25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

Ndaki: Fanyeni kazi kwa kutanguliza maslahi ya Watanzania

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha sekta hizo zinakua na zinachangia kwa asilimia kubwa katika maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki katika kikao chake na watumishi wa wizara pamoja na baadhi ya watumishi wa taasisi na wakala zilizo chini ya wizara hiyo kilichofanyika katika Ofisi za Wizara zilizopo katika mji wa serikali – Mtumba, jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo wakiwemo wakuu wa taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara (hawapo pichani), wakati wa kikao kilichofanyika kwenye viwanja vya ofisi za wizara hiyo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma na kuwasifu wafanyakazi wa wizara hiyo kwa utendaji wao wa kazi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

Waziri Ndaki alisema moja ya jukumu kubwa walilonalo watumishi wa wizara hiyo, ni kuhakikisha sekta hizo zinakua ili zichangie kwenye uchumi, ziondoe umaskini wa watanzania na kutoa ajira.

“Kila mmoja anapofanya kazi yake ahakikishe anachangia kwenye kutengeneza ajira, kuondoa umasikini wa wafugaji, wavuvi na watanzania wanaoishi kwa kutegemea sekta hizi na ahakikishe anafanya kazi ili uchumi wa taifa letu unapande juu ukichangiwa na sekta za mifugo na uvuvi.

“Wizara inayo mipango mingi sana ambayo imeandaliwa na baadhi yake tumeshapitishwa lakini kwa sasa kinachotakiwa ni sote kwa pamoja kuisimamia kuhakikisha inatekelezeka na inaonekana,” alisema Ndaki.

Kuhusu sekta ya uvuvi amesema kipaumbele ni lazima kiwekwe kwenye uchimbaji wa mabwawa pamoja na ufugaji wa samaki kwenye mabwawa.

Yapo mabwawa mbalimbali yanayotengenezwa kwa ajili ya mifugo, kilimo, umeme na mengine ambapo yangeweza pia kutumika kwa kufugia samaki bila kuathiri matumizi yaliyolengwa huku akisema umefika wakati sasa kuanza kuzungumza na wizara nyingine ambazo zina mabwawa ili ufugaji huo uweze kufanyika.

Ndaki alipongeza jitihada na  kazi nzuri inayofanyika ya kuzuia uvuvi haramu kwani uvuvi huo umekuwa ukileta madhara makubwa hasa pale ambapo wavuvi walikuwa wakitumia mabomu huku akiagiza udhibiti wa uvuvi haramu ni lazima uendelee lakini kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kutoleta migogoro wakati wa usimamizi wa rasilimali za uvuvi.

Kwa upande wa sekta ya mifugo alisema nguvu kubwa inatakiwa kuwekwa kwenye ujenzi wa viwanda vinavyotumia mazao ya mifugo kwani utasaidia kubadilisha aina ya ufugaji kwa wafugaji kwa kuwa watakuwa na uhakika wa wapi soko la ng’ombe bora lilipo na faida zake jambo ambalo litafanya kutotumika nguvu kubwa kuwahamasisha wafugaji kutoka kwenye ufugaji wa ng’ombe wa kienyeji na kuingia kwenye ng’ombe bora.

Aidha, Waziri Ndaki amewataka watendaji wa sekta ya mifugo kuangalia namna ya kuwa na mbegu bora ya malisho ya mifugo ambayo wafugaji watakuwa na uwezo wa kuimudu na kwa kufanya hivyo watakuwa wamewasaidia wafugaji kuwa na malisho ya uhakiki na hivyo kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la wafugaji kuhamahama linalosababisha migogoro na watumiaji wengine wa ardhi.

Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alitumia fursa hiyo kuwataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano kwani ndio njia pekee itakayoisadia wizara hiyo kutimiza malengo yaliyowekwa katika kuhakikisha wafugaji, wavuvi na taifa kwa ujumla linapata maendeleo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa wizara ina watumishi wachapakazi na wenye uvumilivi hivyo ni matarajio yake kuwa ushirikiano uliopo utaendelezwa kwa viongozi wapya huku akisisitiza kuwa mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika sio adhabu wala zawadi kwa mtu yoyote ni majukumu ndivyo inavyobidi yaende.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dk. Rashid Tamatamah asema kikao hicho cha watumishi kimesaidia sana kwani watumishi sasa wamesikia kutoka kwa viongozi wao ni njia ipi itakayotumika katika kufanikisha malengo ya wizara yaliyowekwa.

Pia amewahakikishia Mawaziri kuwa watumishi wa wizara watatumia weledi wao katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles