28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

NCHI IKINYOOKA TUTAHESHIMIANA

john-pombe-magufuliNa Aloyce Ndeleio


MIONGONI  mwa maneno ambayo Rais John Pombe Magufuli amekuwa akiyasema na kuyarudi mara kwa mara ni  yale yanayoonesha nchi ilikuwa  ina mambo ya hovyo hovyo. Amekuwa akiyasisitiza  kwa kuonesha kuwa mambo hayo yalikuwa yanaudhi na kulidhihaki kundi fulani la watu.

Katika mazungumzo yake  na waandishi wa habari hivi karibuni  alipoulizwa masuala kadhaa ndipo aliposema kuwa jukumu  alilonalo hivi sasa ni kuhakikisha kuwa anainyoosha nchi kwanza na mambo mengine yatafuata.

Kwa kutafakari kirahisi tu ni kwamba ameiona nchi hii kwamba ilikuwa imetumbukia katika janga la kulea baadhi ya mambo ambayo yaliwahi kuainishwa na waasisi wa Taifa hili na hususani kumea na kustawi kwa janga la rushwa iliyokomaa  pamoja na vitendo vya ufisadi.

Inapoainishwa mifumo ya uendeshaji wa huduma za kijamii kinachojidhihirisha ni kwamba jamii ilishajengeka katika matabaka ambayo mara zote  yanakuwa ni mawili ya wavuja jasho na wavuna jasho.

Ilishakuwa rahisi kuaminishwa kuwa baadhi ya sehemu za kutoa huduma  za jamii  kwamba ziligeuzwa kuwa ni mapango ya uporaji na utukufu wake ulishadhoofu na kwamba  njia ya kuzifikia huduma hizo zilikuwa zimejaa miiiba na zilikuwa hazipitiki.

Inaweza kuelezwa hivyo kutokana na ukweli kwamba miguu  ya wavuja jasho iliyopeku  haingeweza kumudu kupita na kuzifikia. Lakini ni nani aliyejali  hali hiyo ya mvuja jasho?

Taswira inayojitokeza hapo ni kwamba  lilishajengeka pengo katika ya makundi hayo mawili, na hivyo kuwapo dhana ya kudharauliana, kupuuzana na hata kudhihakiana kutokana na kuwapo kwa tofauti hiyo.

Ukweli mwingine ni kwamba wakati wavuna jasho wakiwa wanapanda ngazi wavuja jasho walikuwa wanashuka ngazi kuelekea ndani ya dunia ya umaskini na hivyo taswira hiyo inaonesha wazi kwamba kati ya wawili hawa hawawezi kushikana mikono. Hilo ni jambo lisilowezekana kwa mpanda ngazi na mshuka ngazi kushikana mikono.

Macho ya wavuja jasho yanapoangalia  mambo yanayojitokeza kwa sasa hata kama hayatawafurahisha wengine kwa upande wa pili wapo watakaokuwa wanaoona ahueni kutokana na dhihaka iliyokuwa imekithiri.

Yapo baadhi ya mambo ya kawaida tu ambayo kila wavuja jasho wanapokumbana nayo huwa wanaamini kweli  aliye juu msubiri chini atashuka tu. Lakini awali ilikuwa aliye juu mfuate huko huko. Hatashuka.

Hivi sasa wavuja jasho wameanza kuiamini ile kanuni ya Kifizikia ya mvutano kwamba  huko wavuna jasho walikokuwa wanaelea hawawezi wakadumu huko lazima watashuka kwa kuwa manyoya ya mabawa yao yameanza kupukutishwa.

Inapoelezwa kuwa wavuna jasho hivi sasa wanajifunza kozi ya kuishi maisha  kwa kuvuja jasho na uzoefu wanautafuta kutoka kwa wavuja jasho ambao wamebobea katika kuishi kwa jasho lao miaka nenda rudi ndipo hapo inajionesha kuwa heshima inarudi.

Zilikuwapo kauli za kukufuru kwamba kutokana na kuvimbiwa jasho walilolivuna na kuwajengea hofu wavuja jasho, ilikuwa ni rahisi kuzisikia kama vile  “unajua mimi ni nani?” na nyingine nyingi ambazo zilitokana na jasho walilovuna kuwa limewakifu.

Kile kinachojulikana kwamba  walikuwapo wavuna jasho  ambao katika sehemu nyingine za huduma walikuwa na vigoda vyao maalumu na  hakuna  aliyeruhusiwa kukalia vigoda hivyo  ni kwamba  hivi sasa vinajulikana kama ni vigoda vya moto hawamudu tena makeke ya kuvikalia. Hilo ndilo linamfanya mvuja jasho achoke na kulegea mwili.

Lakini ukweli unabakia kuwa  ukiona mambo yanaenda hivyo jua kwamba  utafika wakati ambao licha ya  baadhi kutoamini  au kukubaliana na mwenendo wa kuinyoosha nchi  wavuna jasho watafumbuka macho na kuona na kukiri kuwa  walivuna jasho la  wavuja jasho na watawapa heshima inayostahili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles