24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MAJANGILI WAPATA PIGO

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe

NA MWANDISHI WETU,

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, ameipongeza China kwa kufunga masoko yake ya ndani ya pembe za ndovu kabla ya mwishoni mwa mwaka huu.

Hatua hiyo inatajwa kuwa ni pigo kwa majangili waliokuwa tishio kwa taifa kila kukicha kutokana na matukio ya mauaji ya wanyama, hasa tembo.

Machi, mwaka huu, China ilitangaza kufunga masoko ya ndani ya biashara ya pembe za ndovu, ikiwamo viwanda vilivyozalisha bidhaa zitokanazo na malighafi za pembe hizo.

Kupitia taarifa iliyotolewa Dar es Salaam juzi na Profesa Maghembe, hatua ya China kufunga masoko yake ya ndani ni mojawapo ya jitihada kubwa za kulinda wanyama hao.

Pamoja na kuishukuru Serikali ya China kwa hatua hiyo, pia alisema soko la kimataifa la bishara ya pembe za ndovu limeshuka kwa kiasi kikubwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita hali inayoashiria mafanikio makubwa katika kipindi kijacho.

“Tunaishukuru China, leo (juzi) ni siku muhimu, ni siku kubwa baada ya viwanda 67 vya China kufunga milango ya biashara ya pembe za ndovu. Katika kuanza mwaka huu, mfuko wa hifadhi unasherehekea msimamo wa China wa kufunga soko lake la ndani la biashara hiyo ya pembe za ndovu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Hii ni hatua kubwa mbele yetu.

“Matunda yameshaanza kuonekana katika jitihada zetu na dunia katika kuzuia ujangili. Ukweli umedhihirishwa pia na rafiki zetu wa Taasisi ya Save the Elephant ambayo katika utafiti wake imeonyesha biashara ya pembe za ndovu imeshuka kwa kiwango kikubwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Kwa wastani wa bei ya kimataifa, imeshuka kutoka Dola 2,100 za Marekani kwa kilo moja mwaka 2014 hadi Dola 730 za Marekani kwa kilo moja kwa sasa.

“Haya ni mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika biashara hii na ni alama ya mafanikio huko tuendako. Asante China, asante kwa kila mmoja aliyesaidia kwa bidii kuokoa tembo,” alisema Maghembe.

Baadhi ya takwimu katika mapori ya akiba na hasa ripoti ya sensa ya mwaka juzi, inaonyesha kuwa Mbuga ya Selous idadi ya tembo ilikuwa ni 13,084 wakati kwa mwaka 2009 ilikuwa ni 38,975.

Hifadhi ya Ruaha nayo inaonyesha kupoteza nusu ya tembo wake kutoka 8,500 waliokuwapo mwaka 2014 hadi 4,200 waliopo hadi mwaka juzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles