Windhoek, Namibia
RAIS wa Namibia, Hage Geingob amelalamikia kucheleweshwa mabadiliko ya sheria za umiliki wa ardhi kwa ajili ya kuwalipa wamiliki wa kizungu fidia inayostahili.
Akihutubia taifa hilo katika maadhimisho ya miaka 27 ya uhuru, Geingob alisema serikali imetumia kila mbinu kuwapa ardhi Waafrika kwa kutoa fursa kwa wale wanaouza na kununua kwa hiari.
Geingob amesema serikali itaitumia katiba ambayo inaruhusu kuchukuliwa ardhi na kulipa fidia inayostahili.
Umiliki wa ardhi ni suala lenye utata ukanda huo na Serikali ya Zimbabwe pia imekuwa ikilaumiwa na upinzani na mataifa ya nje kwa kuchukua ardhi iliyomilikiwa na wazungu.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ametoa wito ya kuwanyang’anya ardhi bila ya kulipa fidia.