25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

NAPE: TUTAPATA SHIDA 2020

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), akilia baada ya kutakiwa apite kwenye migongo ya wanawake waliolala chini, wakati akielekea jukwaani kuwahutubia wananchi wa jimbo hilo jana.

Na Florence Sanawa – Lindi

ALIYEKUWA Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema matendo ya utekaji nyara wananchi yasipotatuliwa yatakipa shida Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Nape alitoa kauli hiyo jana, ikiwa ni siku chache baada ya hivi karibuni kukaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa kama si kuingia msituni kwa miezi 28, CCM ilikuwa inaelekea shimoni.

Akiwahutubia wananchi wa jimbo lake la Mtama jana, Nape alitaka hatua zichukuliwe za kukomesha tabia ya utekaji nyara wananchi, huku akikumbushia tukio la kada wa Chadema, Ben Saanane, ambaye amepotea miezi mingi iliyopita katika mazingira ya kutatanisha.

 “Naomba hatua zichukuliwe tukomeshe hii tabia, Ben Saanane amepotea miezi mingi na mazingira ya kupotea ni ya kutatanisha. Matendo haya yasipotatuliwa na kukomeshwa, tutapata shida sana 2020,” alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa matendo ya kuwateka nyara akina  Ben Saanane, Roma Mkatoliki, na wengine yanamjengea chuki Rais Dk. John Magufuli dhidi ya wananchi.

Katika muktadha wa hoja hiyo, alilijumuisha tukio la mtu aliyemtishia bastola hivi karibuni wakati akitaka kufanya mkutano na wanahabari Dar es Salaam, kumshukuru Rais Magufuli kumteua na kisha kumwondoa katika wadhifa wa uwaziri aliokuwa anautumikia.

“Shida niliyonayo huyu aliyetoa silaha vyombo vya dola vinafanya nini? lazima hatua zichukuliwe, Siamini alitumwa kutoa silaha, lakini alifanya upuuzi wake, ndiyo maana sikutishika, niliona kama anatoa ‘mice’… na mimi nilikuwa na bastola kubwa kuliko yake.

“Nilivyofika yule kijana mpuuzi mliyemuona, akasogea karibu yangu. Nikamnong'oneza tuko moja kwa moja na vyombo vya habari vinaangalia,” alisema Nape.
Akizungumzia uvamizi katika kituo cha Clouds, ambao wengine wanahusisha hatua alizozichukua ndizo zilizogharimu uwaziri wake, Nape alihoji akisema: “Wengine wamevamia kituo cha utangazaji, kama siyo yule tunayemwona kwenye kamera basi ni nani?

“Wengine wamevamia studio na kuwachukua watu akiwamo Roma, watu wanapotea kama nzi.”

Aliongeza kwamba Rais anapaswa kuingilia kati vitendo vya utekwaji watu vinavyofanywa pasipo kuchukuliwa hatua yoyote.

Alisema hatua hiyo inaweza kusababisha watu wabaya kuendeleza matukio hayo kwa kuwa yamekuwa hayachukuliwi hatua.

“Rais achukue hatua ili matendo haya yasijirudie, unajua dawa ya moto si moto, wakati mwingine unaweza kuuzima kwa maji.

“Kifua changu kina mengi sana, siwezi kuyasema, lazima mkumbuke kuwa Rais Magufuli nimemtafutia kura mimi mwenyewe,” alisema Nape.

Akizungumzia uamuzi wa Rais Magufuli kumtengua katika wadhifa wa uwaziri, Nape alisema uamuzi huo ni mabadiliko ya kawaida kwa mujibu wa katiba ya nchi.

 “Nilitumia nguvu zangu zote kuhakikisha dhamana niliyopewa naitendea haki, Rais Magufuli alisema amefanya mabadiliko ya kawaida na ni kwa mujibu wa katiba yetu. Mara nyingi ukiwa na mchezaji mzuri na amefunga magoli mengi, unampumzisha ili acheze kesho.

“Wapo waliosema Nape usiende kuzungumza Mtama, lakini siwezi kuwaacha wananchi wangu na maswali yasiyo na majibu… tusimnunie kocha aliyebadilisha wachezaji,” alisema Nape.

Hata hivyo, Nape alikwenda mbali zaidi kwa kuwasihi wananchi wasiyumbishwe na cheo.

Katika hili, alisema ni bora kuyumbishwa na msimamo ambao umewekwa na wananchi.

Zaidi aliwaasa vijana kusimama imara kuusemea ukweli.

Alisema Tanzania bado itakuwa salama kama vijana watasimama kuusemea ukweli.

Katika hatua nyingine, Nape alizungumzia uhusiano wake na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akisema wao sasa ni kitu kimoja.

“Kama mimi na Lowassa tuna kunywa chai sasa, nyie mnanuniana nini? Sisi ni kitu kimoja,” alisema Nape.

Kauli hiyo ya Nape inatoa tafsiri ya kwenda kinyume na mrengo wake wa siku nyingi wa kutomkubali Lowassa kwa jambo lolote.

Wakati akitumikia wadhifa wa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape alisikika mara kadhaa akitoa kauli chafu dhidi ya Lowassa na mara nyingi alisikika akimfananisha na Oil chafu au marehemu anayetembea.

ALIVYOPOKEWA

Nape alipokewa na umati wa wananchi waliokuwa wakiburudishwa kwa wimbo wa ‘Nyota na ing’are’ wa Peter Msechu.

Katika mapokezi hayo ya aina yake, Nape alitembea kwa kupita juu ya migongo ya akina mama  zaidi ya 10 waliokuwa wamelala  kifudifudi chini kwenye njia ya kuelekea jukwaa kuu.

Wakati Nape akipita juu ya migongo ya akina mama hao, alishindwa kujizuia na badala yake alijikuta akibubujikwa na machozi hali iliyoibua tafsiri ya aidha alikuwa na furaha au hasira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles