26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 28, 2024

Contact us: [email protected]

NBS yatoa ufafanuzi juu ya Takwimu za wapiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imethibitisha kuwa idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kwa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, ni sahihi na imetokana na takwimu rasmi za serikali. Tamko hili limefuatia mjadala na taarifa za upotoshaji zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii, zikihoji usahihi wa takwimu hizi.

Akizungumza leo Jumatatu Oltoba 28, 2024 na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, alieleza kuwa taarifa ya wapiga kura inaendana na takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na makadirio ya idadi ya watu ya mwaka 2024, ambayo inakisiwa kufikia milioni 66.3.

“Takwimu zilizotolewa ni sahihi kulingana na vigezo vya kitaifa na kimataifa. Idadi ya wapiga kura wenye umri wa miaka 18 na zaidi, ambayo ni milioni 32.9, imetokana na takwimu za mwaka 2022 na inakubaliana na kanuni za Umoja wa Mataifa kuhusu takwimu rasmi,” alisema Dk. Chuwa.

Dk. Chuwa pia alifafanua kuhusu viwango vya uandikishaji katika baadhi ya mikoa, ambapo Pwani, Tanga, na Mwanza ziliripoti uandikishaji wa zaidi ya asilimia 100 kutokana na uhamaji wa watu.

Alisema, “Ongezeko hili la idadi ya waliojiandikisha katika baadhi ya mikoa ni jambo la kawaida, likisababishwa na watu kuhamia maeneo haya kwa sababu mbalimbali za kiuchumi na kijamii.”

Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara, Anne Makinda, alionya dhidi ya upotoshaji wa takwimu za wapiga kura na kuhimiza umma kuzingatia taarifa rasmi. “Hizi ndizo takwimu rasmi na zina msingi wa kisheria. Takwimu za sensa ndizo msingi wa kupanga maendeleo ya taifa letu,” alisema Makinda.

Ufafanuzi huu wa NBS umekuja wakati ambapo serikali imekuwa ikihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuchagua viongozi wa serikali za mitaa, huku ikisisitiza kwamba zoezi la uandikishaji limeendeshwa kwa kufuata viwango vya juu vya kitaalamu na kimataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles