Na WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM
NAHODHA wa timu ya Gwambina, Jacob Massawe, amesema imetosha kwa mechi nne walizopoteza na hawatarudia makosa katika mchezo wa kesho dhidi ya Ihefu FC utakaochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Katika michezo minne ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyocheza, Gwambina ilipanda daraja msimu huu, haijapata ushindi hata mmoja na haijafunga bao lolote.
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa simu kutoka Mwanza, Massawe, alisema kuna kitu kikubwa wamejifunza katika michezo hiyo ya mwanzo na wamekifanyia kazi kuelekea mechi ijayo.
Alisema kuwa mashabiki wa Gwambina wasife moyo na kuahidi kuanza kuwapa raha katika mchezo wa kesho na mingine inayoendelea.
“Matokeo tuliyopata katika mechi zetu zilizopita nakiri kweli si mazuri na yanatuumiza hata sisi wachezaji, lakini mashabiki wetu watambue ni hali ya mchezo wa soka.
“Mchezo ujao tutacheza nyumbani japo tutatumia uwanja wa CCM Kirumba, naahidi hiyo ndiyo itakuwa mechi ya kuturudisha katika mstari, tumekaa wachezaji na kujiuliza nini cha kufanya naamini ushindi tutapata,” alisema.
Alieleza kuwa yeye ni mzoefu wa ligi na kilichokuwa kinawakumba ni changamoto ambazo zinarekebika kulingana na makosa.