua kinasimamiwa na aliyekuwa kocha msaidizi wa timu ya Taifa, Sylvster Marsh, Mwanza.

N’daw alifuzu majaribio juzi katika mchezo wa kirafiki kati ya Simba ambapo walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 mchezo uliochezwa Uwanja wa Amaan Zanzibar.

Mchezo huo ni wa pili kwa mchezaji huyo tangu atue kwa majaribio, mchezo wa kwanza ulikuwa dhidi ya JKU ambapo Simba ilifungwa mabao 2-0 na mchezaji huyo alionyesha kiwango hafifu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tully, alisema N’daw amesajiliwa baada ya mwalimu kuridhika na kiwango chake hivyo atakuwa ni miongoni mwa wachezaji wao msimu ujao.

“Suala la usajili wa mchezaji lilikuwa chini ya kocha na ameridhika naye, hivyo tumeshakamilisha usajili wetu na majina yameshapelekwa TFF hivyo tuko tayari kwa ligi,” alisema.

Simba imetimiza nafasi saba za wachezaji wa kigeni ambao ni Juuko Murushid, Hamis Kiiza, Simon Sserunkuma, Justice Mayabvi, Vicent Angban na N’daw.

Klabu hiyo iliamua kuachana na mshambuliaji aliyepewa nafasi kubwa kubaki katika timu hiyo Mmali Makan Dembele, kutokana na mchezaji huyo kuchelewa kutua kwenye timu hiyo aliwasili mwishoni mwa wiki iliyopita na kutaka asajiliwe bila kufanyiwa majaribio, kitu ambacho kocha mkuu wa timu hiyo, Dylan Kerr alikipinga.

Wakati huo huo Kerr amesema tayari  kikosi hicho kimeanza kukaa kwenye mstari ulioonyoka hivyo anaamini watakuwa tishio msimu ujao.

Kerr alisema wachezaji wameonyesha mabadiliko katika kambi tofauti na ilivyokuwa awali visiwani humo Julai mwaka huu.

Alieleza kuwa amegundua njia ya wachezaji kujifunza zaidi ni kujenga ukaribu na kupokea maoni yao kila wanapomaliza kucheza mechi za kirafiki.

“Kiwango kinazidi kupanda taratibu naamini tukimaliza kambi kila kitu kitakuwa vizuri, ndiyo maana hivi sasa tukimaliza kucheza mechi ya kirafiki lazima nikutane na wachezaji wangu, kufahamu wapi palipoonyesha mapungufu na kitu gani kifanyike kuhakikisha tunasonga mbele,” alisema Kerr.

Simba inatarajiwa kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu kwa kuvaana na African Sports ‘Wanakimanumanu’, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Septemba 12 mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles