29.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 19, 2022

Kimbunga Kenneth chayeyuka

AZIZA MASOUD NA FLORENCE SANAWA, DAR ES SALAAM/MTWARA

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi, amesema kimbunga cha Kenneth kwa sasa kipo katika ardhi ya Msumbiji na hakitarajii kutua nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana jioni, alisema kimbunga hicho nchini Msumbiji kimeenda Kusini zaidi kwa longitudi 39.6 wakati kasi ya upepo ikiwa ni kilomita 70 kwa saa na mzunguko wa athari ukionyesha kupungua na kufikia kilomita 200 ambazo haziwezi kufikia katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji.

“Utabiri wa mwanzo ulionyesha kitafika kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji lakini kwa leo (jana) kimbunga kipo ndani ya ardhi ya Msumbiji kipo longitudi 39.6 Mashariki, Kusini latitudi 12.4, upepo kilomita 70 kwa saa na mzunguko umepungua na kufikia kilomita 200.

“Kutokana na hali hiyo maeneo ya Mtwara kwa sasa hali ni shwari bali kuna upepo wenye unyevunyevu kutoka eneo la Magharibi lenye Misitu ya Kongo, ina maana kama kuna baadhi ya maeneo yaliyopo Magharibi na Ziwa Victoria wataweza kupata mvua zisizo za msimu  kidogo na tayari utabiri unaonyesha kuna mawingu katika maeneo hayo,” alisema.

Akizungumzia athari za kimbunga hicho, alisema wakati Tanzania kulikuwa na  upepo kadiri kilivyokuwa kinaongezeka na kufikia kiwango cha juu cha kilomita 60 kwa saa zilizokuwa na mawimbi makubwa katika Mji wa Mtwara, lakini Msumbiji ilikuwa tofauti.

“Taarifa tulizozipata kutoka kwa wenzetu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa ya nchi hiyo zinaonyesha kuwa katika mji wa Moeda kilipiga milimita 194.6,” alisema.

Dk. Kijazi alisema katika Mji wa Muidun napo kilipiga kilomita 86.5 wakati Mji wa Ilhadoido kilipiga milimita 133.7 katika saa 24 na kusisitiza kuwa uharibifu wa miundombinu umetokea katika maeneo ya Mji wa Pemba nchini humo.

Alisema mbali na Msumbiji nchi nyingine iliyopata athari ni Comoro ambako kuna maeneo yameharibika.

Alisema pamoja na kwamba kimbunga hicho kipo maeneo ya Msumbiji, lakini matazamio ya utabiri yanaonyesha kuwa  kitageuka tena na kuingia baharini.

“Kwa kawaida kimbunga kikiingia baharini tena kinapata nguvu kwa sababu ili kiwe na nguvu kinahitaji joto la bahari ambalo linazidi nyuzi joto 26, kikipata nguvu kinaongezeka na kuwa kimbunga maana kwa wakati huo kitakuwa si kimbunga kamili tena kinaitwa EX –Keneth, hii inatokea kitaalamu baada ya kuwapo kwa mkandamizo mdogo,” alisema.

Dk. Kijazi alisema kutokana na utabiri huo, TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na endapo kitarudi tena watatoa taarifa kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Said, alisema endapo kimbunga hicho kingefika nchini kingeathiri halmashauri 11 pamoja na watu wasiopungua 1,175,000.

Alisema kitendo cha wananchi kufuata maelekezo yaliyokuwa yanatolewa nacho kimepunguza athari ndogo ndogo ambazo zingepatikana kupitia upepo wa kilomita 60 uliokuwa unapiga kwa saa.

“Utii wa wananchi tumeweza kuokoa wananchi na wavuvi, kamati za maafa nazo za mikoa zinapaswa kuwa tayari wakati wote na kwa kuwa unaweza kutumia gharama ndogo katika kujiandaa na kutumia gharama kubwa katika kukabiliana kurejesha hali kama ulikuwa haukujiandaa,” alisema Kanali Saidi.

Alipoulizwa kuhusu maandalizi yaliyofanywa na Serikali kukabiliana na kimbunga hicho ikiwamo kutokuwapo kwa huduma muhimu katika maeneo ambayo wananchi walitangaziwa kukusanyika, alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kuahidi kulifanyia kazi.

“Katika tukio hili tumeona pengo na tutalifanyia kazi, yaliyotokea ni kasoro na ni somo kwetu pia,” alisema Kanali Saidi.

HOFU

Awali, kutokana na utabiri wa kimbunga hicho uliotolewa na TMA, hofu iliendelea kutanda maeneo ya Mtwara Mjini na wananchi walionekana wakitembea kando ya barabara wakielekea katika maeneo yaliyoandaliwa ikiwemo majengo, Tandika, Mang’amba na Naliendele na Uwanja wa Ndege kwa ajili ya tahadhari huku baadhi wakipuuzia taarifa hizo.

Saa 12 asubuhi, baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani walionekana kando ya barabara wakiwa na mabegi huku wengine wakiwa katika pikipiki na magari wakielekea maeneo mbalimbali yaliyoandaliwa.

Huku mvua zilikuwa zikinyesha kwa kasi ndogo na upepo ukiwa katika kasi inayokadiriwa ya kawaida kwa saa na ilipofika saa sita mchana wingu zito lililokuwepo lilipotea.

Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda, alisema baadhi ya wananchi walionekana kukaidi na kupuuzia taarifa hizo jambo linaloweza kuleta madhara kwao endapo kimbunga hicho kingetokea.

“Unajua wapo watu wanabisha na hawaamini hizi taarifa za uwepo wa kimbunga, wanapaswa wajue kuwa kikitokea si kama kawaida, kina msukumo mkubwa na kina athari kwenye majengo, miti na kusababisha madhara makubwa ni vema tahadhari ikachukuliwa.

“Yapo maeneo mengi tuliyotenga wananchi wameitikia, lakini tunaamini kuwa wapo wazee na wagonjwa tunajitahidi ili waweze kufika katika maeneo hayo kutokana na umbali uliopo,” alisema Mmanda.

Naye mkazi wa Magomeni Manispaa ya Mtwara Mikindani, Moza Kazumali, aliyekimbilia Shule ya Msingi Majengo, alisema Watanzania wanapaswa kuacha kudharau maagizo ya wataalamu.

Alisema kuchukua tahadhari kunaweza kuwasaidia watu wengi kutokana na majanga mbalimbali ikiwamo hili la kimbunga tunalopaswa kuchukua hatua na kuacha kudharau.

“Unajua lazima uwe na wasiwasi, tunaona nchi nyingine hali inavyokuwa mbaya wanapopata majanga mbalimbali ya uwepo na kimbunga, tumeona viongozi wetu wametutahadharisha lazima tuwe makini wakati mwingine ubishi sio mzuri, ni vema elimu ikatolewa kwa wananchi ili kufahamu,” alisema Kazumali.

Naye mkazi wa Chuno Manispaa ya Mtwara Mikindani, Michael Onesmo, alisema kutokana na taarifa hizo amelazimika kuhama kwa muda ili kujinusuru na janga la kimbunga.

“Sisi kwa kweli tumefunga nyumba hatuwezi kusikia taarifa za wataalamu tukazipuuzia hata viongozi nao wametusihi bado tukaidi, haiwezekani tukipata majanga sisi ndio tunalalamika, ni vema elimu ikatolewa na tukajenga utamaduni wa kupokea taarifa na kuzifanyia kazi,” alisema Onesmo.

Isaiah Dadi ambaye ni mkazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani aliyekimbilia Uwanja wa Ndege, alisema wapo watu wameshaanza kupata madhara ya upepo huu ikiwemo bati kuezuliwa jambo lililowafanya baadhi ya majirani kutoka na kuelekea maeneo yaliyotengwa.

“Mwanzoni nilipopata taarifa nilipuuzia,  nilikuwa moja kati ya watu waliodharau hili jambo, lakini nilipoona jirani kumeanza kuathirika nilikimbia mwenyewe, nashauri watu wasipuuzie jambo hili, linaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii,” alisema Dadi.

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mtwara, Christina Sunga, alisema wananchi wanapaswa kukusanyika maeneo yaliyotengwa ili kutoa huduma kwa urahisi endapo janga litatokea.

“Lengo la kuwakusanya wananchi inakuwa rahisi kuwasaidia tofauti na kuwaacha kila mmoja akiishi kwake, wapo wanaoishi katika mazingira hatarishi, lakini bado wako majumbani tuwasihi ili kuwasaidia endapo janga litakuwa kubwa wapate msaada kwa ukaribu zaidi.

“Unajua kila mwananchi akiwa kwake itakuwa ngumu kuwasaidia, Serikali haitaweza kumsaidia kila mmoja nyumbani kwake endapo maji yatakuwa mengi wananchi wanapaswa kutembea pembezoni mwa nyumba ili kuwanusuru na majanga ya maji tunafahamu,” alisema Sunga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,987FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles