25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Nape afunguka tukio la kutishiwa kwa bastola

MAREGESI PAUL-DODOMA

MBUNGE wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), amezungumzia kwa mara ya kwanza tukio la kutishiwa bastola lililotokea jijini Dar es Salaam, miaka miwili iliyopita.

Nape alizungumzia tukio hilo bungeni juzi usiku, wakati Bunge lilipokuwa limekaa kama kamati kujadili bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Pamoja na mambo mengine, Nape aliwasilisha hoja hiyo wakati wabunge walipokuwa wakijadili hoja ya Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), aliyekuwa ameondoa shilingi kwenye mshahara wa waziri baada ya kutoridhishwa na majibu ya Serikali kuhusu wananchi wanaouawa, wanaopotea, wanaopigwa risasi na wanaoteswa katika mazingira ya kutatanisha.

“Mwenyekiti, hili tukio la mimi kutishiwa kwa bastola limekuwa likisemwa sana, lakini ni muda mrefu nimekuwa kimya kwa miaka miwili sasa.

“Mwenyekiti, kwa kweli kufanya siasa katika maisha ya watu si busara kabisa.

“Nakumbuka siku natishiwa, alikuwepo OCD wa wilaya, alikuwapo RPC, lakini kwa bahati mbaya tangu tukio hilo litokee, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya aliyehusika ingawa anajulikana.

“Aliyeninyooshea bastola namfahamu, lakini tangu wakati huo hakuna hatua zozote alizochukuliwa kama nilivyosema.

“Binafsi naamini mtu huyo hakutumwa na Serikali bali alifanya vile kwa ujinga wake. Kwa hiyo naiomba Serikali ijitenge na matukio ya aina hii na wale inaowatuma wawe wanafanya mambo kwa kutumia akili,” alisema Nape na kukaa.

Awali, Msigwa alipokuwa akiwasilisha hoja yake, aliitaka Serikali itoe taarifa za watu waliowahi kupigwa risasi, kuteswa na waliowahi kutekwa katika mazingira ya kutatanisha.

Kwa mujibu wa Msigwa, kitendo cha Serikali kukaa kimya juu ya matukio hayo, kinatia shaka jinsi inavyoshughulikia matukio hayo na kwamba ukimya huo unachochea mwendelezo wa matukio hayo.

Katika hoja hiyo, Msigwa, aliungwa mkono na baadhi ya wabunge wa Chadema wakiwamo Esther Matiko wa Tarime Mjini, Joseph Selasini wa Rombo, John Heche wa Tarime Vijijini, Sofia Mwakagenda wa Viti Maalumu na Ally Salehe wa Malindi (CUF).

Hata hivyo, Mbunge wa Serengeti kupitia CCM, Chacha Ryoba, aliwashangaa wabunge wa Chadema kwa kile alichosema kwamba pamoja na kutaka Serikali ieleze hatua ilizochukua juu ya matukio mbalimbali ya uhalifu, wao walimficha dereva wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), wakati ndiye shahidi muhimu katika tukio la mbunge huyo kupigwa risasi mjini Dodoma.

Akizungumzia mjadala huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alisema matukio yote ya uhalifu nchini yamekuwa yakifunguliwa majalada kwa ajili ya kuyafanyia kazi kabla hatua nyingine hazijachukuliwa.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wabunge wasiwe na wasiwasi kwa kuwa hakuna kiongozi yeyote anayefurahi pindi watu wanapofanyiwa uhalifu wa aina mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Kangi alizungumzia kauli ya watapigwa hadi watachakaa iliyotolewa hivi karibuni na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Dodoma, Gilesi Muroto, alipozungumzia maandamano yaliyopangwa na wanachama wa Chama cha ACT-Wazalendo hivi karibuni.

“Kuna waheshimiwa hapa wanalalamikia kauli ya Kamanda Muroto aliposema watapigwa hadi watachakaa.

“Hiyo si kauli mbaya hata kidogo, hiyo ni kauli ya kipolisi ila wasiokuwa askari hawawezi kuielewa ndiyo maana wanalalamika,” alisema Kangi.

Akizungumzia mikutano ya hadhara ya kisiasa na mikutano ya ndani, Kangi alisema wapinzani wanalilaumu Jeshi la Polisi kwamba linawanyanyasa na kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa hawataki kufuata sheria.

Kutokana na hali hiyo, alimwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro, aendelee kudhibiti mikutano yote itakayoitishwa bila kufuata utaratibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles